Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Kipekee namshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai. Niunge hoja mkono nisije nikasahau kwa sababu hii Wizara ni muhimu sana kwangu japo siku zote naishia kuomba kuomba, lakini wananchi wangu hawafikishiwi maombi yangu wala hawajibiwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mifugo ni Wizara ambayo kwa kweli kila mtu anastahili kuwa karibu kwa sababu, sisi kina mama tukishajifungua siku hizi unaambiwa miezi sita wasinyonyeshe, lakini baada ya hapo mtoto anaweza akapewa maziwa mengine kidogo; na kama wewe ni Mtanzania mzuri, basi utamchanganyia maziwa ya ng’ombe au kama kuna wale wenye mbuzi wazuri, maziwa ya mbuzi kidogo, mtoto anaendelea kunyonyeshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mara chache sana utakuta mama wa Kitanzania anapenda maziwa ya unga. Sasa naomba kuiambia Wizara hii kwamba, hiyo mifugo tunayohesabiwa kwamba iko ranchi, ng’ombe milioni 33, lakini sasa tunaambiwa ng’ombe wa maziwa ambao ni mitamba itasambazwa milioni moja na ushee. Sasa naangalia, hivi hiyo milioni moja na ushee itakayosambazwa Tanzania kwa ruzuku, itawafikia wafugaji wangapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hiyo figure iangaliwe vizuri, kwa sababu Kilimanjaro, wakati amekuja kuzindua kampeni, Waziri Mkuu aliombwa; tunaomba mitamba ya ng’ombe, tunaomba mbuzi wa maziwa na pia aliombwa, vifaranga wa kuku wa kienyeji kwa kila mwanamama. Huko Kaskazini Kilimanjaro sisi hatujui kusweka ng’ombe, wanafuga kwenye zero grazing. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwombea sana Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mungu amlaze mahali pemba Mbinguni kwa sababu peke yake ndiye aliwafanyia wale watu wakafuga kwa faida kwenye miaka ya 85 mpaka 87. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, alitoa mitamba bora na leo nimemsikia hapa ametajwa Mheshimiwa Kimiti, alikuwepo kwenye Bunge hilo. Mitamba ile ikasambazwa ndiyo wakabadili kutoka kwenye ile indigenous breed wakaja kwenye hybrid. Kuanzia wakati huo, wakaweza kukamua maziwa lita 20 kwa ng’ombe mmoja kutoka lita mbili kwa ng’ombe. Sasa, ni kipindi kirefu na mpaka sasa wameshapoteza ile mbegu. Kwa hiyo, uzalishaji umeshuka, namuomba sana Waziri wa Mifugo ambaye amezoea ng’ombe wengi lakini sijui wanakamua kiasi gani atufikirie tena Kaskazini tupate hiyo mitamba mizuri. Kopa ng’ombe, lipa ndama! Na hapo ndiyo tutaweza kuboresha tena mifugo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba kama zoezi hilo litafanikiwa basi hata uchumi wa wananchi kule utabadilika. Lakini sio hiyo tu kwa ajili ya ng’ombe wa maziwa. Hata hawa ng’ombe wanaofugwa nje, nadhani hali sio nzuri. Ng’ombe ana kilo 100 hadi 120. Ng’ombe mzuri anatakiwa awe na kilo 300, mzungumzaji aliyezungumza kabla yangu ameeleza vizuri sana na mimi nasisitiza kwamba ni bora sasa tukaingia katika ufugaji wa tija kuliko ufugaji huu wa kuangaliangalia tu kubahatisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii nihame sasa kwenye ng’ombe lakini nimalizie kwa kusema ng’ombe wakiwepo nyumbani tunapata samadi ambayo inaboresha mashamba yetu ikiwemo kahawa. Ni juzi tu kimefunguliwa kiwanda cha viatu vya Ngozi pale Karanga. Tunategemea ng’ombe hawa hawa wa Tanzania watupe Ngozi nzuri na sio tukaagize ngozi kuja kutengeneza viatu hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihamie sasa kwenye eneo ambalo nina passion nalo. Kuku wa kienyeji. Niwapongeze sana ALVI wameweza kuja na mbegu ya Horace, katika ule ukurasa wa 11 tumeelezwa ambayo itaweza sasa kutengeneza kuku wa asili ambao ni wazito na ambao wanaweza wakatoa kilo nyingi na mayai mengi.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Ninachoomba tu…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Shally subiri taarifa ya Mheshimiwa Dkt. Mwigulu.

T A A R I F A

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO; Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango mzuri anaotoa mama yangu Mheshimiwa Mbunge pale. Kama ilivyo na ndizi Moshi, Bukoba, mchele wa Kyela na Shinyanga kuku wote wale anaowasema wa kienyeji ni kuku wa Singida na Dodoma, hiyo ni Fahari ya Makao Makuu. Akisema wa asili inaanza kuonekana kama dawa ya kienyeji hivi. Kwa hiyo, aseme kuku wa Singida na Dodoma. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Shally.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea Taarifa, lakini nataka tu nimwambie kwamba kisayansi hilo jina la mkoa alioutaja bado halijaingia na nachangia kutokana na hotuba ya Mheshimiwa Waziri na haya majina ninayoyatamka ndiyo yaliyoandikwa. Lakini, Tanzania tunajua. Hata ukifika Chako ni Chako unauliza kuku wa Singida wapo, lakini kwenye vitabu bado kuku wa Singida hamna. Kwa hiyo nishukuru sana kwa hilo na atakapopelekewa maombi kwamba anigawie kidogo ili wafike kule Kilimanjaro basi asiwe mchoyo kwa vile yeye ndiyo mwenye fungu lote lile la fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe pia pongezi kwa ugunduzi wa chanjo mpya inayoitwa tatu moja. Chanjo hii iko kwenye ule ukurasa wa 37 ni ya kuzuia magonjwa matatu, mdondo wa kuku, ndui ya kuku, mafua ya kuku na hiyo dose kichupa kimoja cha shilingi 6,800 kinatibu kuku 200. Kwa hiyo, mtu wa kawaida akinunua kichupa kimoja amemaliza kazi. Kwa hiyo, naomba sana kwa kweli niwapongeze watafiti hawa walioweza kuleta chanjo hiyo na hivyo basi niseme nmtakaopatiwa vifaranga hao kwa wale wanawake wa Kilimanjaro hata hatutakuwa na uoga wa maradhi ya kuua hao kuku. Pia tutapata samadi ya kuku au inaitwa kinyesi cha kuku lakini mbolea ya kuku kwa ajili ya mashamba yetu na bustani zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme wazi, hakuna bajeti iliyopita hapa, huu ni muongo wangu wa tano bila kuomba vifaranga hivyo. Swali nimeuliza nikaambiwa nikanunue hivyo vifaranga kwa shilingi 2,500 bei ya ruzuku. Sasa sitaki wa kwangu, nataka Wizara ifanye pilot scheme mkoani Kilimanjari akina mama wale wafuge kwenye nyumba zao na pia iweze kufanana katika hali ya ufugaji wa kawaida. Nimechoka kusikia tunahesabiwa mifugo iliyo kwenye mashamba darasa, iliyo kwenye ranch, sasa inafanya nini huko? Yaani tutaje figures za nini? Niseme wazi kwamba kwa kweli…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, oh! Basi niulize tu swali moja. Nilikuwa na swali moja ili nisije kusema nashika shilingi nikakosa hata haya mambo ninayoomba. Bodi ya Wizara kwa umoja wao mwaka huu walitoa gawio la shilingi 348,940,989 ukilinganisha na trilioni 1.5 iliyotolewa mwaka wa 2019 ambayo ni anguko la asilimia 77. Ni nini kilichosababisha hiyo? Nilidhani sasa wangetoa gawio kubwa lakini wameshuka. Naomba watakapokuja kujibu nijibiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono tena. Ahsante. (Makofi)