Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii na nianze kusema naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Spika, vilevile napenda kusema kwamba ajira yangu ya kwanza ilikuwa kwenye sekta hii ya nishati na madini. Kipekee kabisa napenda kumshukuru yeye mwenyewe Waziri Kalemani, Mheshimiwa George Simbachawene, Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo pamoja pia na Mheshimiwa Jenista Muhagama kwa ulezi bora walionipa hadi kufikia hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia eneo la usambazaji wa gesi nchini. Wengi tunafahamu kwamba TPDC haitekelezi zoezi la usambazaji wa gesi nchini kwa kasi inayotakiwa vilevile nchini Kenya na Uganda wanahitaji kununua gesi kutoka kwetu. Napenda kugusia Sheria ya Oil and Gas Revenue Management ya 2015 ambayo Bunge lako Tukufu liliipitisha.

Mheshimiwa Spika, kwenye sheria hii ilikuwa imesema kwamba kutakuwa kuna mfuko maalum ambapo fedha zile zitatumika kuendeleza sekta ya mafuta na gesi nchini. Hivi sasa tunapoongea kutokea 2015 mpaka sasa mfuko huu una takriban shilingi za kitanzania bilioni 400 ambazo zimekaa tu kwa sababu kwenye sheria kiliwekwa kifungu kwamba fedha ile haiwezi kutumika mpaka mfuko ufikie asilimia 3 ya GDP.

Mheshimiwa Spika, itatuchukua muda mrefu sana kwa mfuko ule kufikia hiyo asilimia 3 na ndicho kiwango cha zaidi ya asilimia 3 ndipo ambapo TPDC itaruhusiwa kutumia kwa ajili ya kuwekeza kwenye mafuta na gesi asilia. Kwa hiyo, kwa unyenyekevu mkubwa sana napenda kumshauri Mheshimiwa Waziri ailete ile sheria hapa Bungeni ifanyiwe maboresho ili sehemu ya ile shilingi bilioni 400 ambayo sasa hivi imekaa TPDC waweze kuitumia ili waweze kuendeleza miundombinu ya gesi, usambazaji wa gesi lakini pia kuuza gesi hii nchini Kenya na Uganda jambo ambalo litaendelea kutupa rasilimali fedha ambayo tunahitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wengi tunaendelea kulalamika kwamba TPDC ipewe fedha lakini tofauti na REA mfano Wizara inatoa kiwango cha fedha kwenye REA lakini TPDC haipewi fungu lolote kwenye hili eneo la uendelezaji wa hii miundombinu kwenye sekta ya gesi asilia. Kwa upande mwingine tunayo shilingi bilioni 400 ambayo imefungwa kutokana na kile kifungu cha sheria. Kwa hiyo, naomba sana kwa unyenyekevu Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atuambie ni lini ataweza kutuletea maboresho ya ile sheria ili sisi kwa umoja wetu tuweke vifungu na maelekezo ya namna gani ambavyo TPDC itaweza kutumia sehemu ya fedha iliyopo ili isiendelee kukaa huku na sisi tunaendelea kupoteza mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia, naomba niongelee Mkoa wangu wa Kagera. Sisi Mkoa wa Kagera toka Uhuru mpaka leo hatujawahi kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa tunategemea umeme wa Uganda na uhitaji wa umeme Uganda nao umezidi kukua kiasi kwamba hata na wao wananunua umeme kutoka kwetu. Kwa hiyo, napenda kupata kauli ya Mheshimiwa Waziri ni lini sisi Mkoa wa Kagera tutaunganishwa kwenye Gridi ya Taifa kwa sababu hali ilivyo sasa kuendelea kutuweka gizani; moja ni hatari kwa sababu sisi ni mkoa wa mpakani, lakini pili unaendelea kudhoofisha ukuaji wa uchumi wa Mkoa wetu wa Kagera. Kwa kuzingatia kwamba sisi ni mkoa wa mpakani na ni hatari kuendelea kutuweka gizani, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atupe uhakika ni lini atatuletea Gridi ya Taifa mkoani Kagera tukizingatia imeshafika mpaka jirani yetu Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru sana naunga tena mkono hoja. (Makofi)