Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Furaha Ntengo Matondo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuweza kuchangia katika Wizara njeti ya Mifugo na Uvuvi. Pia napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia afya njema na kuweza kusimama siku ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza, napenda kumshukuru Waziri, Naibu Waziri, Makatibu wetu wote na wadau wa mifugo na uvuvi kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. Napenda sana kuishukuru Serikali kwa kazi nzuri ambayo imefanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoka Mkoa wa Mwanza, tumezungukwa na ziwa. Tulikuwa na changamoto moja kubwa sana. Wavuvi wetu hapo nyuma walikuwa wanapata shida sana, wakitoka wilaya moja kwenda wilaya nyingine ni lazima walipe. Tuna wilaya saba katika Mkoa wetu wa Mwanza, unamkuta mvuvi mmoja kwa mwezi mmoja analipa mara saba. Kwa kweli ilikuwa ni kero kubwa sana na iliwasumbua sana wavuvi wetu, lakini nipende kuishukuru Serikali kwa sababu kero ile iliweza kuondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naipongeza Serikali na kuishukuru kwa kazi nzuri ambayo ilifanya kwa wavuvi wetu; tulikuwa na desturi ya mvuvi mmoja ikifika Januari unatakiwa kulipa leseni na ukishindwa unapewa faini mwezi Januari huo huo au Februari. Sasa tumepewa kipindi cha miezi mitatu, mvuvi anajianda na kuweza kulipa kuanzia mwezi wa Kwanza mpaka mwezi wa Tatu wanalipa kwa hiari, lakini kama hatalipa, atakwenda kulipa kwa faini ifikapo mwezi wa Nne. Naishukuru sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuiomba Wizara ya TAMISEMI pamoja na halmashauri zetu, tuna kero kubwa sana katika Halmashauri zetu. Tuna wavuvi wadogo wadogo ambao kwa Kiswahili kizuri, wanavua kwa kasia ambayo ni mitumbwi midogo ya futi 14; lakini tuna mitumbwi mikubwa ya futi 28 mpaka 30 ambayo inatumia engine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajikuta wavuvi wale wanalipa ada ya leseni sawa na mvuvi mwenye mitumbwi ya mashine. Ni kero na inawaumiza sana wavuvi wetu, hawawezi kujikomboa kutoka kwenye hali ya umasikini wakaenda kwenye kipato cha kati. Naomba sana Wizara husika iweze kuingialia kati na kuona hili suala. Napenda kuiambia Serikali, mchango wangu ni kwa wale wavuvi angalau kama Halmashauri inalipa 100,000/=, wavuvi wa kasia waweze kulipa shilingi 50,000/=. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ada ya ushuru kwenye mitumbwi. Wanapewa kulipa mitubwi sawa na mtumbwi wa mashine, kiasi kwamba mitumbwi ya kasia wala haiwezi kwenda sehemu yoyote mbali. Unaukuta mtumbwi wa mashine unatoka Mwanza mpaka Bukoba, lakini unakwenda kuleta mazao unakuja kuuza Mwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtumbwi wa kasia hauwezi kutoka hapa mpaka hata kisiwa kingine, kwa sababu ukipanda kwenye ule mtumbwi kwanza unayashika hata maji; ni mtumbwi mdogo, ni mtumbwi hatarishi, ni mtumbwi ambao watu wanajitafutia chakula. Naomba sana viongozi wetu na Serikali yetu iweze kuliona hili suala. Ushuru unaolipwa kwenye mtumbwi wa mashine wasipewe hata wale wengine kulipa kwenye mtumbwi wa kasia. Hii inawaumiza sana wavuvi wetu wadogo wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimechangia hapa hata muda ulioisha, nikaomba sana, wavuvi wetu wadogo wadogo waweze kutoka kwenye hali waliyonayo, Serikali iweze kuwatambua na kuwapatia mitaji waweze kutoka, lakini kila wakati wanabanwa. Wakitaka kujikwamua huku, wanabanwa, kweli watatoka? Hili suala ni gumu, lakini nina imani Serikali ikiingilia kati, hili suala litakuwa jepesi na watafanya kazi kwa weledi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba, tuna vijana wetu ambao wamemaliza vyuo vikuu, lakini hawajapata ajira. Ni wafugaji wazuri sana wa samaki, tunapata shida. Wananchi wengi wanatafuta jinsi gani ya kuweza kujikwamua kuchimba mabwawa hata kupata kipato, lakini hakuna wataalamu. Halmashauri zetu hazina wataamu wa ufugaji wa Samaki. Hebu niiombe Serikali iweze kuwachukuwa wale vijana, waweze kuji-organize, wapewe mtaji, wataweza kuwasaidia hata wananchi wetu ambao wanahitaji kufanya ile kazi, lakini hawana utaalamu. Unakuta hata kwenye Halmashauri husika, mtaalam ni mmoja, Halmashauri nzima inawezaje kuhudumiwa na mataalamu mmoja wa ufugaji wa Samaki? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Wizara husika iweze kuliangalia hili suala angalau ipitie kila Halmashauri waweze kuajiriwa hawa vijana waweze kuleta weledi katika nchi yetu. Nina imani kubwa ufugaji wa samaki unaleta pato kubwa sana katika nchi yetu na walaji wetu wa samaki wanaweza kupata protein za kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la ulinzi au salama wa wavuvi wetu wakiwapo ziwani. Wavuvi wetu wameachwa sana. Wavuvi wetu wanaliletea Taifa letu pesa nyingi sana, lakini hawajaliwi kabisa. Nikitoka Goziba nikija Ukerewe, Rolia, Muleba hakuna Kituo cha Polisi (Police Marine) cha kuangalia usalama wa wavuvi wetu na wafanyabiashara wanaoishi kandokando ya ziwa. Hii inaumiza sana kwa sababu wale watu wasipoangaliwa kila wakati wanavamiwa ziwani; kila wakati wananyang’anywa mashine; kila wakati wanaumizwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iweze kufuatilia hili suala, iweze kuwapatia hawa watu waweze kuwa na ulinzi ambao utawasaidia hata wakiwa wanafanya kazi zao waweze kufanya kazi zao lakini wakiwa wametulia na akili zao zikiwa kabisa ziko vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wanawake wenzetu ambao wako katika hali ya kufanya biashara ndogo ndogo katika mihalo. Wale akina mama ni wachakarikaji, nilishasema last time wakati naongea hapa. Naomba sana Serikali iweze kuona hili suala waweze kupatiwa mitaji wana biashara ndogo ndogo za kuchukua dagaa, lakini unawakuta wale akina mama wanaanika dagaa kwenye mchanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale dagaa wanakuwa ni wachafu na hata hawawezi kuliwa wakawa ni chakula cha binadamu. Naomba wapatiwe mitaji waweze kutengenezewa chanja. Zile dagaa wakianika kwenye chanja wanaweza kujipatia kipato kikubwa, lakini pia wakaingia hela Serikalini, nao wenyewe wakajikwamua kutoka kwenye umasikini walionao wakaingia hata kwenye hali nyingine. Wanahangaika sana siku hadi siku. Siku zinavyozidi kukatika lakini hawapati chochote, hali inakuwa ni ile ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, Serikali yetu ni sikivu, imejaribu kutusikiliza sana kila wakati. Kwa hiyo, naomba sana kuhusiana na hii kero ya wavuvi wadogo wadogo kutoa tozo. Kwa kweli inaumiza. Hata ukiuliza, yaani inaumiza sana. Waweze kutoka katika sehemu ya tozo ambazo ni sawa na mitumbwi mikubwa, angalau wapate tozo ambazo ni tofauti na wengine. Nina imani sana, ikiwa hivyo itasaidia sana wavuvi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wavuvi wetu wanakwenda ziwani, wanafanya kazi ngumu, wanafanya kazi kubwa, lakini wanapoleta mazao yao, hawana sehemu ya kuonesha kwamba tuna masoko yetu ya kuuzia samaki ambayo nikileta mzigo wangu, nikipeleka soko fulani nitapata faida.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)