Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Tarimba Gulam Abbas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niwe mchangiaji wa kwanza kabisa katika hotuba aliyoitoa ndugu yangu Mheshimiwa Bashungwa.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nataka niseme kwamba naunga mkono asilimia mia moja hotuba hii na ninataka nimpongeze kwa kazi nzuri, hotuba nzuri yeye mwenyewe binafsi pamoja na wasaidizi wake wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nataka nichangie katika maeneo mawili makubwa; eneo la kwanza, ni uendeshaji wa mpira wa miguu katika nchi hii na eneo la pili, nataka nizungumzie kuhusu timu yetu ya Taifa ya mpira wa miguu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mazungumzo haya naanzisha kutoka kwenye page namba 46 ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri pale ambapo amevitaka vyama vya michezo nchini kuendeshwa kwa mujibu wa taratibu za utawala bora, kufuata kanuni zao na vilevile kuhakikisha kwamba michezo inaleta tija na kuleta maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na kutokana na hili nilitaka nizungumze kwanza upande wa mpira wa miguu. Mpira wa miguu ndiyo mchezo unaopendwa sana katika Tanzania, ipo michezo mingine, lakini mpira wa miguu ndio unaoshika namba moja na kutokana na hali hiyo mpira wa miguu umekuwa ni ajira, umekuwa ni biashara, lakini vilevile imekuwa ni maeneo ambapo watu wanapata burudani na kuwaliwaza wale ambao wanapata matatizo ya aina fulani na kwa fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwa bahati mbaya sana uendeshaji wa michezo hii umekuwa mara nyingi sana kumekuwa na changamoto za ajabu, mara nyingi uendeshaji hauridhishi, wadau wanalalamika na utakuta mambo mengine ambayo yanatufanya tulalamike wala hayana sababu ya kulalamika. Kwa mfano unakwendaje kubadilisha ya mchezo mzito kabisa, mchezo ambao watu wamewekeza kwa hali na mali kwenye furaha zao, wengine wametoka mbali sana wametoka Dodoma kuja kule Dar es Salaam, unakwenda kutubalidilishia mchezo mwisho mwisho wa siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naambiwa kuna watu walichungulia katika darubini zao wakaona wanakwenda kupigwa mabao basi wakaenda kufanya mipango ya kuweza kuupeleka mbele mpira ule, sasa tarehe mpya inakuja tuone watasogeza tena? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, viongozi wa klabu wamekuwa wakipewa adhabu za.., nitatumia neno ambalo siyo zuri, za hovyo hovyo kabisa, hakuna standard, leo huyu akifanya makosa yaleyale anapona mwingine akifanya makosa yaleyale anaadhibiwa kesho yake na adhabu za kutisha kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda mbali zaidi unakuta hata waamuzi wameathirika nao, wamejiingiza katika mambo kama hayo, wanafanya mambo ya upendeleo wa dhahiri uwanjani, wanakosesha klabu nyingine ushindi kwa sababu tu ya mapenzi yao wakijua kwamba watafungiwa mechi moja au mbili halafu wanarudi tena uwanjani. Mambo kama haya yanaleta taabu na kwa hali hiyo utakuta malalamiko yanapelekwa TFF leo, kesho yanapatiwa majibu, mengine yanakaa miezi miwili mpaka miezi saba, standard ipo wapi na hapa napata mashaka kwamba ndani ya chama chetu kile au federation hakuna uadilifu hata siku moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na yanapeleka mpaka mwisho yanafikia very personal, mnakutana katika sherehe, kwa mfano kama juzi kulikuwa na sherehe ya first division, watu wanapeana mikono, sijui ni jana, sijui watu wanapeana mikono wengine wanakataa kutoa mikono, wanatuonesha nini? Kwa sababu tu ya mapenzi yao. Mpira wa miguu umekuwa tented vibaya sana Mheshimiwa Waziri. Tusafishieni mpira wa miguu katika nchi hii ili uweze kutuletea matumaini yanayotarajiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na haya mambo yanayofanyika sasa hivi yanaathiri vilevile timu yetu ya Taifa, timu ya Taifa ya Tanzania haina matumaini, haina matumaini kabisa utafikiri timu ya Uingereza bwana! Uingereza ndiyo nchi za kwanza duniani ambazo zimewahi kucheza international competition. Mwaka 1872 wakicheza na Scottland wakatoka zero-zero, hebu fikiri timu kama hiyo imeshiriki na kupata ubingwa wa World Cup mara moja katika miaka yake yote, walipata mwaka 1966, lakini wana timu nzuri sana, timu zao za binafsi zile moja moja kina Chelsea, kina Manchester United na City wanacheza mpira mzuri sana kwa sababu gani, wao wameamua ku-commercialize ligi yao.

Mheshimiwa Spika, ligi yao ni nzuri sana katika dunia, wachezaji wote wazuri wanakimbilia kule. Lakini timu yao ya Taifa haioneshi ule ukali wa ligi yao, so it is the opposite, inavyotakiwa ligi ya nchini kwako hasa premier league ndio iakisi timu yako ya Taifa. Sisi timu zetu ziko kali, zina ligi, ligi yake inaanza kuendelea kuwa vizuri zaidi, lakini where is local talent, iko wapi local talent? Tunaletewa wachezaji wengi wa nje, timu zetu zinafanikiwa, lakini zinafanikiwa kwa sababu ya wachezaji sana wa timu za nje ambao pia nao ni wa mashaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini wa mashaka, wewe ukiangalia naomba niitaje baadhi ya timu, ukiangalia pale kwetu Young African kwa mfano, tunao wachezaji wa nje wengi tu, lakini hawaisaidii Young Africans mpaka iingie kina Kaseke na kina nani ndio watuletee magoli. Simba Sports Club wachezaji lukuki wamo mle ndani sijui, wachezaji saba mpaka nane kwa timu moja wanaocheza uwanjani, akiingia Boko ndio analeta maneno. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa point yangu ni nini, point yangu ni kwamba ili tuweze kupiga hatua ningependa intervention ya Serikali kwa maagizo kwa TFF kwamba bwana sasa ni wakati wa kuangalia suala zima la wachezaji wa nje na jinsi gani ligi zetu zinaweza zikaibua local talents na timu yetu ya Taifa iweze ikasimama. Bila wachezaji wa ndani kupata nafasi za kutosha, wakacheza katika timu zao, tusahau kupata mafanikio katika timu ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpira wa miguu kama nilivyosema ni mchezo ambao unaotegemewa sana. Sasa kama utakuwa na premier league ambayo haiakisi mafanikio ya timu ya Taifa tutaendelea kubakia kama England. Sisi tumeshiriki mashindano ya ubingwa wa nchi huru za Afrika nafikiri mara mbili, Nigeria na juzi hapa Misri, lakini kote huko hatujapiga hatua, kwa sababu gani; hata uchaguzi wetu wa makocha, kocha akija hapa akikaa miezi sita ameshatimuliwa tayari, continuity unaipata wapi Mheshimiwa Waziri? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu wanatakiwa kustahamili na hiyo imeathiri mpaka kwenye klabu zetu sisi za mjini humo. Young Africans sijui katika msimu huu wameondoa makocha wangapi! Hata makocha wazuri huwezi ukamjua kama huyu mzuri kwa sababu ndani ya miezi mitatu hata hajapoteza mechi nakumbuka ameondolewa. Ukija Simba Sports Club nako ni hivyo hivyo, ukienda kwenye klabu nyingine ndogo ndogo ni hivyo hivyo. Hebu watanzania tuwe na tabia ya kustahamili tunapowapa makocha timu zetu kutulelea na hili nalitaka sana kwenye upande wa timu ya Taifa Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwamba timu ya Taifa muisaidie na katika kuisaidia sio kuwapa fedha tu, wapeni maelekezo yanayofaa na najua Serikali haitakiwi iingilie masuala ya mpira, lakini jina la Tanzania ndilo linalotumika. Tukifanya vibaya nchi yetu kama nchi ndio inayopata ratings mbovu, tusikubali Tanzania ipate ratings mbovu kwasababu ya viongozi ambao hawajitambui. Hawa viongozi wasiojitambua wanaopewa mamlaka ya kuongoza TFF, Mheshimiwa Waziri wawekeeni taratibu ngumu sana ili hata kupima uadilifu kwa timu zetu za Taifa, kupima uadilifu wao kwa Tanzania uwe ni moja ya vigezo vya kupata viongozi wa namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sio tu kura, msiangalie sana suala la kura, kama mtu tunamuona akienda kwenye kupigiwa kura atashinda, muondoeni. Mbona wangapi wamekatwa katwa katika nafasi chungu mzima, kwani kuna lazima wawe ni wao wao tu? (Makofi)

Mheshimiwa Waziri naomba nikuunge mkono katika mipango yako ambayo umeizungumza ya mwisho. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana nakushukuru. (Makofi)