Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Eric James Shigongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nianze na pongezi kwa Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi kubwa ambayo wameifanya kwenye Wizara hii. Nina siku mbili tu tangu nimerejea na Mheshimiwa Naibu Waziri kutoka Jimboni kwangu ambapo tumesafiri pamoja kwa mtumbwi mpaka kwenye visiwa ambako amekutana na wavuvi na kusikiliza kero zao; nampa pole sana kwa shida aliyoipata wakati tunapita ziwani kwani alijua asingeweza kurejea mahali hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa inafanyika katika nchi yetu kwenye suala zima la uvuvi ambalo nitachangia kwalo. Nataka nizungumzie sana suala la uvuvi kwa sababu eneo/Jimbo langu lina visiwa 32 na asilimia 35 ya watu wanaoishi eneo lile wameajiriwa kwenye uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze kwanza kwa kusema kwamba kama kweli kama Taifa tuna dhamira ya dhati kabisa ya kukuza uchumi wa nchi yetu, ni lazima sasa tuanze kutumia zawadi ambazo Mungu ametupatia; zawadi mojawapo ni uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu imebarikiwa kuwa na vitu vingi sana, ukienda huko Liganga kuna mlima wa chuma, kando yake kuna mlima wa mawe; vyote hivyo Mungu alitupatia. Ni wakati wetu sasa kuanza kuvitumia vitu hivi, hatukuvinunua, Mungu alitupatia kama zawadi na ile sisi maisha yetu yabadilike ni lazima sasa tuanze kuvitumia, hilo ni jambo la kwanza ambalo nilitaka kuwakumbusha Watanzania wenzangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo moja kubwa na kama hotuba yangu/mchango wangu huu ungepewa jina ungeitwa contribution of political will kwenye development. Tunazungumza mambo mengi sana mazuri, nakaa hapa ndani nasikia michango mizuri najiuliza what is wrong with us; watu wanajua jinsi ya kutoka mahali tulipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokikosa kabisa kwenye Taifa letu ni political will, utashi wa kisiasa. Bila utashi wa kisiasa hatutoki mahali tulipo na ndio maana nataka kusema ni lazima sasa tuanze kuwa na utashi wa kisiasa na determination na commitment ya kwamba ni lazima uvuvi ubadilishe maisha ya nchi yetu, ni lazima uvuvi utupandishe kutoka tulipo kwenda hatua ya juu zaidi; bila ya political will hatupigi hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze kwa kusema kwamba zawadi tulizopewa na Mungu zipo underutilized, ziwa letu na bahari yetu vipo underutilized; ni wakati wa sisi kuanza kuvitumia hivi vitu kuleta maendeleo ya nchi yetu. Kwa mfano, nataka nikupe data ndogo tu, mchango wa uvuvi kwenye GDP yetu kwa mujibu wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri ni 1.7 percent, wakati huo tuna maziwa yote na bado kwenye bahari yetu tuna maili 200 kutoka ufukweni, zote ni za kwetu tunaweza kufanya chochote. Nchi ya Uganda ambayo ina asilimia 45 tu ya Ziwa Victoria na Tanzania ina asilimia 49, GDP yake ni asilimia 12 mchango wa uvuvi. Ukianza kuona hivyo lazima ujue hapa kuna tatizo/kasoro ndio maana nasema kuna mambo ambayo wenzetu wanayafanya sisi hatuyafanyi, tunahitaji political will. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma Sheria ya Uvuvi ya Uganda ya mwaka 2018 na Sheria ya Uvuvi ya Tanzania yam waka 2003 nimegundua kwamba sheria yetu sisi imejielekeza zaidi kwenye ku-control lakini sheria ya wenzetu imejielekeza kwenye ku-facilitate. Hivyo basi, kama sheria yetu inaelekea kwenye ku-control, kila siku tutakuwa tunakamatana na wavuvi wetu, kuwachomea nyavu zao; jambo hili sio sahihi hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tujielekeze kwenye sheria ambayo ita-facilitate wavuvi wetu kuweza kuvua na kujipatia kipato na kuchangia kwenye GDP ya nchi yetu. Kama mambo haya hayawezi kufanyika nataka nikuhakikishie kabisa mchango wa uvuvi utaendelea kuwa mdogo kwa maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, samaki wanachangia asilimia 20 ya protini ya wanyama katika nchi yetu. Kwa Uganda natolea mfano, samaki wanachangia asilimia 50 ya protini ya wanyama. Matumizi ya samaki wa Tanzania kwa mwaka kila Mtanzania anatumia kilo 5.5 tu lakini wenzetu ni kilo 15 mpaka 20. Ni lazima tufike mahali sasa tuamue kwa dhamira moja kabisa ya kuhakikisha kwamba watu wetu wanatumia samaki. Jimboni kwangu samaki imekuwa kitu expensive, watu wa kawaida hawawezi kumudu samaki kwa sababu gharama yake imekuwa kubwa sana. Sasa tufanye nini? Ili uvuvi wetu uchangie kwenye pato la Taifa letu, ili uvuvi wetu uwe na impact kwenye uchumi wetu ni lazima kama nilivyosema tuanze kuhakikisha kwamba kuna political will (dhamira ya kisiasa), tusije hapa kuzungumza tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunatoa michango mizuri sana, lakini kama hakuna political will hatupigi hatua. Kama Mheshimiwa Waziri hapa hawataachana na hofu na kuanza kutenda, hatupigi hatua hata kidogo. Tutabaki nyuma, tutaendelea ku-lag behind hatuwezi kukuza uchumi wa nchi yetu. Hatuwezi kuendelea namna hii, ni lazima tubadilike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya nchi hii TBS wana kipimo chao cha nyavu na Wizara ina kipimo chake cha nyavu. Lazima hawa watu wawili wakae pamoja na wakubalianeā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.