Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Soud Mohammed Jumah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Donge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, na mimi nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhana Wataalah kwa kutujaalia na kutupa afya njema na kuendelea na Bunge sasa hivi karibu mwezi wa pili.

Lakini pia nikushukuru wewe kwa kuweza kunipa hii nafasi kuweza kutoa mchango wangu muhimu katika Wizara hii muhimu ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Hali kadhalika niwashukuru Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri Sheikh Mbarouk pamoja na watendaji wa Wizara hii kwa kweli wamekuwa wakifanya kazi nzuri na tumeanza kuona mabadiliko chanya katika maeneo mengi. Kwa mfano, kule Zanzibar hivi sasa hivi tayari tuna mchoro wa bandari na nafikiria kwamba Wizara yetu hii itafanya hima kuweza kuhakikisha kwamba utekelezaji wa ujengaji wa bandari unafanyika haraka ili yale matokeo chanya yanayokusudiwa kutokana na bandari zile basi yaweze kupatikana.

Mheshimiwa Spika, ningependa kuchangia mchango wangu katika maeneo mawili makubwa; la kwanza ambalo Mheshimiwa Fakharia amelianza ni kuhusu ofisi yetu ya Zanzibar. Kwa kweli Ofisi ya Zanzibar kama alivyosema Mheshimiwa Fakharia, sio ofisi kwa kweli na ni nyumba ambayo ni ya muda mrefu sijui kama tulijenga au tulihamia tu lakini haina hadhi ya kuwa ni Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Ofisi ile imechoka na hivi sasa tuna taarifa kwamba inafanyiwa marekebisho. Sio kujengwa mpya, inafanyiwa marekebisho.

Kwa hiyo, ningewaomba tu wenzetu wa Wizara kwa kweli aidha, sahihi kama tunafanya marekebisho au matengenezo haya ya dharura basi tuendelee na matengenezo ili tuweze angalau kupata pa kuanzia, lakini tuwe na utaratibu wa muda mrefu wa kuangalia uwezekano wa kujenga ofisi mpya aidha pale kwa sababu pale sasa hivi pameshakuwa kama ni museum, ni eneo la mji lile sasa hivi. Kwa hiyo, sio mbaya tukatafuta eneo nje ya mji, kiwanja kizuri tukaenda tukajenga ofisi kubwa ambayo itakuwa na hadhi ya Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje.

Mheshimiwa Spika, kama tunavyojua kwamba ile ofisi ndiyo sehemu kubwa ambayo mabalozi wakienda Zanzibar ile ndiyo sehemu yao kubwa ya kufikia. Lakini pia hata viongozi mbalimbali wenye hadhi ya Kimataifa ile ndiyo ndiyo center yao ya kuweza kufikia, lakini sasa hivi viongozi hawa wengi wanafikia hotelini. Kwa hiyo, ningeomba Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri Sheikh Mbarouk tukajitahidi katika kipindi chenu hiki Inshallah tukaweza kushuhudia kwamba angalau katika kipindi hiki cha miaka mitano tunapata eneo na miaka mitano inayokuja tunajiandaa kwa kujenga ofisi yenye hadhi ya kimataifa ambayo itakuwa ina-represent Umoja wa Mataifa kule kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni suala zima la uratibu na taratibu za ofisi zetu za kikanda na za kimataifa. Kama tunavyojua kwamba kwamba Zanzibar ni kisiwa na inategemea sana ndugu zao wa upande wa pili wa Muungano kuweza kuwawakilisha katika mambo ya kikanda na ya kimataifa. Lakini kidogo kuna changamoto mbili kubwa ambazo zinakabili katika maeneo haya; changamoto ya kwanza ni uwezo wa taasisi za Zanzibar kuweza ku-access fursa za mbalimbali zinazopatikana katika maeneo ya kikanda na maeneo ya kimataifa.

SPIKA: Hebu rudia hapo hujaeleweka.

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, uwezo au capacity ya Taasisi…

SPIKA: Tangu ulipoanzia kwamba Zanzibar…

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, naam!

SPIKA: Rudia kidogo hapo ulipoanzia hoja yako.

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, nasema kwamba changamoto mbili ambazo zinakabili ya kwanza ni uwezo wa taasisi za Zanzibar kuweza ku-access fursa zinazopatikana katika maeneo ya kikanda na maeneo ya kimataifa. Nitatoa mfano, ya kwanza kama tunavyojua kwamba kuna mifuko ya fedha mbalimbali, lakini hali kadhalika kuna balozi zetu hizi kama mfano ukienda Ubalozi wa Japan kuna Shirika la Maendeleo la JICA, ukienda Shirika kama USAID, kuna mashirika mbalimbali ya kikanda, kuna ADB lakini ningependa kuwashauri wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wakatusaidia kutujengea uwezo zile taasisi za Zanzibar kuweza kutafuta hizi fursa kwa sababu sasa hivi kuna malalamiko mengi, lakini ukiangalia wakati mwingine changamoto vilevile sio kama iko katika upande wa Wizara peke yenu, lakini pia wale wenzetu wa Zanzibar bado uwezo wao sio mzuri sana kuweza ku-access hizi fursa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la pili ni urasimu au wenzetu wa upande wa pili kwa sababu kama tunavyojua kwamba Zanzibar hata kama ni jambo sio la Muungano kwa mfano jana mwenzangu Mheshimiwa Ravia alizungumzia hapa suala la michezo. Suala la michezo sio suala la Muungano lakini tukitoka nje ya nchi ni lazima tuweze kuungana. (Makofi)

Sasa tukienda kwenye masuala ya CAF, FIFA lazima tuwe tuko pamoja. Sasa wenzetu wa upande wa pili wa Muungano kama ni Wizara hizi zote lazima washike mkono wenzetu wa Zanzibar vizuri, kwa sababu mimi mwenyewe nimeshawaji kupata changamoto kipindi fulani. Kulikuwa kuna mradi ambao nilikuwa nauratibu Zanzibar kule na nikaomba mradi mimi mwenyewe ambapo ilitangazwa call for proposal, nikaomba na ile call ilikuwa call ambayo ni competitive ya kupambana mwenyewe. Tukaomba ile pesa na tukawa tumeshapata, lakini wakati tunatafuta zile fedha ilikuwa lazima kwa sababu pesa tumezipata through ADB lazima Waziri wa Fedha wa Muungano ndiyo asaini ule mkataba. Ilichukua miezi sita nahangaika kutafuta signature ya Waziri wa Fedha, mpaka tulipomtumia Waziri wa Fedha wa Zanzibar pia naye alishindwa kuweza ku-fast track kuweza kupata signature ya Waziri wa Fedha haraka. (Makofi)

Sasa wakati mwingine changamoto zinakuja kwa sekta za Bara, Wizara za Bara hizi zinakuwa zinashindwa kuzishika mkono zile taasisi za upande wa Zanzibar. Kwa hiyo, ningependa tujitahidi fursa kuweza kusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ningependa kumaliza kwa upande wa mikutano ya kikanda hasa ya Afrika Mashariki. Kuna mikutano ambayo tunashiriki sisi kwa upande wa Tanzania, lakini kuna wenzetu wa Tanzania Visiwani inabidi tuwaalike tuwe nao pamoja lakini taarifa hizi zinakwenda Zanzibar late, inawezekana mkutano uko kesho taarifa zinakwenda leo.

Pia inawezekana mkutano ule unafanyika either Arusha, Kigali, Entebbe na kadhalika katika Afrika Mashariki au SADC. Lakini taarifa zinakuja late, Wazanzibari wanashindwa kujiandaa mapema na ukienda kwenye mikutano wanakuwa ni wasikilizaji tu hawana mchango wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna tatizo la kwamba kwa sababu hakuna maandalizi inawezekana taarifa zile zikienda hata bajeti kule hakuna ya kuweza kumpeleka mwakilishi. Pia kuna mikutano ya maandalizi ambayo aidha inafanyika Dodoma au Dar es Salaam, mikutano ile mara nyingi Wazanzibari hawahudhurii kwa sababu hawapati taarifa mapema na hata wakija kwa sababu inaonekana ni gharama matokeo yake inakuwa ni Tanzania Mainland peke yao ndiyo wanahudhuria kwenye vile vikao na inakuwa havina tija kwa upande wa Zanzibar. (Makofi)

Kwa hiyo, ningeomba tu Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na Wizara kwa ujumla wakajitahidi kuondoa urasimu vile vile kusaidia kujenga uwezo Zanzibar na kuwashika mkono ili waweze kuweza kupata hizi fursa au kuzi-access fursa za kikanda na za kimataifa. Ahsante nashukuru. (Makofi)