Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nitajikita katika kusisitiza umakini, usimamizi kwenye mikataba yetu kwa maslahi ya Taifa letu, hatuhitaji kujikwaa tena, lakini viporo tulivyoviacha lazima tuvifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wewe unajua mwaka 1997 Kampuni ya SONGAS ilianzishwa kama kampuni binafsi ambapo Serikali tulikuwa tuna hisa ya asilimia 40 na kampuni hii ilikuwa inafua umeme kutoka katika visima vya gas vya Songosongo. Sasa tunajua kwa nini Serikali iliamua kuingia ubia ni kutokana na tatizo kubwa la umeme ambalo iliikumba Taifa letu miaka ya 1990 mpaka 2000.

Mheshimiwa Spika, lakini kutokana na kusuasua na sintofahamu kutokea kutokana na uhalali wa hisa na mali za Serikali katika uwekezaji huu. Bunge lako Tukufu kupitia kamati inayohusiana na masuala ya nishati mwaka 2008 ilitoa taarifa kwamba mradi huu hauinufainishi Taifa letu, Serikali yetu inapunjwa na ikapelekea CAG kufanya uchunguzi. Moja ya mambo yaliyobainika ni kwamba mbali ya uwekezaji wa Serikali ya Tanzania wa asilimia 40 TANESCO ilihamisha mali na madeni kwenda kwenye kampuni ya SONGAS. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mali ambazo zinazohamishika zilikuwa na thamani ya dola za Kimarekani milioni moja, lakini pia mali zingine ni sehemu ya Ubungo Complex, mali zingine ni sehemu ya ardhi iliyokuwa inajengwa bomba la gas kupeleka kwenye Kiwanda cha Saruji Wazo. Lakini vilevile makubaliano yalikuwa yanasema SONGAS ilipe deni la mkopo lenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 45.88 hadi tunapozungumza leo SONGAS hawakuamisha lile deni, zile pesa, lile deni linalipwa na TANESCO kupitia capacity charge kwenye ankara ya kila mwezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na hii CAG amesema kwa sababu TANESCO inaendelea kulipa lile deni wenyewe Serikali yetu ingeongeza thamani kwenye mradi na tungekuwa tuna hisa, lakini mpaka tunavyozungumza hili halijafanyika, mbali na kamati yako, Kamati ya Bunge inaisimamia Serikali kutoa maoni mbali na CAG tunapata kigugumizi wapi kulinda mali ya nchi yetu na mkataba unaturuhusu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na kipindi hichohicho tuliingia mkataba na makampuni 936 katika kuhakikisha tunazalisha umeme wa dharura na makampuni yale uchunguzi ulivyofanyika ukaonyesha kabisa yalikuwa na gharama kubwa mpaka tunavyozungumza, mpaka 2018 kutokana na mikataba ile ya makampuni yale 936 TANESCO imekuwa na deni la bilioni 938. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini cha kushangaza kati ya makampuni 936 yaliyofanyiwa uhakiki ni makampuni 23 ambayo yenye thamani ya deni ya bilioni 643 hivi tunavyozungumza IPTL yenyewe imeshindwa kuthibitisha deni la bilioni 1.2 hivi tunavyozungumza makampuni 913 yameshindwa kuthibitisha deni ya bilioni 291, tujiulize kama Taifa tuna wanasheria, tujiulize kama Taifa hata kama tunapata crisis lazima tuwe makini katika kuingia mikataba, tuwe makini katika kuhakikisha mbali na kutatua tatizo tusiingie gharama kubwa hizi pesa zingeenda kumaliza miradi ya umeme vijijini, hizi pesa inawezekana tungepeleka katika miradi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kaka yangu Dkt. Kalemani nenda kamalize haya madudu yanatia aibu na inafanya TANESCO lishindwe kujiendesha, lakini tukija kwenye madeni bado sijazungumzia deni la TPDC la bilioni 246, Mheshimiwa Dkt. Kalemani unajua, hili deni tena la TPDC hili deni CAG amesema shirika letu linaweza likaporwa mali na Benki ya Exim ya China kwa kushindwa kulipa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini wakati hii TPDC ni shirika la Serikali, Serikali wenyewe mnadaiwa, mnadaiwa na TANESCO bilioni 258, ili kulikomboa shirika letu mngeweza tu kwenye lile deni mnalodaiwa mngewalipia hawa TPDC hiyo bilioni 240 na, bilioni 9 inayobaki mngewapa TANESCO. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nije kwenye uzembe wa kusimamia mikataba hata kama inatulinda. Mwaka 2004 Serikali iliingia mkataba na Kampuni ya PANGEA kwa ajili ya kutengeneza miundombinu ya umeme kwenye mgodi wa Buzwagi. Kwenye makubaliano ya ule mkataba ilikuwa kwanza wafungue benki ya pamoja kwa sababu kwenye makubaliano TANGEA walikuwa wanakata dola 5000 mpaka 3500 katika kila nusu saa ya ankara ya mwezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ninavyozungumza mpaka sasa hivi na yale makubaliano ili zile pesa ziende TANESCO, hivi tunavyozungumza na lengo lake lilikuwa kufanya miundombinu ikitokea hitilafu hivi tunavyozungumza takribani miaka kumi benki ya pamoja haijafunguliwa zile pesa zilikuwa zinaingia kwenye akaunti ya PANGEA na TANESCO ilikuwa inafanya ukarabati kupitia pesa zake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunavyozungumza bilioni kumi TANESCO haijalipwa aibu na hii tabia ya kutosimamia makubaliano ya pesa zetu wenyewe mikataba tunayoingia tunapata kigugumizi gani tunawaogopa wawekezaji wakati mikataba inatu- favor haya hata mikataba yetu wenyewe Mheshimiwa Waziri unajua TANESCO haijaingia makubaliano ikaenda kufanya ukarabati wa Mkongo wa Taifa na mpaka sasa hivi inaidai Wizara ya Mawasiliano bilioni nane hakuna mkataba na mpaka juni 2020 CAG anasisitiza ingieni mikataba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Waziri lazima tufanye uchunguzi kwenye mitambo yetu ya kuzalisha umeme. Mtambo wa Kinyerezi I na Kinyerezi II ilijiwekea malengo ya kuzalisha Megawatt 398, lakini hivi tunavyozungumza malengo hayajatimia wamezalisha Megawatt 290, nenda kule Mwanza - Nyakato najua una mradi kule ilikuwa izalishe Megawatt 63, lakini wamezalisha Megawatt 36 hiyo ni miradi miwili ukijumlisha hapo ni Megawatt 155 zimepotea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na hii yote wanasema ni tatizo la mitambo, huu wa Nyakato wanakwambia ni tatizo la, kulikuwa na matatizo kwenye mashine nne sasa hii ukienda haya matatizo ya kiufundi, matatizo ya kiufundi kwenye miradi mingi hivi ni Megawatt ngapi ambazo tunapoteza. Sasa Mheshimiwa Waziri haya ni mambo ya msingi ya kwenda kuyaangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ningependa kuzungumzia Mheshimiwa Waziri tatizo la mita kwenye mita kuu ambazo linasoma ni namna gani umeme wetu unavyozalishwa ni kiwango gani unapotea. Najua mlinunua mita 666, lakini mita zinazosoma ni mita 336 hii inachangia kutojua umeme unaozalishwa ni kiasi gani unapotea, lakini vile vile hili tatizo linatuletea hasara na inaongeza gharama ya uendeshaji.

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)