Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Amour Khamis Mbarouk

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tumbe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nikupongeze kwa namna unavyotuongoza, lakini pia niwapongeza sana Waziri wa Wizara hii na Naibu wake kwa kazi nzuri sana wanayoifanya ndani ya nchi yetu na kwa kufuata Ilani ya Chama chetu Cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumzia habari ya wavuvi na wafugaji, mimi ni mvuvi niliwahi kuvua kwa miaka mingi sana. Kwa hiyo, najua kwamba wavuvi hawana elimu maalum, wavuvi wetu wengi sana wanavua kwa mirathi yani kwa elimu ya mirathi. Jinsi mtu alivyomkukuta baba yake anavua ndivyo hivyo anavyovua na yeye na sina hakika kwamba wizara hii imeweka siku kwamba itakutana na wavuvi ana kwa ana kuwasiliza changamoto zao kule waliko au wataandaa mafunzo juu ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, ni kwamba hawa wavuvi wengi hawavui kwa sababu ni kazi anayoipenda kwa sababu uvuvi ni kazi hatari sana, ni sawasawa na mtu anapopanda mnazi yaani wakati wowote unaweza kusikia chochote na hasa kwa kuzingatia vyombo wanavyovitumia, kuelekea katika mazingira hayo ya uvuvi. Kwa hiyo, naiomba Serikali sana, badala ya kuchukua maamuzi ya kuchoma tu nyavu au kutunga tu sheria ngumu walikuwa wafikirie sana namna ya kuwaendeleza wavuvi. Nasema hivyo kwa sababu, kwa mfano, Serikali inapotaka kupitisha njia eneo inapitisha barabara wanafika mahali wakikuta kibanda cha mtu kwa sababu ya kuthamini binadamu yule wanaamua kumlipa fidia. Lakini kwa bahati mbaya sana mvuvi hafanyiwi hivyo inachukuliwa tu nyavu kwa sababu ya kigezo cha uvuvi haramu inachomwa au kitu kingine chochote kinaangamizwa bila kufikiria kumbe Serikali ilitakiwa ikinunue kile kwa sababu na yeye ndio maisha yake. (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, sawa sawa na nyumba au ardhi inayopatikana wakati inapopitishwa barabara. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali iwahurumie sana wavuvi wanafanya kazi hatari sana na sisi kama Serikali hatujafikia kiwango cha kuwaendeleza moja kwa moja. Huwa nachukulia mfano ingekuwa yule mvuvi ni mtoto wangu siningempa mtaji nikamnunulia chombo kizuri sana mashine nzuri, mitego mizuri lakini Serikali inatakiwa ijue kwamba wale wavuvi ni kwa ajili ya mapato ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo na wao ipo haja ya kuwaandalia utaratibu wa kuendesha maisha yao lakini pia na pato kwa Serikali. Jimbo langu sehemu kubwa sana imepakana na bahari ya Hindi na pale kuna wavuvi na mara nyingi sana wavuvi hawa wanaenda kuvua mbali sana lakini Serikali bado haijaweza kuweka ulinzi huko wanakokwenda, sina hakika kwamba Serikali hapa Tanzania Bara kwa mfano imeweka vyombo maalum huko baharini kwamba wavuvi wakipata tatizo lolote wanaenda kuokolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hilo halipo naomba sana Serikali ifanye hivyo kwa sababu uvuvi ni kazi hatari sana na sisi wote naamini kila anayemsomesha mwanae uvuvi hampi chombo kwenda kuvua baharini bali anamtafutia eneo zuri kwenye Serikali awe mhudumu ofisini ili awasimamie wavuvi. Kwa hiyo, bado uvuvi na changamoto kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ndipo tunapotakiwa sasa kutumia sayansi yetu tumesoma sayansi kwa muda mrefu sana na Tanzania wanasifiwa sana kwa wanasayansi, na hapa ndio tunatakiwa kuitumia vizuri sana kwa kuelewa ni eneo gani lina Samaki ili Serikali ipate faida kubwa zaidi, kama hautujaweza kutengeneza vifaa vitakavyotuonesha kwamba hapa hili eneo kuna, Samaki tukawatayarisha wavuvi wetu wawe katika utaratibu huo, elimu hiyo, basi tusitegeme kwamba sekta hii ya uvuvi itakuwa nzuri. Kwa sababu mpaka sasa hivi wavuvi wetu wanavua kwa kubahatisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu ana ring net anaenda kuzungusha anavua hamna kitu mara mbili tatu, bado tunabahatisha. Haya maeneo tajiri sana sisi watanzania Mwenyezi Mungu ametubariki sana maeneo haya ya uvuvi tuna maziwa mengi, lakini tuna bahari kubwa sana ya Hindi. Kwa nini hadi leo hatujafikia mahali bahari ya Hindi ikatuneemesha? Na kila mtu anajua kwamba bahari ni tajiri mbali ya Samaki kuna mambo mengi sana ambayo ni ya kufanya nchi yetu iwe tajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, bado Serikali haijafikia maamuzi ya kuandaa utaratibu wa kuwanufaisha wavuvi, na wahudumu wengine wa bahari lakini pia kwa kupata mapato makubwa zaidi. Naomba sana Serikali iwafanye wavuvi ni watoto wao lakini pia ni waajiwa wao kama vile wanavyohudumiwa walimu sisi Wabunge na wafanyakazi wengine ndivyo wahudumiwe wavuvi, kama kweli tunahitaji wavuvi walete tija ndani ya nchi hii vinginevyo tutawapelekea wavuvi hasara ndio maana hapa nina tarehe 3 Novemba, 2018 kuna wavuvi walikamatwa kesi yao haijulikani iko wapi lakini walipelekwa mahakami ni watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwaelekeze lakini pia Serikali kuna wavuvi walipigwa mpaka risasi kwa nini?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana naunga mkono hoja na nawatakia heri sana Waziri na Naibu wake na wewe mwenyewe, ahsante sana. (Makofi)