Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara

Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema. Naomba kuchangia mchango wangu katika bajeti ya Viwanda na Biashara kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu nazungumzia suala la viwanda vya kuchakata pamba katika nchi hii. Mikoa inayolima pamba katika nchi hii ni mikoa 17, lakini Wilaya 54 zinalima zao la pamba kwa ukubwa kabisa. Katika Ilani yetu ya uchaguzi tumeainisha kwamba tutatengeneza tani milioni moja katika nchi hii ndani ya miaka mitano kuanzia mwaka 2021 na kuendelea mpaka mwaka 2026. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kufikisha tani milioni moja kama hujajiandaa kuwa na viwanda. Ushauri yangu kwa Serikali katika Wizara ya Viwanda na Biashara; Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo ni miongoni mwa wasomi wakubwa wenye heshima katika nchi hii, mimi binafsi nakukubali na ninashangaa maono haya Mheshimiwa Rais aliyapataje ya kukufikiria kwamba Profesa Mkumbo anaweza akawa sababu ya kubadilisha maisha ya Watanzania, akakuweka katika hii Wizara. Sasa itendee haki hii Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba, Mheshimiwa Profesa Mkumbo, Waziri wa Viwanda na Biashara, andaa andiko, mimi najua wewe ni mwandishi mkubwa katika nchi hii, andaa andiko kwa ajili ya kuweka mashine za kuchakata pamba. Hizi mashine zilizopo katika vyama vyetu vya ushirika vya Nyanza, Shirecu, Musoma, Kagera kule Biharamulo, Tabora na Singida; hivi viwanda haviwezi sasa hivi kuchakata pamba kwa sababu mashine hizi zilikuwa za kizamani. Hizi mashine zimetoka India, kuna mashine zimefungwa kule Nyakalilo mwaka 1959, mashine zimefungwa pale katika ginnery ya kwetu Nyamililo, hizi ni mashine zimewekwa pale mwaka 1967.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mashine zimekuja kufungwa Buyagu Ginnery, hizi ni mashine za mwaka 1972. Lakini kuna mashine mpya ambayo imefungwa pale Manawa Ginnery katika Wilaya ya Misungwi, hii ndiyo mashine mpya peke yake katika Mkoa wa Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mashine zilizoko Nasa Ginnery, ukienda Nyambichi Ginnery Kwimba; hizi mashine zimechoka. Nenda Bariadi, hizi mashine zilizoko kule zimechoka; nenda Maswa, kiwanda kilichoko Maswa sasa hivi ni gofu. Majengo yapo na haya majengo ni imara; andaa andiko la kuweka mashine za kisasa ambazo gharama zake ni ndogo, ni dola 50,000 mpaka dola 70,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mashine hizi zikishachakata pamba andika andiko Mheshimiwa Profesa Mkumbo, kila Halmashauri ambako pamba inalimwa wawe na viwanda vya nyuzi. Lazima utenganishe kiwanda cha kuchakata pamba na kiwanda cha nyuzi. Hizi viwanda vya nyuzi vikiwa katika Halmashauri husika, huko hawa Wakuu wetu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na sisi Wabunge, tutahakikisha hili zao la pamba linatoa ajira kubwa kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini baada ya hapo nyuzi zitauzwa katika viwanda vikubwa. Tutakuwa tuna viwanda vikubwa katika makao makuu ya mikoa ambako pamba inazalishwa. Kule watatengeneza majora halafu yale majora yatashuka chini tena kwa ajili ya hao washonaji watakaokuwa wanashona nguo hizi. Kwa hiyo, watashona nguo na tutazalisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Profesa Mkumbo aende akajifunze Thailand. Thailand hawalimi pamba kama Tanzania, lakini leo ndiyo nchi ya kwanza duniani kwa kuzalisha nguo za watoto na nguo za akina mama. Pamba inatoka Tanzania, hatuwezi kukubali katika jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Profesa Mkumbo kaa ufikiri uwasaidie Watanzania na utapata heshima kubwa; ukibadilisha mapinduzi ya zao la kilimo na viwanda katika nchi hii utapata heshima kubwa sana. Na kule unakokwenda kutengeneza walipakodi, utakwenda kuwatengenezea kule katika kilimo. Mazao ya kilimo yakipata uchakataji mzuri katika nchi hii tutaiokoa nchi hii na ajira itapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema tunatengeneza ajira milioni nane; nini milioni nane, tutatengeneza ajira milioni 17. Kwa sababu tukiwa na viwanda sisi nchini, tujiondoe kuuza robota. Na usifikiri kutengeneza viwanda vikubwa, kuna viwanda vinakuja katika kontena la 20 feets au 40 feets, kontena dogo tu, kontena lile dogo linakaa hata makao makuu ya kata. Watalima pamba na watachakata robota. Uwe na viwanda vya kuchakata robota 35 mpaka 100, basi inatosha. Utaibadilisha nchi hii kuhusiana na suala la pamba. Kila Mbunge anayesimama hapa anazungumzia jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, kuna jambo ambalo linaonekana katika nchi hii halileti afya, suala la biashara ya Zanzibar na Tanzania. Hili jambo lazima liangaliwe kwa nguvu kubwa. Haiwezekani nchi inaitwa Tanzania Bara, Tanzania Visiwani tunaunda Tanzania, leo mzigo ukija ukaupitishia Zanzibar unaonekana umefanya jambo haramu katika nchi hii, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tengenezeni sera nzuri ya biashara katika nchi hii. Wazanzibari waone wana haki ya Muungano kuuza vitu hapa na sisi Watanzania tuone tuna haki ya kuuza bidhaa zetu Zanzibar. Haiwezekani kitu kama hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Wazanzibari hawatufurahii sisi kwa sababu tumefunga mpaka, yaani inaonekana kama mzigo unatoka Zambia au Uganda, haiwezekani kitu kama hiki. Kwa hiyo tengenezeni sera nzuri ya biashara, kwamba mzigo utakaoshuka Zanzibar kuja Tanzania Bara ni asilimia tano au kumi ulipiwe ushuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo biashara zetu za mipakani za sheria za Afrika Mashariki, hizi biashara zilizoko tumetengeneza majengo. Ukienda katika mpaka wa Burundi na Tanzania kule Kobelo, leo tunagongwa Kobelo, unagonga Kabanga, ukienda Rusumo, hali kadhalika. Ukienda katika mpaka wa Tanzania kule Misenyi, Mtukula, ukienda mpaka wetu sisi wa Sirari leo ule mlango wa Sirari unaonekana ukipitia Sirari unakuja wewe unakuwa kama unafanya biashara haramu, haiwezekani kitu kama hiki katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, angalieni hii biashara ya mipakani, Tanzania imeshuka katika biashara ya kuagiza mizigo nje ya nchi. Wekeni hizi kodi kwa sababu wewe ndiyo una haki ya kutengeneza walipa kodi wapya na wewe ndiyo una haki ya kulinda walipa kodi na wafanyabiashara katika nchi hii. Hii dhamana umeichukua wewe umepewa na Mheshimiwa Samia Suluhu kuhakikisha wafanyabiashara wanakua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nchi, Rais akija wa aina hii biashara inakufa, akija Rais wa aina nyingine biashara inapanda, haiwezekani katika nchi hii. Tengenezeni sera ya biashara wafanyabiashara tufanye biashara kwa amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na-declare mimi ni mfanyabiashara, lakini biashara nyingine tumeziacha katika nchi hii. Leo kuna biashara mfano kama sasa hivi nilitoa ushauri mimi, kuna biashara ya mifugo, hii biashara ya mifugo ni kubwa sana katika nchi hii. Leo mifugo wetu, ng’ombe wananunuliwa na watu wa Comoro, wanakuja kununua ng’ombe Kahama, Sengerema na Kwimba. Wale ng’ombe wanapelekwa Comoro wanalishwa miezi miwili wanakwenda kuuzwa Ufaransa, haya ni mambo ya ajabu sana. Kwa nini sisi tusitafute soko la ng’ombe Ufaransa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna soko kubwa kule Ghuba, wenzetu wanakwenda katika ibada ya Hijja sasa hivi. Hii ibada ya Hijja Mheshimiwa Profesa Mkumbo, ni kwamba mnatakiwa mkatafute soko hili la mbuzi na ng’ombe haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mbuzi anauzwa mpaka dola 200, 300 Saudi Arabia, wakati huyu mbuzi anauzwa kwenye masoko Kongwa, Sengerema na sehemu nyingine kwa shilingi 50,000, shilingi 70,000, anauzwa Saudi Arabia dola 300; sasa haya ni maajabu makubwa sana. Ng’ombe anauzwa shilingi 700,000, anakwenda kuuzwa dola 2,000 au 1,500 Jiddah. Sasa hili ni jambo ambalo hii ni kazi yako Mheshimiwa Profesa Mkumbo; hakikisha hii minada kwenye haya masoko yetu tuuze sisi wenyewe katika hizi nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna suala la kuweka viwanda vya nyama. Viwanda vya nyama katika nchi hii ni vichache kulinganisha na idadi ya ng’ombe tulionao. Tanzania leo ni nchi ya pili kwa mifugo ikitoka Botswana…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Tabasam kwa mchango wako mzuri, muda wako umemalizika.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Lakini kama umenikatia kidogo hivi maana yake bado nilikuwa naendelea kuserereka, ahsante sana. (Makofi)