Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi siku ya leo kuchangia kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, kwanza nipende kutumia fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kazi ambazo wanazozifanya. Michezo duniani ndio inayotumika kutangaza nchi na utalii, leo ukizungumza Brazil, ukisema Brazil unajua kuna ile timu ya Taifa ya Brazil, lakini Brazil imetangazwa kupitia michezo. Ukizungumza Ujerumani hata mtoto mdogo wanawajua wachezaji wa zile timu, ukizungumza Afrika unaweza ukajua Misri, ukaijua Nigeria, ukaijua Ghana kwa performance nzuri. Michezo inatangaza nchi, hata kuongeza utalii na kipato cha nchi ni michezo, kwenye michezo hatujawekeza vya kutosha, hatujawekeza kwa manufaa ya Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukitaka tufanikiwe kwenye michezo na tukitaka tufanikiwe kwenye kupata kipato kupitia michezo, uwekezaji kwenye michezo unatakiwa uwekezwe kwa namna moja ama nyingine. Moja, tuondoe au tupunguze kodi kwenye vifaa vya michezo, tukipunguza kodi kwenye vifaa vya michezo itasaidia wananchi wengi kuweza hata kununua mpira. Mpira mmoja ambao ni bora shilingi 60,000, vijana wa vijijini kwetu wanatumia masandarusi, wanawezaje kukuza na kukilinda kipaji chake kama vifaa havipatikani? (Makofi)

Mheshimwia Spika, na kuvipata ni kwenye watu wenye uwezo, lazima tupunguze kodi kwenye vifaa vya michezo. Tunayo ile sport center pale Dar es Salaam ya Jakaya Kikwete ni moja Tanzania nzima, halafu unataka michezo ikue, sport center zile zinatakiwa ziwepo kila mkoa katika nchi hii na ikiwezekana kila Wilaya. Utakuza sekta ya michezo, utaibua vipaji vinginevyo, tutakuwa tunazunguka na kudanganyana, ni lazima tuondoe kodi tuwarahisishie, kwa sababu sekta ya michezo haiwekezwi na Serikali itawekezwa na watu binafsi ambao wataweka hizi sport center, wataweka academy, wataweza kununua vifaa vya michezo, jersey, mipira na vitendea kazi pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, turahisishe kuondoa kodi, tuwarahisishie wawekezaji wa sekta binafsi wawekeze kuwa na academy nyingi, tutazalisha hawa vijana wengi. Sio kwenye mpira wa miguu tu hata michezo mingine, ukipunguza kodi itaturahisishia kusonga mbele, otherwise tutakuwa tunapiga mark time.

Mheshimiwa Spika, binafsi niwapongeze wasanii wanafanya vizuri, nimpongeze Diamond, nimpongeze Ali Kiba, nimpongeze Harmonize, nimpongeze Lava lava na wengineo. Hawa vijana tunatakiwa hata tuwape nishani katika Taifa, hawa vijana kupitia muziki wamekuwa maarufu Afrika, kupitia muziki wameitangaza Tanzania. Leo Kiswahili kinaweza kuimbwa Afrika, hawa wanafanya kazi nzuri na kubwa, lazima tuangalie vijana hawa wanavyofanya vizuri kwenye sekta hii ya sanaa ya kuimba, sasa huku wamefanya vizuri, je, wamewezeshwa? (Makofi)

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Seif, pokea.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nilikuwa napenda kumpa taarifa mchangiaji hususani anavyowapongeza wasanii ni jambo zuri sana, lakini pia tuwakumbuke waasisi kina Inspekta Haroun, kina Juma Nature, kina Lady Jaydee, kina Profesa Jay, kina Sugu wao walianza halafu wadogo zao wakafuatia. Kwa hiyo, hawa wanaofanya vizuri tukumbuke kwamba kuna wengine ambao walianzisha kufanya vizuri pia. (Makofi)

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, haya, nakushukuru sana Mheshimiwa. (Makofi)

SPIKA: Unapokea taarifa Mheshimiwa Seif.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, hiyo yote kila mmoja ana mchango wake kwenye sekta hii, ndio maana tunasema wasanii mpaka wamefika hapo, wamefanya vizuri sana hasa kwa sababu ya vipaji vyao. Wanatutangaza, leo ukienda nchi zingine Tanzania utasikia Diamond, Ali Kiba, Harmonize, wanatutangaza hawa vijana na kutangazwa ni unaitangaza nchi. Hata watalii kuja tunapata kipato lazima tuangalie tunawekezaje kwenye sekta ya michezo kuhakikisha kwamba tunatangaza Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nikikuambia katika Afrika ziko derby tano bora, maarufu Afrika; ya kwanza ni Cairo derby - Zamalek na Al-Ahly; ya pili Casablanca derby - Raja Casablanca na Wydad Casablanca; ya tatu ni Tunis derby, Club African na Es Tunis; ya nne, ni Soweto derby kati ya Kaizer Chiefs na Orlando Pirates; ya tano ni Kariakoo derby, Afrika derby tano. Kariakoo derby ipo Simba na Yanga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu wanatoka Kenya, watu wanatoka Uganda, watu wanatoka Congo, Zambia, watu wanatoka hata Ulaya kuja kuangalia derby ya Simba na Yanga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tusizichezee hizi timu, tuziimarishe, tuziboreshe, zinatangaza nchi zetu. Kitendo kilichotokea juzi hatukifurahii sana kwa sababu mechi ilikuwa inatambulika inachezwa saa 11. Timu moja ikaingia mitini, sasa hii na yenyewe ni tatizo, mtu anatoka Kenya anajua mechi saa 11 unabadilisha inakuwa saa mbili usiku. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, hili suala nikuombe…

SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Seif Gulamali, Taarifa.

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, napenda kumpa taarifa mzungumzaji kwamba, Simba haikuingia mtini ila walifuata maagizo yaliyokuwa yametolewa, ahsante. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Seif pokea taarifa inasema kwamba Yanga walitia mpira kwapani. (Makofi)

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, unaweza ukaona jinsi gani ambavyo…, tusipoteze ladha ya michezo hii kama tunaweza kuwatoa watu nchi za watu kuja hapa, wewe unaahirisha kienyeji enyeji sio kitu rahisi, mechi ile ni mechi kubwa. Leo unaona uwekezaji wa Azam kwenye tasnia hii ya michezo hasa kuonesha ligi kuu, kwanza binafsi nampongeza sana Azam kwa kitendo chake cha kuwekeza mzigo mkubwa shilingi bilioni 225. Hili ni jambo la kupongezwa na tunahitaji kumlinda kuhakikisha kwamba anafanya kazi hii kwa uzalendo mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kutangaza ligi yetu inaonekana Rwanda, Zambia, Burundi ndio maana unapata watu wanakuja, isingeoneshwa watu wasingekuja. Kwa hiyo, unaweza kuona impact, sasa Serikali na wadau lazima tuone.

Mheshimiwa Spika, kingine kimegusiwa hapa namna gani ambavyo mpira unavyoendeshwa, lazima tuwe na shirikisho ambalo halina unazi. Mimi naweza nikawa na timu yangu, lakini inapofika suala la kusimamia michezo, usiweke unazi wako kwenye michezo, usipendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona baadhi ya viongozi wa shirikisho wamekuwa na upendeleo kwenye kusimamia ligi, tumeona kesi zikisimamiwa, wengine wakishtakiwa, kesho wanakaa kikao, hukumu inatoka, wengine wakipeleka kesi mzee mpaka leo, kuna kesi ya Morrison ilipelekwa na Yanga pale mpaka leo miezi saba hamna hukumu, hamna kikao, viongozi wanajifanya kama hawaoni vile.

Mheshimiwa Spika, hili ni jambo la aibu hatuwezi kuona jambo hili linaendelea kuendeshwa kienyeji enyeji kama vile shirikisho la timu moja, haiwezekani. Lazima shirikisho lisimamie haki za timu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jana tumeona wanaenda kupewa zawadi viongozi na vilabu vilivyopanda ligi kuu. Wakati kocha mmoja anakwenda pale amekuwa kocha bora wa ligi daraja la kwanza, anatoa mkono kwa kiongozi mkubwa wa shirikisho, kiongozi yuko busy na mambo yake, hataki kutoa mkono. Amebeba zawadi anaenda kumpa tena mkono kiongozi yuko busy, mara ya kwanza it is okay, mara ya pili tena! Tena kiongozi mkubwa wa shirikisho, ni aibu tusiweke unazi kwenye mashindano yetu, hii haiko sawa ni ubaguzi. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, nipende kusema…

SPIKA: Mheshimiwa Seif kuna taarifa unapewa.

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, ahsante napenda kumpa taarifa mzungumzaji kwamba kitendo hicho anachokisema ni kocha aliyekuwa ameshinda kuwa kocha bora katika ligi la kwanza na timu yake ya Geita Gold Mine imepanda inaingia ligi kuu Tanzania Bara. Wakati anapewa ushindi wake, kombe lake Rais wa TFF mara mbili amekataa kumpa mkono na tafsiri yake ulimwenguni kote michezo huwa hairuhusu kabisa masuala ya ubaguzi. Kwa hiyo, tungependa kufahamu je. kwa sisi Tanzania tunachukuliaje masuala ya kibaguzi kwenye mchezo ambao unatuunganisha Watanzania? Ahsante. (Makofi)

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimwia Spika, haya.

SPIKA: Mheshimiwa Seif unaipokea taarifa hiyo.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa hiyo.

Mheshiiwa Spika, tupunguze upendeleo, tupunguze unazi, hata marefa sasa wamekuwa inabidi ukipendelea timu fulani una halali, ukichezesha mechi fulani unakuwa na wakati mgumu, hatuwezi kwenda. Ili kuleta ubora wa ligi yetu haki inatakiwa itendeke na isimamiwe.

Mheshimiwa Spika, kingine, kwenye hii hotuba ya Mheshimiwa Waziri, sijaona kuna mashindano ambayo CAF wameya-launch hivi karibuni ya Interschool Championship. Ni mashindano ya Kiafrika ambayo shule za sekondari zitashiriki mashindano hayo kwa Afrika, sisi nafasi yetu kama Tanzania tumeji-position vipi kuweza kuchukua hii fursa na kuweza kupeleka vijana wetu kwenda kushiriki kwenye mashindano hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri na timu yako lichukueni hili sijaona kwenye hotuba yenu, lakini chukueni hili mkalifanyie tafiti ili muweze kuona mnapeleka hizi timu ambazo zinashinda kwenye timu za UMISETA. Mpeleke hizo timu kama ikiwa Dar es Salaam, kama ikiwa Tabora mpeleke, naamini Tabora mwaka huu tutachukua hili kombe la UMISETA kwa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine ambacho napenda kuchangia, niwaombe tu Wabunge wenzangu kwamba kipindi cha kukaribia kampeni huwa tunachezesha sana ligi za mpira kwenye majimbo yetu. Niwaombe hii tusiiache, tuiendeleze, itatusaidia kuinua kiwango cha michezo kwa vijana wetu hasa tunakotoka. Tuwe na mashindano kama tutashindwa kwa mwaka mmoja basi, baada ya mwaka mmoja tunafanya. Ligi za vijiji, ligi za kata, ligi za wilaya zitasaidia kuboresha. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Seif Gulamali.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha mchango wangu na nakushukuru sana kwa muda wako. (Makofi)