Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili na mimi niwe miongoni mwa Waheshimiwa Wabunge waliochangia katika bajeti ya Wizara hii ambayo ni Wizara muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri. Baada ya kumaliza kuwapongeza niendelee kuwapa pole, nawapa pole kwa sababu gani? Kilimo ni suala la kuwekeza kwa maana ya bajeti uone kwamba inaongezeka kwenda kwenye kilimo lakini kwa takwimu nilizonazo kwa mwaka 2018/2019, 0.5% ya bajeti ndiyo ilienda kwenye kilimo; mwaka 2019/2020 asilimia 0.63 pekee ndiyo ilienda kwenye kilimo; mwaka 2020/ 2021 ni asilimia 0.58 ya bajeti ndiyo ilienda kwenye kilimo na mwaka huu wa 2021/2022 ni asilimia 0.8 chini ya asilimia moja ndiyo inaenda kwenye kilimo. Tafsiri yake ni nini? Kama zaidi ya 65% ya Watanzania na 70% wakiwepo wanawake wanajishughulisha na shughuli za kilimo, lakini katika kutenga bajeti unaweka asilimia 0.8 tafsiri yake ni kwamba we are not serious. Kama tunataka kufanya transformation kuhakikisha kwamba Watanzania walio wengi wanaondoka katika lindi la umaskini ni kuweka fedha za kutosha kwenye sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu umefanya utaratibu mzuri naomba Waheshimiwa Wabunge katika hili tusimame pamoja. Kama tunataka yafanyike mapinduzi ya uhakika ni kuhakikisha kwamba Wizara ya Kilimo inaenda kuongezewa bajeti. Na katika utaratibu ambao umeuweka kwa makusudi hizi Wizara zingine pamoja na kwamba bajeti zao zimepita, tuungane Waheshimiwa Wabunge kuhakikisha kwamba Wizara ya Kilimo inaenda kuongezewa pesa ili tuweze kufanya mapinduzi na kuwasaidia Watanzania. Kwa hiyo, haijalishi bajeti ipi imepita kwa sababu bajeti ya mwisho ni bajeti kuu na sisi kama Wabunge tuna uwezo kabisa wa kuhakikisha Wizara hii inaongezewa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo linazidi kushangaza na kusikitisha, sisi Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa mikao mitano ambayo ni big five katika uzalishaji lakini kichekesho chake kinakujaje, katika ambao wapo miongoni mwa big five, ndiyo mkoa ambao unaongoza katika lindi la umaskini. Tafsiri yake ni kwamba hiki ambacho mwananchi anazalisha kinakosa thamani, unazalisha mahindi lakini kama huwezi kuyauza maana yake huna uwezo wa kwenda ku-transact na kuweza kupata fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali kwa ujumla wake katika hali hii ambayo wananchi wapo kwenye lindi la umaskini na huku wamezalisha wanatizama hicho ambacho umetoa jasho na damu yao hakina thamani, Serikali ije na majibu. Wanaenda kuchukua hatua gani ya makusudi kuhakikisha kwamba wananchi hawa ambao wanafanyakazi kwa bidii lakini wanaendelea kuwa maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimuombe Mheshimiwa Waziri na timu yake, tumelima mahindi miaka nenda rudi lakini tunazidi kuwa maskini. Naomba Serikali itujie na mazao mbadala, sasa hivi Serikali tulipata kota kwa ajili ya kupeleka soya beans China lakini niambieni wapi soya inapatikana na sisi kwa Mkoa wa Rukwa ardhi hiyo inafaa kabisa kwa kilimo hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ni vizuri Waziri ukatujia na majibu, unaenda kusaidiaje ili tuachane na habari ya kilimo cha mahindi ambacho kinatupa umaskini twende kwenye mazao ya soya, tukalime ngano ili na sisi tuondoke katika kundi la maskini na hiyo itakuwa imetusaidia. Vinginevyo tutakuwa tunalima, tunafanya kazi lakini tija haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miaka ya nyuma kidogo nchi ya Zambia ilikuwa kila mwaka wanategemea tulishe sisi Watanzania tuwalishe Wazambia lakini leo imebadilika yield per acre Wazambia kwa mahindi wanazalisha gunia 35, sisi Watanzania gunia 8 au 10, hatuwezi kufika. Pamoja na kuzalisha hizo 8 na 10 hata soko mwananchi hana la uhakika. Kama tunakubaliana sisi sote kwamba zaidi ya asilimia 65 au 70 wakiwemo wanawake lazima Wizara hii kwanza tuhakikishe kwamba bajeti inaongezeka ambayo ita-reflect uhalisia. Hii bajeti ambayo inakuwa chini ya asilimia moja hakika tutakuwa hatuwezi kufanya transformation ambayo inatakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa sababu naamini Wizara watakuja na majawabu ya uhakika badala ya majibu, naomba niunge mkono hoja, nakushukuru sana. (Makofi)