Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Dr. Thea Medard Ntara

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, niungane na wenzangu wasemaji waliopita kama Mheshimiwa Mpina aliongea jana na Mheshimiwa Aida na huyu wa leo kwamba inabidi bajeti ya kilimo iongezeke na tufuate kabisa ile Maputo Declaration ambayo ilizitaka nchi za Afrika zitumie angalau asilimia 10 ielekezwe kwenye kilimo. Sasa ikielekezwa huko kwenye kilimo fungu hili likiongezeka Wizara itaweza kukuza kilimo lakini pia itaweza kupata mbegu bora kupitia seed science and research. Bila hivyo tutaendelea kununua mbegu nje, kulima karanga Dodoma halafu mnasema hazioti; hili tatizo ni kwamba fedha Wizara ya Kilimo hazitoshi.

Mheshimiwa Spika, Waziri wa Fedha atafute fedha ndiyo kazi yake, atafute fedha na zikipatikana ndiyo tunaweza kufanya vitu katika hii Wizara ya Kilimo. Haya mambo ya kuchukua mbegu kutoka nje au kutegemea nje maana yake ni kweli hatuna wanasayansi. Kuna Profesa anaitwa Susanne Nchimbi alitengeneza mbegu nzuri sana za maharage pale SIA na zikasambaa Tanzania. Kwa nini tusitumie hao wanasayansi wetu ili tupate mbegu ambazo hazitaleta utata zinavyooteshwa sehemu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia ni wakati sasa wa ku- intensify, kukuza na kupanua kitu kinachoitwa commercial farming; tusipokuwa na commercial farming hatuwezi kufanya biashara za kilimo. Tukifanya commercial farming ina maana kwamba hata hawa vijana wetu tutafanikisha hata hicho tunachosema irrigation schemes lakini kutegemea hizi mvua za misimu bado hatutaweza kuwa ni nchi inayoweza kuzalisha kwa ajili ya kuuza. Tukifanya commercial farming ina maana tutakuwa na mazao bora lakini pia tutaweza kutoa mafunzo (practical skills) kwa wanafunzi wetu wanaotoka katika vyuo vya kilimo lakini pia wanaotoka katika vyuo vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii tunasema hakuna ajira lakini hao Watoto wakiweza kwenda kujifunza kwenye hizo commercial farms itatusaidia hata wao kutengeneza vikundi na Serikali ndiyo hapo itapeleka fedha kwa hivi vikundi. Tunaweza kuwa na hivi vikundi kwenye mikao yote 26; wengine wakawa na kikundi wanalima karanga, wengine maparachichi Njombe, kikundi kingine cha hawa vijana ambao ni wasomi watapewa mikopo waweze kulima mahindi Ruvuma na wengine michikichi huko sijui Kigoma. Kwa hiyo, tukifanya hivyo tunaweza tukaendelea, watafute fedha.

Mheshimiwa Spika, kama World Bank inaweza/ imejipanga kufanya investment kwenye nchi za Afrika, dola bilioni 150 na Tanzania kwanini tukose hizo fedha. Waziri wa Fedha akatafute fedha, IFAD wanatoa mikopo tena ya bei nafuu, wakatafute fedha ili iongezwe kwenye Wizara ya Kilimo. Tukiendelea hiki kilimo cha kijungujiko hatufiki. Sasa hivi inatakiwa tuwe na mashamba makubwa ndiyo tutaweza kuwapa hao vijana mikopo waweze kufanya ukulima wa kisasa na wenye tija. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalize kwa kusema nawashukuru Wizara wameleta wanunuzi wa zao la soya huko Ruvuma lakini Ruvuma wanalima ufuta pia na mikoa mingine. Watafute na wanunuzi sio wanunuzi hawa wa kusema ulete sijui stakabadhi ghalani, tunataka mtu akipeleka zao anapata pesa yake palepale, wakulima ndiyo wanapenda hivyo. Lakini haya mambo ya kusema unaleta zao kama yalivyokuwa kule mambo ya tumbaku ndiyo yanaleta shida, upigaji unakuwepo mwingi sana hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa kule Tabora najua shida ya AMCOS, mtu akitoka kule ameiba hela ya wakulima anatoka pale ana pesa nyingi halafu anaingia mara Diwani, mara Mbunge. Walikuwa wanawaibia wakulima fedha siwasemi hawa wakina Mheshimiwa Gulamali lakini ndiyo kilichokuwa kinatokea kule Tabora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ninakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)