Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika Bajeti ya Wizara ya Niashati.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kukushukuru sana kwa message uliyotoa kwa vijana wetu ni nzuri sana wakaifanyie kazi. Cheti siyo issue, issue ni Maisha, kwa hiyo, mnasoma mpate vyeti ili muingie kitaa mpige kazi siyo kung’ang’ana kutuma CV kwa Wabunge kutafutiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri aliyoifanya. Wabunge wote tuliomo humu hakuna Mbunge amepata kura bila kutaja Wizara ya Nishati, hasa upande wa umeme. Ni kazi nzuri, tunaendelea kumwombea Waziri pamoja na wataalam wote wafanye kazi bila kuogopa, najua mtapigwa mishale, lakini sisi Wabunge tunawategemea maana 2025 tutategemea tena kuisema vizuri kulingana na ile ahadi waliyosema watamaliza vijiji vyote.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili niseme kuhusu suala la Bwawa la Mwalimu Nyerere. Niwapongeze sana Serikali na Waziri, sisi kama Kamati tulienda kutembelea mradi ule. Ni heshima kubwa sana, asilimia 85 ya mradi wasimamizi wake ni wazawa. Hii ina tafsiri nzuri, baadaye tutakapoanza kujenga mabwawa yetu mengine tutakuwa na wataalam waliobobea ambao tumewajengea uwezo kwa kuwapa zile nafasi za kusimamia mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la tatu naomba nizungumzie suala la depot za mafuta. Ndiyo maana mimi huwa nikisema humu kuna watu wananipiga mishale, sisi Watanzania ni wazuri sana kupanga mipango; Serikali iliamua kupanga mipango na kuwahamasisha wawekezaji wa ndani kwamba mnataka kuwa na depot Mtwara na depot Tanga ili kupunguza msongamano wa malori Dar es Salaam, lakini pia kulinda hata barabara zetu kule Dar es Salaam, mkahamasisha watu wakawekeza Mtwara na Tanga na Serikali Mheshimiwa Rais na viongozi wote wakubwa wameenda kukagua depot zile. Cha kushangaza baada ya wazawa hawa ku-invest kwenye hizo depot, wamekopa benki, Serikali imewatelekeza. Katika mpango mliokuwa mmepanga na tulipitisha sheria hapa kwamba mafuta sasa yatanunuliwa kikanda; Kanda ya Kaskazini watanunua depot ya Tanga, Kanda ya Kusini watanunua depot ya Mtwara, lakini hata yale mafuta yanayoenda nje ya nchi kwenye nchi zinazopakana na Tanzania baada ya ku-invest mpango huu umekufa, watu wamekopa hela kwenye mabenki sasa wako taabani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikuombe Mheshimiwa Waziri ile sheria tuliyoipitisha hapa ya kwamba mafuta yauzwe Kikanda, depot zipo na Serikali ninyi ndiyo wajibu wenu mlileta mpango huo mkawaingiza chocho wafanyabiashara, ni lini mnaanza kuusimamia mpango huu? Sheria na fine tulishapitisha hapa Bungeni watu waende huko, hata nchi kama Rwanda na Uganda mnaweza mkawapeleka Tanga wale wanaotoka Msumbiji wakaenda Mtwara. Hii mnakuza na miji mingine, unapopeleka malori zaidi ya 1,000 unafungua fursa za ma-guest na vitu vingine na hii inasaidia hata hiyo mikoa iliyoko pembezoni kuwa na uchangamfu. Mungu hakufanya makosa kutupa ziwa na tukaligawa katika bandari hizi tatu, nashauri sana Mheshimiwa Waziri akija hapa aje na majibu sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini suala lingine, tulienda kukagua sehemu ya uagizaji wa mafuta kwa pamoja (PBPA), ukiangalia kwa mwaka mzima kampuni za nje tu ndiyo zinachukua kazi hiyo, sisi kampuni za Tanzania tumekuwa kama wasindikizaji. Sababu ni nyepesi, mwanzoni walikuwa wanaagiza kwa pamoja na kampuni zote zilikuwa zinatakiwa ziwe ni za Watanzania, lakini baadaye sheria ikabadilika kwamba tuingize na kampuni za kimataifa, kampuni nyingi zinazo-bid na kushinda ni kampuni za nje lakini zina kampuni za kitanzania, hazitumii kuomba kwenye kampuni za kitanzania zinatumia kampuni za nje. Sasa wanaposhindana na Watanzania, Mtanzania ana mkopo wa asilimia 14 wa CRDB, hawa wenzetu wana mkopo wa asilimia 1 benki za nje. Cha kushangaza zaidi ikitokea Mtanzania umeshinda baada ya kulipa kodi zote za mafuta unatakiwa ulipe income tax na service levy, mtu akishinda na kampuni ya nje halipi income tax wala service levy. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikuombe sana, mimi niko kwenye Kamati hii, hiki kitu hakiwezekani Mheshimiwa Waziri lazima abadilishe sheria, atenganishe sehemu waagize wazawa na sehemu nyingine waagize hao wa nje. Ama zile kampuni za nje watumie zile kampuni zake za ndani ili Serikali iweze kukusanya kodi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, naomba sana wapangaji muwe mnanipanga siku ya kwanza. Hizi dakika tano mashine inachemka, naambiwa ahsante. Nakushukuru Mheshimiwa. (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Musukuma. Mheshimiwa Joseph Zacharius Kamonga atafuatiwa na Mheshimiwa Benaya Kapinga.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.