Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Onesmo Koimerek Nangole

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Longido

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ONESMO K. NANGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yoyote duniani ambayo inahitaji maendeleo ya watu wake, panahitajika pawepo na viwanda (Viwanda ni uchumi mama). Tanzania baada ya kupata uhuru wake tulikuwa na viwanda 125. Serikali ilisimamia viwanda hivyo kwa kupitia mashirika yake ya Umma, hasa baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki 1977. Viwanda hivyo vimeendelea kudhoofika hadi kufa kabisa. Kutokana na hali hiyo Serikali ilibidi kubinafsisha viwanda hivyo kwa sekta binafsi hapo mwaka 1990.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wa nchi yoyote duniani inategemea uwepo wa viwanda. Bila viwanda maendeleo ya watu kwa sekta mbalimbali ni tatizo na matokeo yake ni watu kuendelea kubaki katika lindi kubwa la umasikini kwa wananchi wake. Hivyo basi, bila kuwepo viwanda, maendeleo yanarudi nyuma na uchumi unabaki kuendelea kuwa hafifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri wa Viwanda na Biashara na Uwekezaji aliyotoa Bungeni hapo tarehe 5 Mei, 2016, nimesoma hotuba hiyo kwa makini sana. Serikali bado haijaonesha nia thabiti ya kukuza viwanda vyetu. Jambo kubwa hapa ninaloona siyo lazima kuanzisha au kuigiliza nchi zilizoendelea kuwa ni lazima kuanzisha viwanda vikubwa. Kutokana na bajeti hii ilivyo ndogo hatuwezi kufikia lengo la uchumi wa kati (itakuwa ndoto tu). Bajeti hii haioneshi matumanini ya dhati katika kukuza na kuendeleza viwanda vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo la kuangalia kwa umakini mkubwa, ni vyema sana tuanze kuimarisha viwanda vidogo hatimaye kufikia hatua ya viwanda vya kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni bora sana kwa Wizara hii kuungana na Wizara nyingine kama Wizara ya Kilimo, mifugo na maji katika kuanzisha tena viwanda vilivyokufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo katika Mkoa wa Arusha wananchi wengi wanajishughulisha na kilimo, ufugaji, utalii na biashara. Napenda kushauri kwamba Wizara hii ingeungana na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, wawekezaji wakapatikana wakaanzisha viwanda vidogo kama vile eneo la Arusha, pakawepo na kiwanda cha maziwa; Longido, Monduli, Ngorongoro pakawepo kiwanda kwa ajili ya nyama na ngozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi nchi jirani wanafaidi sana na mifugo mingi huenda Kenya kwa njia za panya. Faida kubwa wanayopata kutokana na mifugo yetu ni ushuru kwa Serikali za Mitaa, kusafirisha nyama kupeleka nje na kupata fedha za kigeni. Viwanda vya Kenya wanapata sana ngozi ya mifugo kwa kukuza viwanda vyao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa upande wa Mikoa ya Tanga ni vyema pia pawepo na kiwanda kwa ajili ya kutengeneza juisi. Machungwa na maembe yanayolimwa Korogwe na Muheza, mengi yanaoza kwa kukosa soko. Mengi yanapelekwa nchini Kenya kwa ajili viwanda vyao. Tumeshindwa kuanzisha viwanda hivi vidogo kwa ajili ya maeneo hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma sana hotuba hii, kwanza tunataka kujenga viwanda vikubwa na kujifananisha na nchi kubwa kama vile China na kadhalika; hatuwezi kufika huko. Hotuba hii imejaa sana historia na hamasa, hatufikii huko!
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ifike mahali Serikali ijipange kwa upya na kuchagua maeneo machache ambayo nguvu ikiunganishwa kwa Wizara nyingine hasa Wizara ya Kilimo kuanzisha viwanda vitatu kwa kuanzia. Tuanze kwa viwanda ambavyo vitawagusa kwa haraka na mahitaji ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda kama cha mbolea, Kiwanda cha Sukari na Kiwanda cha Mafuta; viwanda hivi vinatosha sana kwa kuanzia kukuza na kuendeleza uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Viwanda ina umuhimu wa pekee sana katika uchumi wa nchi, hasa katika kutoa ajira nyingi kwa wananchi wake, pia katika kuchangia pato la Taifa. Sekta ya Viwanda ni msingi wa maendeleo ya kilimo na ufugaji.