Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Nashon William Bidyanguze

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nimpongeze Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayofanya. Lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa jinsi alivyoweza kutatua mgogoro wa wavuvi katika Mkoa wa Kigoma kwa maana ya Majimbo matatu; Kigoma Kaskazini, Kigoma Mjini na Kigoma Kusini ambalo ndilo jimbo langu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli ametusaidia sana pale ambapo walikuja wale wavuvi na wakaja na agenda zao zilizosababisha Mheshimiwa Waziri kifuta baadhi ya kanuni ambazo hazikuwa rafiki. Mheshimiwa Waziri, nakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze Serikali kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa jinsi ambavyo mpango wa Serikali uliopo ni wa kuhakikisha kwamba inanunua meli za uvuvi katika Bahari Kuu ili nasi tuweze kufaidi samaki wale ambao watatusababishia kuongeza Pato la Taifa katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli tunasikitika sana wananchi tunapoona kwamba tunalo ziwa kuu lakini tumekuwa hatupati faida itokanayo na samaki wale katika ziwa kuu. Lakini inaonekana mpango wa Serikali ni kwamba sasa itanunua meli nne ambazo zitahakikisha kwamba zinavua samaki ambao watasababisha tupate mapato makubwa kutoka kwenye chanzo hiki cha mapato ambacho tumekiacha kwa muda mrefu. Hii naomba niwapongeze Serikali kupitia kwa Mheshimiwa Waziri kwa hii ambayo itakwenda kuongeza uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, alivyomaliza kutatua ule mgogoro katika zile kanuni kwenye jimbo langu pamoja na majimbo ya wenzangu wa Kigoma ambayo nafahamu kabisa utatuzi ule alikuwa anaendana na wavuvi wale wa Ziwa Tanganyika lakini katika Mkoa ule wa Katavi pamoja na Wilaya ile ya Tanganyika, na wenyewe walikuwemo katika ule ujumbe. Nina imani kwamba ukanda wote ule tatizo sasa hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo moja; naomba uige mfano wa Wizara ya Madini ambayo ina wachimbaji wadogo. Lakini wachimbaji wadogo wale wamewekewa utaratibu ambao Serikali imewatambulisha kwenye mabenki na sasa wanakopesheka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wavuvi wetu katika Ziwa Tanganyika wanatumia vifaa ambavyo ni duni. Na ndiyo maana wakati mwingine samaki hawawezi kupatikana vizuri kwa sababu hakuna utaalam wa kisasa. Naomba katika eneo hili wavuvi wa Ziwa Tanganyika, pamoja na maeneo mengine waweze kukopesheka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atengeneze utaratibu kama ambavyo Wizara ile ya Madini imeweza kufika mahali sasa wachimbaji wadogo wanaweza kukopesheka. Hii sekta ya uvuvi pia ni sekta muhimu. Wakopesheke. Pia Wizara iweke utaratibu namna ambavyo baada ya kupata samaki wale waweze kuhifadhika kwenye majokofu ili waweze kuuzwa hata baadaye, lakini samaki wanapopatikana bado wabichi wanalazimika kuwauza harakaharaka ili wasiweze kuoza. Sasa wanapoteza fedha kwa sababu hawawezi kuweka, lakini kama wataweka maana yake watauza wakati ambao soko lipo. Hili naomba Mheshimiwa Waziri ulichukue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye eneo la ufugaji wa ng’ombe kwa maana ya mifugo. Amezungumza mchangiaji mwenzangu kwamba Wasukuma ndio watu ambao kwa kweli wanajishirikisha na mifugo. Jimbo langu lina vijiji 61; wote wanaofuga ng’ombe pale wao wanaochunga ng’ombe kule katika vijiji vile ni Wasukuma, sisi Waha hatufugi ng’ombe. Kama vile Mheshimiwa Spika alivyokuwa akizungumza kwamba Serikali haifugi ng’ombe na sisi Waha hatufugi ng’ombe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba, ng’ombe wale ni wengi. Katika wilaya yangu ile, kwenye jimbo langu, tuna ng’ombe takribani 200,000 na hawa ng’ombe wamezagaa. Hakuna mpango wowote lakini wanasumbua wananchi ambao wanajishirikisha na kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika eneo hili naomba nimshukuru Waziri kwa sababu alifika jimboni kwangu akaenda kutatua mgogoro ambao kwa kweli ulikuwa ni mkubwa katika eneo moja, ingawaje maeneo mengine hakufika, pale ambapo aliruhusu kwamba kwenye eneo ambapo alitoa hekta 6,000 ziweze kutumika kwa wafugaji. Hilo ni jambo ambalo wananchi wamelifurahia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona bado kuna eneo lingine, kwa mfano kata nane za ukanda wa maji, bado hukufika na hukutoa maelekezo yoyote, na huko ndiko kwenye matatizo ya kuingiliana wale wafugaji wanapoingia kwenye maeneo ya wakulima. Kesi ziko nyingi mno na ng’ombe wakishaingia kwenye shamba, hata ungeenda mahakamani, kesi inaamuliwa kwamba ng’ombe ndio wamekula; sasa unashitakije ng’ombe? Inakuwa ni ngumu sana. Kwa hiyo, naomba katika eneo hilo Wizara iweze kuja na mpango wa kuhakikisha kwamba hizi ranchi ambazo zipo ambazo hazitumiki basi ziweze kutumika sasa katika kipindi hiki ambacho hazitumiki Wizara iweze kuwapa wananchi waendelee kuzitumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tunajinasibu kwamba sisi nchi yetu ni nchi ya tatu katika mifugo. Sasa Serikali katika eneo hili imefanyaje? Imewatengea maeneo gani? Unakuta ni migogoro. Kwenye maeneo ya wakulima kuna migogoro ya wakulima, lakini kwenye maeneo ya ranchi wakati mwingine pia wakiingia kwenye ranch kuna matatizo tena katika maeneo hayo. Sasa nadhani Wizara ingekuja na mpango ikatenga maeneo kwa ajili ya hawa ambao nao ni wafugaji na ni eneo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimalizie kwa kusema kuwa eneo hili Serikali bado haijawekeza. Kwa sababu jiulize; hawa ng’ombe 200,000 katika jimbo langu, kuna majosho mawili tu. Sasa tunasema nchi yetu ni nchi ya tatu katika mifugo kwa Afrika, sasa kwa nini tusifike mahali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)