Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kupata nafasi kuzungumza lakini afya yangu sio nzuri nitazungumza kwa shida, Jimbo langu la Same Mashariki asilimia 99 mfano, wote ni wakulima kwa hiyo wao bajeti yote wanasikiliza Wizara ya Kilimo. Ninamshukuru Mheshimiwa Waziri ninamshukuru Naibu Waziri wote ni wachapakazi ninafahamu, lakini ninaomba niwaambie tatizo langu kubwa, Jimbo la Same Mashariki lina tarafa tatu na katika tarafa tatu tarafa mbili zinalima tangawizi tarafa moja inalima mpunga.

Mheshimiwa Spika, wamelima haya mazao kwa muda mrefu na hayo mazao ndio yanayowafanya nao waishi. Tatizo ambalo liko Same Mashariki ni kwamba kuna tatizo kubwa la miundombinu ya kilimo, miundombinu ya kilimo imekuwa imechakaa sana nikisema hivyo nina maana hawa wanaolima mpunga wanategemea scheme ya kulimia ule mpunga scheme ile imechoka na niseme kweli hili jambo ya scheme yangu ya Kata ya Ndungu nimeliungumza sana na Naibu Waziri na Naibu Waziri nakiri kwamba umeanza kulifanyia kazi nashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, lakini tarafa mbili Tarafa ya Gonja na Tarafa ya Mambavuna wananchi wangu wanalima sana tangawizi, na ninaomba niseme kweli katika Tanzania nzima Jimbo la Same Mashariki ndilo Jimbo pekee ambalo wananchi wanalima tangaziwi mno, sasa Mheshimiwa Waziri Jimbo ambalo wananchi ndio asilimia kubwa wanalima tangawizi na wanajitahidi sana. Ninaomba tukimaliza bajeti, ili Bunge la Bajeti Waziri twende wote tukaone hao wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, alikuja Rais Kikwete kwenye Kata ya Miamba ambayo Mheshimiwa Mbuge wa Peramiho umekuja juzi alikuja Rais Kikwete mwaka 2014 nikasimama jukwaani nikamlalamikia kwamba Mheshimiwa Rais wananchi hawa wanalima tangawizi vizuri wanashirikiana na Mbunge na tumejengwa na kiwanda cha Tangawizi, miundombinu imekufa nikiri na nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Kikwete alitoa shilingi milioni 800 akanipa kusaidia ile miundombinu ya kilimo cha tangawizi hiyo ilikuwa ni Awamu ya Nne, Awamu ya Tano, sikuwa Mbunge kwa hiyo sijui nina uhakika aliyekuwa Mbunge hakuzitafuta fedha kwa hiyo wananchi hawakupata zile fedha, sasa hii ni Awamu ya Sita… (Makofi)

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Naghenjwa Kaboyoka.

T A A R I F A

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, msemaji anaposema sikutatufa fedha wakati alikuwa anasema kiwanda kinafanya kazi ningetafuta fedha ya nini lakini ajue kwamba PSSSF walileta mashine mpya, kiwanda kilichokuwepo kilikuwa ni bomu.

SPIKA: Unapokea taarifa hiyo Mheshimiwa Anne Kilango.

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, sipokei huyu mama amechanganyikiwa ninaongelea Kilimo, naongea kilimo cha tangawizi siongei kiwanda amechanganyikiwa naendelea Mheshimiwa. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ninachoomba sasa ninakwenda kwenye kazi sizungumzi mambo hayo nakwenda kwenye kazi. Ninaiomba Serikali ya Awamu ya Sita, Serikali ya Awamu ya Nne iliona tatizo la miundombinu Rais akanipa shilingi milioni 800 na aliponipa alisema Mheshimiwa Anne Kilango jitahidi sana kila awamu ikupe fedha za miundombinu Awamu ya Tano sikuwepo Serikali haikutoa. Awamu ya Sita sasa ninaomba kwa unyenyekevu mkubwa Mheshimiwa Waziri tukimaliza Bunge hili ninafunga mizigo yangu ninakuja kukuchukua kwako, twende ukaona hayo matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, matatizo ya wananchi wangu ni matatizo yangu mimi, wao wamenituma nije niwasemee mimi sikuja hapa kucheza niwasemee wananchi wangu na leo nimekuambia tangu jana ninaumwa lakini nimekuja ili niwasemehe wananchi wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakuomba Mheshimiwa Waziri Tarafa ya Bonja na Tarafa ya Mambavunda twende mimi na wewe ,tarafa ya Ndungu nitakwenda na Naibu Waziri naomba niseme ninaunga mkono hoja kwa sababu ninajua Mheshimiwa Waziri tutakwenda ninaunga mkono hoja tena sina mahali ninapoleta vuruga na wewe ahsante sana. (Makofi)