Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Zahor Mohamed Haji

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nianze kwa kuwapongeza wataalam wetu wa Wizara ya Mambo ya Nje wakiongozwa na mama yetu, hakika ndani ya nafsi yangu nafarijika kwamba Wizara imepata mtaalam ambaye kwa kweli amelelewa na kukulia ndani ya chombo hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni muda mfupi nimewahi kufanya kazi naye lakini ndani ya nafsi yangu sina mashaka na uwezo wa Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake lakini Pamoja na hayo Wizara ikiongozwa na Waziri pamoja na wataalam wake ombi langu kwao warudishe heshima ya Taifa letu, warudishe umoja wa nchi yetu mbele ya jumuiya za kimataifa, tulitetereka kidogo hasa kwa sababu ya kutokuendana na wenzetu na mawazo ya wenzetu pamoja na kwamba sisi tunamini, lakini ni wajibu wetu kama walimwengu ambao tunaishi na wenzetu maana yake lazima tuishi na wenzetu ili tuweze kwenda nao pamoja na yale yote ambayo yanatupa changamoto kama walimwengu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mdogo ni suala la covid ambalo kwasasa nashukuru sana tumeanza kulivalia njuga na ninaamini sasa taaluma itatolewa na hatua za tahadhari zitaendelea ili tuendelee kuishi kama walimwengu, Tanzania siyo sehemu ya pekee Tanzania inaishi kama wanavyoishi wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Waziri Wizara ya Mambo ya Nje ni taaluma pekee, ni taaluma unique, siyo kila mmoja anaweza aka-practice mambo ya uhusiano wa kimataifa, ni taaluma iliyotukuka. Siyo kila mmoja anaweza kupangwa kwenda kufanyakazi Wizara ya Mambo ya Nje. Tumejifunza muda mfupi au miaka mchache iliyopita Pamoja na kwamba ni mamlaka ya Wizara yetu ya Utumishi kuweza kumtumia mfanyakazi yeyote kumpeleka popote ombi langu kwa Wizara yetu ya Utumishi lakini vilevile kwa wenzetu wa Wizara ya Foreign Affairs ikae ifanyekazi na wenzetu wakubaliane kwamba siyo kila mmoja anaweza akapangwa kwenda kufanyakazi hasa za kidiplomasia ndani ya Wizara hii. Tunaweza tukapeleka mwandishi wa habari, mhasibu, mpiga picha lakini kazi zinazohusu diplomasia tuwaache wanadiplomasia wafanyekazi za diplomasia ili nchi yetu iweze kufanyakazi zake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa maana hiyo hiyo ningeomba sana sasa tumezungumza wenzetu wengi hapa wamezungumza kuhusu economic diplomacy mana yake tunalazimika sasa kuondoka tulipokuwa tupo huko miaka ya nyuma, sasa hivi tunatakiwa kuangalia ni Nyanja gani na nani ambaye tunaweza kushirikiana naye hasa inapokuja maslahi ya Taifa letu. Marafiki wako wengi, lakini waswahili wanasema nionyeshe Rafiki yako nitakwambia wewe ni mtu wa aina gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, zamani tulikuwa na mirengo ya siasa; kuna wenye siasa kali za kijamaa, kuna mabepari kuna na wasiofungamana, naamini kidogo tumeanza kutoka hapo sasa hivi tunaangalia economic diplomacy.

Ombi langu kwa Wizara tuchague marafiki zetu na tusione haya kuchagua ili mradi Taifa letu litafaidika pamoja na wananchi wake kuhakikisha kwamba tunatengeneza ajira, lakini na biashara zinafanyika ndani na nje ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu imejaaliwa kuwa na bidhaa nyingi sana hasa zinazotokana na kilimo. Ombi langu sana kwa Wizara hii ifanye kazi ya makusudi wala isiogope kufungua balozi kwenye maeneo mengine eti kwa sababu tunaogopea gharama. Gharama ni pesa, lakini pesa zinatafutwa, lakini hakuna kazi kubwa duniani kama kutunza marafiki, ni kazi ya gharama, ni kazi ngumu, lakini lazima sisi kama Tanzania tuhakikishe kwamba tunaishi kama wanavyoishi wenzetu tuweze kuwatunza marafiki zetu. (Makofi)

Ombi langu sana tutafute mataifa ambayo balozi zetu zitafunguliwa, lakini kubwa liwe ni kuhakikisha kwamba Taifa letu linafaidika ili tuweze kufanyabiashara za ndani na nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wakati huo huo naomba nizungumzie hoja moja kuhusu wataalam wetu, ni kweli kwamba tunafundisha, ni kweli kwamba watoto wetu vijana wetu wanasoma kwenye maeneo mbalimbali, ombi langu kwa Serikali wenzetu hawa kama mtakumbuka hotuba aliyoisoma Mheshimiwa Waziri ukiipitia kwa ndani utagundua kwamba mambo mengi waliyoyapanga walishindwa kuyatekeleza kwa sababu tumeshindwa kuwapatia uwezo. Sasa tutaendelea kuwalaumu, tutawashambulia, lakini ukweli ni kwamba sisi kama Bunge tumepitisha bajeti, tumeidhinisha walichokitaka, bahati mbaya sana tulishindwa au Serikali haikuwapatia fedha kama ambazo walizoomba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali ili wenzetu waweze kufanya kazi zao na ili kesho na kesho kutwa tuje tufanye tathmini walichokiomba na walichokifanya, naiomba sana Serikali tuwapatie uwezo wenzetu ili waende wakafanye majukumu waliyojipangia ili Taifa letu lifaidike. Kama unajipangia kazi za Serikali halafu Serikali yenyewe haikuwezeshi maana yake ni kama vile tunatwanga maji kwenye kitu. Ombi langu kwa Serikali tuhakikishe kwamba tunawapatia wenzetu hawa ili waweze kufanyakazi zao kama walivyojipangia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ambalo linaweza likaungana na hili niliwahi kusema kule nyumba kwamba tutawalaumu Wizara zote tutazilaumu tutalaumu Mambo ya Nje, Polisi, Jeshi tutawalaumu Wizara ya Maji, Miundombinu tatizo siyo Mawizara, tatizo ni sisi wenyewe kama Wabunge tumeshindwa kuchukua nafasi yetu ya kuisimamia Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni wajibu wetu basi kuisimamia na kuishauri ili waweze kupatiwa fedha wenzetu hawa wahakikishe wanatekeleza majukumu yao, then ndiyo tuje tuwahukumu hapa kwamba kuna kitu hawakutekeleza tuanze kulalamika. Vinginevyo kila mwaka tutapitisha bajeti haiendi, kila mwaka tutapitisha bajeti kwa sababu tumeiachia Wizara ya Fedha kwa mujibu wa makubaliano yetu kwamba ndiyo iamue nani impe, nani isimpe, impe lini, impe kiasi gani, hili halijakaa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nawaomba sana naiomba sana Serikali naliomba sana Bunge hili tuone namna gani tunaweza kusimamia au kufanyakazi yetu kama Wabunge kusimamia Serikali lakini kuhakikisha yale tunayoamua humu ndani basi yanatekelezwa kwa mujibu ambavyo tumeamua, vinginevyo sisi hatufanyi wajibu wetu na Serikali hatuisaidii ili iweze kuwahudumia wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)