Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nichangie hii Wizara ya Viwanda na Biashara. Nakushukuru wewe mwenyewe kwa kumuomba Mwenyezi Mungu amekuleta hapa Bungeni, lakini umekaa maeneo yako yale yale kama ulivyo kawaida, tunakuombea uendelee vizuri. Nashukuru Wizara yangu Wizara ya Viwanda ambayo mimi ni mwanakamati, namshukuru Profesa na crew yake yote Naibu Waziri na Katibu, kazi zinaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea ni kwamba naomba nchi yetu hii Mungu anaipenda sana na nadhani tuendelee kumuomba Mungu atuepushe na haya magonjwa mabaya yanayokuja na mimi naamini kama tutaendelea kumuomba Mungu hali itaendelea kuwa nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti,Na niombe tu kwenye mikutano yetu yote tunayokuwa tunakuwa nayo tuwe tunaanza na yale mambo yetu ambayo ni ya Mungu kwa mfano, Bunge letu huwa tunaanza kuomba Mungu kwanza ndio tunaingia, hata kwenye mikutano tuombe kwa kuomba kwamba Asalaam Aleykum, Tumsifu Yesu Kristo, Bwana Asifiwe, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kazi Iendelee. Kwa hiyo nadhani hili nalo ni jambo kumtanguliza Mungu kila tunapokuwa tunafanya shughuli zote ambazo tunataka kuzifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichangie kwenye Wizara hii kwenye upande wa Mchuchuma na Liganga. Mimi kama mwanakamati nilivyoona ile hali na wakati sisi humu tunajipa matumaini kwamba Mchuchuma na Liganga itakuwepo, mimi kwangu naona kama hatutatafuta mwekezaji mwenye uwezo wa kuendesha ule mradi itakuwa ni majina tu tunaita kila siku mpaka tunafia humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili Liganga na Mchuchuma iwepo lazima tutafute mwekezaji mwenye uwezo wa kuendesha ule mradi, maana Serikali haiwezi kuendesha ule mradi. Kama Serikali haiwezi kuendesha ule mradi, tutafute mwekezaji mwenye uwezo wa kuendesha ule mradi na mwekezaji mwenyewe tukishampata mikataba yake tuisome wazi ionekane kwamba, anashughulika na miradi miwili mradi wa madini na mradi wa chuma aelewe mapema kutoka sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru…

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa taarifa kaka yangu kwa mchango wake mzuri kwanza wa Liganga na Mchuchuma. Ningependa kumpa taarifa kwamba, kwanza huo mradi umechukua muda mrefu takribani miaka 20, lakini Serikali imeingia ubia na mwekezaji Mchina, amekaa zaidi ya miaka nane, ameshindwa kufanya chochote, wako kwenye hatua ya kulipa fidia, mbaya zaidi wanaenda ku-review mkataba na mwekezaji yule yule.

Sasa taarifa yangu nakupa kwa nini wasimfukuze na naungana na wewe watafute mwekezaji anayeweza kwenda kuwekeza kwenye Liganga na Mchuchuma ili tuweze kupata faida katika Taifa letu. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, taarifa yake naikubali nadhani dada yangu sasa hivi yuko vizuri sana, kwa hiyo, naikubali taarifa yake. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua tusiwe tunazungumza mambo humu Bungeni kama kujifurahisha. Nchi yetu inahitaji kupata viwanda ule mradi ni mradi mkubwa sana, mkubwa sana. Kwa mwekezaji aliyopo kama ana-tender nyingi maana yake anataka afanye mradi mmoja yeye kwa mradi mmoja huo hataki ku-separate mambo ya madini na chuma. Kwa hiyo, mimi nione kama ni kazi, kwa hiyo, nimesema tutafute, kama yeye yupo, kama mikataba yake inaeleweka, tuilete hapa Bungeni tuione, tuizungumze humu Bungeni tuione kama anaweza kuifanya ile kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama hawezi kama alivyosema Mheshimiwa Ester tumuondoe, tutafute mwekezaji mwingine mwenye uwezo. Sasa siku hizi nako nimesikia Tanzania kuna matatizo, tunaweka makandarasi, tunawaondoa, sijui ni kienyeji sijui ndio ujanja wao, wanarudi nyuma kinyume nyume kutudai tunalipa mabilioni. (Makofi)

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Taarifa.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa muangalie tena mambo haya yanavyokwenda ili tuwe tunaweka hii mikataba na mambo mapya tusiwe tunaingia tena kudaiwa mabilioni ya watu wanaokuwa wanaweka mikataba…

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita subiri kidogo, Taarifa Mheshimiwa Mhagama.

T A A R I F A

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kukupongeza kwa kurudi katika nafasi yako, naomba nimpe taarifa mzungumzaji mzuri sana Mheshimiwa Getere kwamba commitment ya Serikali ya kuendeleza mradi wa Liganga na Mchuchuma haupo tu kwenye kuingia mkataba na mwekezaji, bali pia kujenga mazingira ya kuanza kutekeleza mradi huo kitu ambacho hakijafanyika mpaka leo kwamba ilipaswa tuwe na reli ya Kusini ambayo itasafirisha chuma, tulipaswa tumalize barabara ya Madaba – Mkiu kwa ajili ya kusafirisha makaa ya mawe na chuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hoja yake ni ya msingi na hata mazingira yetu ambayo tulitakiwa tuwe tumeyafanya hatujafanya. Kwa hiyo, hata wakisaini mkataba wa kuchimba kile chuma hawana baraba raya kusafirisha wala reli ya kubeba chuma. Ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nashukuru leo naona kila point ninayokwenda mtu anaichangia namshukuru sana kwa point hizo ambazo ameenda nazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa Liganga na Mchuchuma, kulipa fidia lazima wananchi wa maeneo yale waambiwe, mwenye fedha ya kuwalipa wale wananchi ni nani ni mwekezaji au ni Serikali? Kama ni Serikali itoe maandalizi ya kulipa fidia kwa wananchi, kama ni mwekezaji tuwaambie wananchi kwamba sisi fidia hatutalipa mpaka mwekezaji atakayekuja hapa ndio atalipa ili wananchi wale wajue kinachoendelea pale. Sio wanakaa wanasubiri fidia, fidia, fidia kumbe inasubiri mwekezaji na mwekezaji anaweza kuja mwaka 2030 tumeshatoka humu Bungeni kwa hiyo, wawaambie wananchi kwamba nani anapaswa kulipa hiyo fidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihame hapo niende kwenye viwanda vya Wilaya ya Bunda. Wilaya ya Bunda inaenda kuwa maskini kama ilivyokuwa huko nyuma kwamba sisi tulikuwa maskini kwenye Wilaya ya Bunda. Viwanda vilivyokuwepo Bunda kulikuwa na Kiwanda cha Kibara Ginnery, kuna S & C Ginnery, kuna Mount Meru Ginnery, kuna Olam Ginnery, kuna Mara Lint Ginnery, kuna Ushasi Ginnery, vyote vinaenda kufa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilikuwa viwanda vya pamba na Wilaya ya Bunda ndio inazalisha pamba nyingi kwa maeneo yote ya Mkoa wa Mara. Ndio eneo bora viwanda vimekufa, Kibara Ginnery imekufa, Ushasi msimu wa mwaka 2019/2020 Serikali tulilazimisha watu wanunue pamba kwa bei ambayo ni kubwa, wakasema yale makampuni yakinunua watapata refund kutoka Serikalini, hawakurudishiwa. Makampuni yamekufa, Olam ilikuwa inafanya kazi imefungwa, S & C inakwenda kufungwa, viwanda vingine Ushasi Ginnery imefungwa miaka mingi, Mara Lint imekufa, Bunda inaenda kuwa maskini ya mwisho katika Mkoa wa Mara na katika maeneo yote ya Tanzania. Kwa hiyo tuombe sasa Waziri…

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa ya mwisho hiyo Mheshimiwa Ester.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe taarifa kaka yangu Boni mbali na mchango wake huo mzuri wa ginnery, lakini pia Mkoa wa Mara tuna kiwanda pale Musoma cha MUTEX, Serikali bado inashindwa ku-invest ili wakulima wetu wa pamba, mbali tu ya Mkoa wa Mara na maeneo mengine wawe wana uhakika wa soko. Lini pia Serikali itaenda kuwekeza fedha kwenye kile Kiwanda cha MUTEX. Nilikuwa nampa kaka yangu taarifa Mheshimiwa Boni.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Getere.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante namshukuru sana Mheshimiwa Ester yuko sasa hivi nadhani amebadilika yuko vizuri sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumza haya mambo, hatuwezi kuwa na Wilaya kubwa ambayo inazalisha pamba kwa wingi halafu viwanda vyote vimekufa. Kwa hiyo, Wizara ya Viwanda na Wizara ya KIlimo nadhani wakutane sasa waende waangalie vile viwanda msimu wa mwaka huu haijulikani pamba itauzwa wapi! Kwa hiyo, waende wakutane waone kiwanda kipi kama ni Mara Lint kama ni Kiwanda cha S & C wawalipe fedha waliyolipa ambayo wanadai Serikali, kama ni Olam wawalipe waliyokuwa wanalipa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna viwanda vya mafuta, mimi hii nchi sijui ina miujiza mimi sielewi. Kama leo tuna alizeti ambayo tukiamrisha mwaka kesho au msimu unaokuja, kwa miezi mitatu tunauwezo wa kupata mafuta mengi na yakabaki ziada tukauza nje hatushughuliki nayo! Tunashughulika na michikichi iive baada ya miaka miwili, mitatu ndio ipatikane tunaendelea kuagiza mafuta kutoka nje.

Naomba Serikali tuwe tuna sehemu mbili, tuwe na long term kwa maana ya kupata viwanda vya mafuta na mazao ya mafuta kwa maana ya michikichi ambayo ni long term tutakuwa nayo, tuwe na short term ambayo ni alizeti ambayo leo Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda wakikubaliana kwamba wanatoa mbegu bora, wanasimamia masoko inapatikana kwa wakati na mafuta yanapatikana kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)