Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Alexander Pastory Mnyeti

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Misungwi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. ALEXANDER P. MNYETI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Nianze kwa kupongeza Wizara kwa kazi nzuri wanayofanya chini ya Waziri Bashungwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mchango mfupi sana kwenye Wizara hii ya Michezo, jambo la kwanza ni makato yanayofanywa na Serikali baada ya mechi. Tunafahamu wote kwamba kuandaa timu au kuandaa mchezo ama mchezo ni gharama kubwa, lakini inasikitisha sana baada ya mechi, Serikali mmekuwa mkivamia hayo mapato na kuanza kuyakatakata vipande vipande. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unapoandaa mechi tatizo la Serikali wanakwenda kuangalia nini kimepatikana siku ya mechi. Hawaangalii umetumia shilingi ngapi kuandaa hiyo mechi. Tafsiri yake ni kwamba wanakuja wanakatakata mpaka wanakula mtaji halafu kesho timu zinashindwa kuandaa mechi. Serikali haijui mchezaji ili ahudhurie mechi moja anahitaji kula, kuvaa, kutibiwa, kunywa maji, kwenda mazoezi na kufundishwa na mwalimu aliyebobea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yote hayo Serikali hawayajui na hawataki kuyasikia. Siku ya mechi utawaona wako getini TRA wanakata asilimia 18, Halmashauri wanakata asilimia 10, BMT wanakata asilimia tatu, pasipo kujua umewekeza shilingi ngapi mpaka kufika siku ya mechi. Sasa kwa mfano, unatumia shilingi milioni nane kuandaa mechi moja, halafu getini unapata shilingi 2,100,000. Lakini fedha zote hizo Serikali inaziangalia na inakwenda kuzikata pasipo kujua umetumia shilingi ngapi kwenye kuandaa hiyo mechi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naona huu ni uonevu na kwa stahili hii hatuwezi kuendeleza mpira wa miguu kwa namna yoyote ile, vinginevyo kama tunapiga story ili muda uende hakuna, haitawezekana. Hii kuandaa timu imekuwa ni kama watu wanapiga story sio jambo rahisi kama tunavyofikiria. Wachezaji hawa wanakula, wanatibiwa, wanaumwa, ankle, magoti, sijui visigino vimefanya nini. Ukimtibu mpaka kumpeleka kwenye mechi ni gharama kubwa, lakini inasikitisha sana wakati unafanya hayo yote Serikali haipo. Unawatibu wachezaji Serikali haipo, unalipa kocha Serikali haipo, Serikali inakuja kuonekana siku ya mechi inataka asilimia 18. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri akaliangalie hili vizuri akae na wenzake muone mnawezaje kusaidia hivi vilabu ambavyo vinasuasua havina hata shilingi ya kuendesha huu mpira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, tunampongeza sana Azam kwa udhamini mkubwa wa mwakani ambao ameufanya, lakini si tu mwakani, Azam hata mwaka huu, mwaka jana, mwaka juzi walau chochote ameweka kwenye mpira huu wa miguu na tayari ameanza kwenye michezo mingine kama ngumi, netball na michezo mingine. Tunampongeza sana huyu mwekezaji, mwekezaji mzawa tunaomba aendelee kufanya hivi kwa sababu ndio njia pekee ya kuinua soka la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimuombe Mheshimiwa Waziri kuna mdhamini mwingine anaitwa Vodacom ambayo ligi inayokwisha sasa ambayo bado mechi tatu, nne kuisha. mdhamini huyu ndio mdhamini mkuu kwenye ligi ya Vodacom. Nasikitika kukujulisha mpaka sasa hajawahi kuweka hata shilingi 10 pamoja na udhamini huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kila vilabu vinapouliza jambo hili limekuwa likipigwa chenga. Mheshimiwa Waziri ingilia kati, saidia hivi vilabu vipate haki yao hata kama anaacha, lakini haki ya vilabu vimepatikana ili waendelee na mpira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, najua hili linaweza likachelewa sana kueleweka lakini ndio ukweli, tukizungumza siasa ya mpira katika nchi hii tunazungumza siasa ya Simba na Yanga, lakini Simba na Yanga hawana msaada wowote kwenye kuunda timu ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tusisubiri matokeo ya timu ya Taifa ifanye vizuri halafu akili zetu na nguvu zetu zote tumeelekeza kwenye Simba na Yanga. Simba na Yanga hapa wote tunajua ina nguvu kubwa, ina political mileage kila mtu anashabikia na wengine tuko humu tunashabikia ni sawa kabisa. Lakini tusiulize kwa nini timu yetu ya Taifa haifanyi vizuri, ni kwa sababu akili zetu na nguvu zetu zote tumeelekeza kwenye Simba na Yanga, tumesahau vilabu vidogo ambavyo ndivyo vyenye mchango kwenye timu yetu ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikutolee mfano mmoja, ukiongelea habari ya Simba, juzi Simba wamecheza robo fainali ya Kombe la Afrika tunawapongeza sana. Lakini nikutolee mfano mmoja kule, lineup ya Simba wachezaji watatu tu ndio Watanzania golikipa, namba mbili na namba tatu basi. Namba nne Mkenya, namba tano Ghana, namba sita Mganda, namba saba Mozambique, namba nane Zambia, namba tisa Congo, namba 10 Zambia, 11 Rwanda. Huwezi kupata timu ya Taifa kama wachezaji wa Simba na Yanga wote lineup wanatoka nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kule Yanga, mara sijui Tusiletusinde, mara Tunombetunombe, mara Mandama, sijui vitu gani. (Kicheko)

Nataka nikuambie tunajenga Simba na Yanga kwa nguvu kubwa lakini hatujengi timu ya Taifa kwa sababu tunapoita wachezaji wa timu ya Taifa hatuwaiti wale kwa sababu wanatoka nje ya Taifa letu. (Makofi)

Sasa nikuombe Mheshimiwa Waziri kama kweli tunataka tujenge msingi wa mpira katika nchi hii, haya mambo ya Simba na Yanga tungeweka baadaye ikawa ni second option. Kipaumbele ikawa ni wachezaji wetu wa kitanzania wazawa, ambao tunaweza tukawatumia kwenye timu yetu ya Taifa na wakaleta tija kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii kwenye Taifa letu kila mtu ni Simba ama ni Yanga; anayejua mpira yuko Simba ama Yanga. Simba Yanga, Simba Yanga, Simba Yanga nonsense, hatuwezi kila saa hapa tunaongelea mambo ya Simba Yanga, Simba Yanga, which is Simba and Yanga. Kama tunazungumza habari ya maendeleo ya mpira ya miguu kwenye Taifa letu, Simba na Yanga ziwe second option.

Mheshimiwa Naibu Spika, cha kwanza, tuunde wachezaji wetu wa kizawa wanaoweza kuleta tija kwenye Taifa letu, tofauti na hapo tukiendelea kupiga hizi story tutapoteza muda na hakuna tutakachopata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha, ahsante sana. (Makofi)