Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara

Hon. Prof. Kitila Alexander Mkumbo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ubungo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya kujibu baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge ambazo wamezitoa katika hoja yangu niliyowasilisha asubuhi.

Kwanza nichukue nafasi hii kukushukuru sana wewe mwenyewe kwa jinsi ambavyo umeweza kuongoza mjadala huu vizuri sana na kuweza kuniongoza pia katika uwasilishaji wangu. Niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri sana katika kuboresha hoja yangu. Lakini kwa nia njema ya kuendeleza Sekta ya Viwanda na Biashara.

Nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu vizuri sana baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge ambazo wamezitoa hapa. Tumepokea michango mingi, michango 20 ya kuchangiwa hapa moja kwa moja na michango miwili kwa njia ya maandishi. Niwaahidi tu kwamba…

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge waliochangia kwa maandishi naambiwa wako kumi, niwaahidi Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa kauli na kwa maandishi tutajibu hoja zote hizi bila kuacha hoja hata moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, naomba tu kusema kwamba hoja zote ambazo zimetolewa ni za msingi. Zile ambazo ni ushauri, tunazipokea na tutazifanyia kazi zaidi katika kuboresha utendaji wa kazi kama Wizara. Yale ambayo yanahitaji uboreshaji wa kisheria na kimiongozo, tutayafanyia kazi. Baada ya kusema hayo, naomba uniruhusu nipitie baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, nianze na hoja inayohusu miradi ya makaa ya mawe wa Mchuchuma na chuma cha Liganga. Kama mnavyofahamu, wote tumepitisha Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano hivi karibuni katika Bunge hili hili. Mradi huu ni moja ya miradi 17 ya miradi ya kielelezo ambayo Serikali imepanga kuitekeleza. Ni mradi ambao unaendelea. Ulikuwepo katika Mpango wa Maendeleo uliopita na Waheshimiwa wengi wamehoji kwa nini mradi huu umechelewa. Kwa kweli umechelewa, Serikali haipingi hilo, lakini muhimu ni kujibu hasa kwanini umechelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tukubaliane katika hatua ya utekelezaji ya miradi mikubwa kama hii kuna hatua nyingi, tunafahamu feasibility study ya mradi huu ilikamilika mwaka 2012, ni kwa feasibility study hii ndiyo tukagundua kwamba tunazo tani milioni 428 za makaa ya mawe katika eneo la Mchuchuma na tunazo tani milioni 126 za chuma katika eneo la Liganga. Hiyo ilikuwa ni hatua ya kwanza ya feasibility study. Lakini baadaye, ikaja ikagundulika kwamba pale sio tu kwamba tuna mawe na chuma, tunayo pia madini ya maana sana duniani, madini ya titanium na vanadium.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maandalizi ya mradi pia kama Waheshimiwa Wabunge walivyoeleza, upo ujenzi wa barabara, kilometa 221 pamoja na ujenzi wa reli. Hii nayo ni hatua muhimu. Lakini hatua ya tatu ni kufanya tathmini ya mazingira; athari za mazingira katika utekelezaji wa mradi huo, hili limefanyika. Kwa hiyo, kusema kwamba hakuna kitu ambacho kimefanyika sio sahihi. Yapo mambo ambayo yamefanyika na kwa kweli, zile shughuli za msingi za Serikali imezifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya nne ambayo ni ya msingi ilikuwa ni kutafuta mwekezaji. Mradi huu investment cost yake ni zaidi ya dola milioni tatu. Kwa hiyo, ni mradi ambao ilikuwa lazima kutafuta mwekezaji ili kushirikiana na Serikali kupitia Shirika la NDC kuweza kutekeleza. Kwa unyeti wa mradi wenyewe na ukubwa wa mradi wenyewe, kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wameeleza, ni mradi muhimu sana kwa maendeleo ya nchi hii. Ni mradi ambao unabeba rasilimali za msingi na muhimu za Taifa. Kwa hiyo, lazima Serikali yoyote duniani na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ingetaka kujiridhisha kuhusu faida ambazo Serikali na nchi hii itazipata sio tu leo. Miaka mingi ijayo, unazungumzia tani milioni 428 za makaa ya mawe na tani milioni 126 za chuma. Unazungumzia uwepo wa madini ya titanium and vanadium, some of the most precious minerals in the world. (Makofi)

Kwa hiyo, ni mradi ambao lazima ujiridhishe; mwekezaji akapatikana, tukafanya majadiliano, lakini hatukufikia mwisho kwa sababu mwekezaji alitaka masharti ambayo hayakubaliki kwa nchi, kwa sababu mengi ya masharti yanapingana na sheria zetu, hasa sheria ambazo Waheshimiwa Wabunge tumezipitisha hivi karibuni za mwaka 2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazingira hayo ingekuwa ni vigumu Serikali kusema aah, twende tuanze kutekeleza mradi. Bahati nzuri mwekezaji anaelekea kukubali masharti mengi ya Serikali na taarifa ambazo ninazo kutoka kwa Government Negotiating Team, bahati mbaya ni kwamba wawekezaji wameshindwa kuja kwa sababu ya mazingira ya sasa ya pandemic, lakini mazungumzo yanarudi na masharti mengi anaelekea kukubaliana na akishakubali masharti ya Serikali ambayo tunajiridhisha kwamba ni muhimu kulinda maslahi ya nchi, mradi utaanza kutekelezwa ili mradi uwe na manufaa, sio tu kwa kizazi cha leo sisi hapa, lakini kwa miaka mingi ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, isije pakatokea hapa wakataka kutafuta hili Bunge la Kumi na Mbili waliokuwepo ni akina nani ambao walikwenda kuiuza nchi? Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge Serikali inatambua umuhimu wa mradi huu kama ambavyo nyie mnatambua na Serikali ipo committed kuutekeleza na ndio maana upo katika documents zetu zote za ajenda za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo ningetaka kuitolea maelezo ni suala la blueprint. Waheshimiwa Wabunge wameongea kwa uchungu kuhusu blueprint. Kwanza niwakumbushe, blueprint tumeipitisha kama nchi tarehe 01 Julai, 2019, maandalizi yakaanza katika mwaka 2019/2020, mwaka 2020/2021 tukafanya mambo ya kawaida yakiwemo kuondoa baadhi ya tozo, ada na adhabu ambazo zilikuwa zinakwaza biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukatengeneza taasisi za utekelezaji wa blueprint. Tukasema tutengeneze action plan, tukatengeneza action plan imekamilika na action plan hii ukiisoma inaanza utekelezaji wake rasmi mwaka 2021/2022 na ndio maana moja ya kitu ambacho tumepata, tumepata Euro milioni 11.5 kutoka Jumuiya ya Ulaya kwa ajili ya kutekeleza mradi huu. Na moja ya hatua kubwa sana ni kwamba, tunakwenda kufungua One Stop Centres kwenye kila Halmashauri, kwa sababu tathmini inaonesha kwamba, tumefanya mengi katika ngazi ya kitaifa, Serikali Kuu, lakini kwenye local government wanaendelea ku-behave business as usual.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio likaandikwa andiko, tumepata fedha Euro milioni 11.5 zaidi ya shilingi bilioni 50, hizi zote zinakwenda kwenye ngazi ya local government. Moja ya kazi ya kufanya ni kutengeneza ki-TIC kingine kule ambacho kitakuwa na One Stop Centre ili mwekezaji akienda apate huduma zote palepale haraka iwezekanavyo, kwa hiyo, ni hatua kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunaendelea na maboresho ya sheria na baadhi ya sheria Waheshimiwa Wabunge mmezipitisha wenyewe hapa ikiwemo Arbitration Act ambayo imepita mwaka jana. Hii inakuwa ni moja ya utekelezaji wa blueprint, lakini mwaka huu tunafanya marejeo ya sheria kadhaa ambazo zitakuja hapa Bungeni kupitia Miscellaneous Amendment na zingine kama ni sheria za kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumefanya mazungumzo na Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu suala zima la work permit ambalo mmelizungumza hapa. Hili nalo tunalifanyia kazi, yale maeneo ambayo yanahitaji mabadiliko ya sheria yanakuja hapa na tumeshaelewana kwamba, kwa kweli ile Sheria ya Work Permit lazima tuipitie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna suala la maagizo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan aliyatoa hapa na ameyarudia tena juzi, nadhani kwenye moja ya hotuba zake kwamba hizi taasisi nyingi ambazo zinafanya kazi katika nchi yetu, hizi katika ku-regulate business lazima zifanyiwe marejeo na alitumia neno ziwe reviewed, maana yake lazima tuzipitie na sisi wenyewe katika Wizara yangu tuna taasisi 15 na moja ya kazi ambayo nimeeleza tunaenda kuifanya katika Wizara yetu ni kupitia hizi taasisi kuona kama kuna muingiliano wa majukumu, ili tuweze kuyaweka vizuri.

Kwa hiyo, tunakwenda kufanya mapitio ya taasisi mbalimbali katika nchi hii ambayo tunadhani yanakwaza biashara, ili tuyaweke vizuri. Hili ni agizo ambalo tunalitekeleza halihitaji sheria yoyote kwa sababu tunalifanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumeboresha mifumo ya electronic. Mifumo mingi ya electronic ambayo tunaiona kwa sasa ndani ya BRELA na TBS ni matunda ya utekelezaji wa blueprint. Mifumo mingi ambayo mnaiona kupitia TRA na Wizara ya Fedha na Mipango ni matunda ya utekelezaji wa blueprint. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge inawezekana hatua hazitoshi, lakini sio sahihi sana kusema kwamba hakuna kitu ambacho kimefanyika. Tunafanya mambo mengi, lakini pia, hatupo nyuma ya wakati kwa sababu ndio kwanza action plan imekamilika na utekelezaji unakwenda kuanza katika mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la mwisho katika hili, mambo mengi ni mindset change, aliongea Mheshimiwa Mbunge Lucy pale. Mengine hayahitaji sheria, hata mimi ninapozungumza na watendaji wangu na wakuu wa taasisi mbalimbali nawaambia pengine tulikosea kutafsiri, hizi bodi zinaitwa regulatory authorities tukatafsiri kwamba ni mamlaka za udhibiti. Sasa udhibiti kiingereza chake ni control, ninawaambia hapana, tunapaswa ku-facilitate sio kudhibiti. Kwa hiyo, mambo mengi ambayo tunayafanya mengine kwa kweli, ni kubadilisha mtazamo tu mtu akae pale akijua kwamba anakwenda kuwezesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, ndani ya Wizara ya Viwanda na Biashara tumesema tutakwenda kusimamia kitu kinaitwa service charters. Taasisi zetu zote zina mikataba ya huduma kwa wateja na mle ndani tumeainisha huduma hii ichukue muda gani, tunakwenda kusimamia kuhakikisha kwamba huduma zinatolewa mapema iwezekanavyo. Muhimu zaidi nasisitiza kwamba ni kubadilisha mtazamo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ni viwanda vilivyobinafsishwa. Waheshimiwa Wabunge viwanda hivi vipo katika maeneo makubwa matatu, vipo viwanda ambavyo vilitelekezwa; kwa nia njema Serikali ilivibinafsosha tukaingia mikataba na wawekezaji wakavichukua, wakavitelekeza. Yamekuwa mapori, wengine wamebadilisha viwanda hivi kuwa sehemu ya kufugia ng’ombe, wameweka mifugo yamekuwa maghala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mikataba na hawa watu na tulisema wataviendeleza viwanda hivi kwa mujibu wa tulivyokubaliana. Tulipofika hapo Serikali isingekaa kimya na wenyewe kule tulipoenda kuzungumzanao wakasema aa aa, kwa kweli tulikosea chukueni viwanda vyenu; tungefanyaje kwa hiyo, hatujapora wamevirudisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kundi la pili wapo wawekezaji ambao tuliona kwamba hawajaishi vile mkataba ulivyotaka. Tukafanyanao mazungumzo, tukakubaliana wakakiri kwamba tulifanya makosa, wamevunja masharti hapa na hapa, wakakubali kujirekebisha. Hawa tunawarudishia viwanda kwa masharti mapya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wapo ambao wamekubali kwamba kweli tulivunja masharti makubwa na kwa kweli, hatuna uwezo wa kuendelea kufanya hii kazi. Wamevirudisha viwanda 22 hivi ndivyo ambavyo tumevitangaza tunavitafutia wawekezaji wapya na moja ya kipaumbele ambacho tangu niteuliwe nimekipa kikubwa sana ni kusimamia zoezi hili ili viwanda hivi vipate wawekezaji vianze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kundi la mwisho ni viwanda ambavyo kwa kweli tumeshindwa kukubaliana kati ya Serikali na mwekezaji. Yeye anaving’ang’ania anadhani kwamba, yupo sahihi na sisi tunaamini kwamba hayupo sahihi. Sasa nchi hii ni nchi ya utawala wa sheria, katika mazingira hayo tutakwenda kwenye vyombo vya sheria ili tupate haki ama Serikali ama mwekezaji. Hii ndio hatua ambayo tunakwenda nayo katika suala la viwanda ambavyo vimebinafsishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nitolee maelezo mafupi kuhusu suala hili la EPZA na SEZ; Waheshimiwa Wabunge wameongea hapa. Nimeeleza katika hotuba yangu kwamba, moja ya hatua ambayo tunakwenda kufanya, tunakwenda kufanya tathmini ya kina kuhusu mafanikio na changamoto za uwekezaji katika maeneo maalum ya kiuchumi. Hii tathmini itatupa wapi tumefanikiwa, wapi kuna changamoto, nini turekebishe, lakini kwa ujumla wake tathmini ya ndani ambayo tumeifanya uwekezaji katika maeneo haya umekuwa na mafanikio makubwa sana. Mpaka dakika hii tunazungumzia uwekezaji wa dola bilioni
2.5 ni uwekezaji mkubwa, lakini tukifanya tathmini itatupa zaidi tuelekee wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimtoe wasiwasi ndugu yangu Mheshimiwa Getere kuhusu uwekezaji pale Bunda anasema wananchi wake wanakwenda kuwa masikini, hapana. Mwaka huu tumeiagiza EPZA inakwenda kujenga shades kwenye eneo ambalo tumelitenga lile ili viwanda vianze kujengwa pale. Kwa hiyo, Mheshimiwa Getere hapana, watu wako hawatakuwa masikini, tunakwenda kuwekeza pale, tutaweka shades na eneo lile utafiti wa awali unaonesha kwamba ni eneo potential sana, litapata wawekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kwenye hoja hizi nizungumzie kidogo kuhusu mkakati wa C2C, mkakati wa nguo na mavazi. Waheshimiwa Wabunge wameongea kwa uchungu. Ni kweli karibu nusu ya nchi hii ni wakulima wa pamba, ni zao muhimu. Haikubaliki kama ulivyosema kwamba tuna-export asilimia 30; asilimia 70 ya pamba ambayo tunazalisha hapa. Kumbukeni Waheshimiwa Wabunge mwaka 1992 tulikuwa na viwanda vya nguo 32, lakini mpaka sasa hivi tunazungumza tuna viwanda 12 vya nguo; viwanda nane vya pamba viwanda vingine vilivyobaki vinne vya polister.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na viwanda hivi katikati viliyumba, laki ni kwa kufuatia mkakati wa C2C vingi vimeanza kufanya kazi na juzi nimetoka Morogoro kutembelea baadhi ya viwanda vinafanya kazi vizuri. Muhimu ni kwamba huu mkakati ambao tumeuhuisha, wengi mnafahamu, tumeuhuisha mkakati wetu kwamba sasa unakwenda kutekelezwa kwa miaka mingine kumi, baada ya kuonesha mafanikio makubwa tuna mkakati mwingine mwaka 2021 mpaka mwaka 2031 ili kuhakikisha kwamba viwanda hivi vinasimama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini muhimu san ani lile wazo ambalo Mheshimiwa Tabasam amelitoa, ni wazo zuri sana lazima tugawanye. Mchakato wa kutengeneza nguo una hatua karibu sita, lazima tuwe na viwanda vikubwa ambavyo vinapokea kutoka kwenye viwanda vidogo. Tuwe na viwanda ambavyo kazi yao ni ku-feed viwanda vikubwa, unaweza ukawa na viwanda vikubwa vitano tu nchi nzima ambavyo kazi yao ni kumalizia mpaka nguo, lakini viwanda vingine vinachakata kuanzia kwenye kuchambua pamba mpaka kutengeneza uzi na uzi ukaenda kwenye viwanda vikubwa. Tupeni nafasi tutekeleze mkakati huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwenyewe kwa kweli mkakati huu ni mzuri sana na ni moja ya kipaumbele katika utekelezaji wangu, ukiona kwenye ile hotuba yangu, ni namba mbili. (Makofi)

Sasa Waheshimiwa Wabunge niwaombe mnipitishie hii bajeti mapema iwezekanavyo, ili mimi kazi hii nianze mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie; kuna Waheshimiwa wamesema hapa hatutembelei viwanda, tunakaa tu ofisini. Waheshimiwa Wabunge mimi nimeapishwa tarehe 9 Aprili, 2021 kama mwezi mmoja umepita, nimeshatembelea tunavyozungumza tayari viwanda vitano. Cha mwisho nimetembelea juzi kiwanda kikubwa sana cha 21st Century pale Morogoro cha nguo, kikubwa kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshakutana na wadau mara tano, nikiwa hapa Bungeni ndani ya mwezi mmoja tangu niteuliwe. Kwa hiyo, kutembea ni sehemu yetu, kutembelea viwanda, lazima tutembelee viwanda, tukutane na wadau, tuone changamoto zao, tuone mafanikio yao, Mheshimiwa Naibu Waziri kila siku yupo barabarani. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge hili tunalo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la bidhaa la ubora; moja ya taasisi yenye mafanikio makubwa katika nchi hii, na ni vizuri Waheshimiwa tujivunie vitu vyetu, ni TBS. wanafanya kazi kubwa sana kudhibiti ubora wa bidhaa zinazozalishwa ndani ya viwanda vyetu, lakini pia vinavyoingia kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sana na mimi nimekutana na wafanyabiashara wengine wanalalamika, ukiwauliza nini, unakuta kwamba ana product yake ambayo ni inferior imekwama test ya kawaida ndani ya TBS, wana maabara tisa za kisasa kabisa. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge tusiwe na shaka tunazo taasisi ambazo zinafanya kazi, wanafanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea ushauri wenu kwa maana ya kuboresha na ushauri wa Mheshimiwa pale amezungumzia suala la labeling kuhusu vyakula, wataliangalia kama kuna upungufu tulirekebishe tuimarishe zaidi, lakini kwa ujumla wake nirudie tena, TBS kwa maana ya Shirika letu la Viwango, linafanya kazi nzuri. Ni moja ya mashirika ambayo yanaheshimika sana hapa Barani Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo nimtoe wasiwasi tu Mheshimiwa ambaye alizungumzia kuhusu Zanzibar na Tanzania Bara. Tumeshakaa, tumekutana na ndio maana tumekubaliana kwa mfano kwa Zanzibar Bureau of Statistics (ZBS) wamekubaliana na TBS wakipima Zanzibar wakakubaliana kwamba, ni kiwango vizuri hapa Tanzania Bara hakuna haja ya kupima tena. Kwa hiyo, limeshawekwa vizuri, tunafanya mazungumzo ya mara kwa mara kati ya sisi na wenzetu Wazanzibari kuhakikisha kwamba hizi kero ndogo ndogo za muungano ziondoke kwa sababu, sisi ni nchi moja, hilo ndio jambo la msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge tena waridhie ili bajeti yetu ipite tuanze utekelezaji wa kazi. Ninawasalimu tena kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

MWENYEKITI: Toa hoja.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki. (Makofi)