Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Asya Mwadini Mohammed

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. ASYA MWADINI MOHAMED: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuweza kunipa nafasi nami niweze kuchangia hotuba hii ya Wizara muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, naomba ninukuu Taarifa ya Kamati ya Bunge ya mwaka 2018 ambayo inasema kuhusiana na shughuli za uvuvi wa Bahari Kuu, kama utasimamiwa vizuri ipasavyo, basi Serikali tunaweza kuiingia pato la moja kwa moja shilingi bilioni 352. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali kadhalika, Kamati ya Bunge leo hapa ilipokuja, imehakikisha na imezungumza pia bado Serikali haijafanya uwekezaji wa kutosha katika Sekta hii ya Uvuvi, hasa katika Bahari Kuu. Hili nimeliamini na limejidhihirisha pia; kwenye hotuba ya Waziri amesema pia kuwa wapo katika mchakato wa hatua ya kufufua Shirika la Uvuvi TAFICO ambalo Mheshimiwa Waziri ameliongelea zaidi kwenye ukurasa wa 119. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa sisi tumezaliwa na bahari tumeikuta, lakini leo ndio kwanza tunazungumza ufufuaji wa shirika. Kweli tumekuwa tuko tayari kwenye uwekezaji wa bahari?

Mheshimiwa Spika, ukiangalia bahari hii inaambiwa ina iwezo wa kuleta mapato shilingi bilioni 352. Sioni Serikali inakwama wapi kwa ajili ya kwenda kuwekeza, lakini kama Serikali nguvu hazitoshi kuna wadau wako tayari kuwekeza ambao tunawasema wawekezaji. Nadhani, nishauri, Wizara itoe wazo na iseme kwa bayana wawakaribishe wawekezaji kwenye bahari kuu waweze kuwekeza, ili tuweze kusaidia vijana wetu kupata ajira, lakini halikadhalika tuongeze pato la Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unapozungumza bahari huwezi kuacha kuzungumza uhifadhi wa maeneo ya mazalia ya samaki, nikimaanisha matumbawe. Haya matumbawe ambayo yapo yanazunguka ndani ya bahari yetu ndio sehemu salama na ndio muhimu kwa samaki wetu ambao wana uwezo wa kuzaliana, lakini pia samaki wanapata chakula kupitia hifadhi hizi muhimu za matumbawe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa matumbawe yetu yanapotea na yanaathirika kweli, kwa ambao wale wataalamu wa bahari wanakwenda baharini, nikiwemo mwenyewe nilishawahi kuangalia hayo matumbawe, unakuta matumbawe ambayo tayari yamefariki. Ukiwauliza wataalamu wanakwambia haya matumbawe yamefariki kwa sababu ya uchafuzi wa mazingira. Bahari inajaa joto kutokana na uchafuzi mbalimbali ambao unafanywa wa kimazingira hivyo husababisha matumbawe yale kufariki. Yanapofariki yale matumbawe na kuondoka kabisa itabidi samaki hawa waweze kuhama sehemu ile ambayo hawawezi kuzaliana wala kupata chakula na kwenda kutafuta hifadhi mbali. Sasa maana yake wanavyokwenda mbali wana uwezo wa kutoka ndani ya bahari yetu ama kutoka ndani ya Tanzania na kwenda nchi jirani. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwadhibiti samaki hawa ambao wanatoka? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, Serikali je, ilishawahi kukaa na nchi jirani na kutengeneza mikataba ya makubaliano juu ya usimamizi wa hifadhi za bahari na hasa samaki wetu wanavyotoka na kwenda kuhamia katika nchi jirani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna samaki wanaitwa Tuna, hao wana tabia kama ya nyumbu. Kuna msimu wanaondoka Tanzania, wanaondoka ndani ya bahari wanakwenda katika nchi jirani, wanakwenda kustarehe huko then wanarudi wanapenda kufanya tour. Kwa hiyo, samaki hawa wana uwezo wa kutoka na kwenda, lakini wakifika kule wakavuliwa then tunarudishiwa samaki hawa wanauzwa kwenye vikopo tunaambiwa nunueni Tuna kwenye makopo, lakini kumbe tunauziwa mali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu tunahitaji Serikali, nishauri, iwekeze zaidi ifanye mashirikiano na nchi jirani kuhakikisha wanasaini mikataba ambayo halali ya kusimamia samaki tuna na wengineo, ili kuweza kusaidia pato la nchi hii lisiweze kupotea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halikadhalika kwenye uhifadhi, naomba niishauri tena Serikali, kuna kisiwa Zanzibar kinaitwa Chumbe Island, hiki kisiwa kwa wale wanaosafiri kwa boti mara kwa mara utakutananacho utakuta mnara pale wakati unaelekea Zanzibar. Hiki kisiwa kimepata tuzo ya uhifadhi wa utalii wa kimazingira mwaka 2019 kwa East Africa kimekuwa cha kwanza. Ni kwa sababu, kisiwa hiki kina muwekezaji kwa hiyo, wamewekeza vizuri, wana wataalamu wa kutosha na wanahifadhi vizuri yale matumbawe kwa kushirikiana na Serikali ya Zanzibar. Kwa hiyo, wamefikia kupata hiyo tuzo, lakini pia sio hiyo tu, wamepata tuzo nyingine kuwa Wanautalii wa kihifadhi bora ndani ya miji ya kidunia yote wapo ndani ya namba 10. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, lisiwe tu kwa Chumbe na ukienda Chumbe kweli ni kweli hata kama hujui kuogelea wewe unaweza ukavishwa mask na ukasaidiwa na ukaona hayo matumbawe na jinsi roho yako itakavyoburudika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nishauri, matumbawe kwa jina jingine yanaitwa coral reef jamani. Niishauri Serikali kama Wizara ya Uvuvi imeona pia ni mzigo wa kuhifadhi kuna Wizara ya Utalii na Maliasili hawa ndio makonkodi wa uhifadhi. Kwa nini wasii-move hii marine park wakawapelekea Wizara ya Utalii na utalii ukaweza kuhifadhi vizuri? lakini nje na kwamba, tunatumia kupata samaki haya matumbawe, lakini vilevile ni utalii wa kimazingira ambao wageni walio wengi wanapenda kufanya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukifika pale kwenye Kisiwa cha Chumbe unafanya booking mwezi mmoja kabla ukiwa unataka kwenda kuyaona matumbawe. Kwa hiyo, unaona jinsi gani pato linaongezeka na wageni wanapenda kwa hiyo, nishauri Serikali kama wao mzigo umekuwa mzito wawape Wizara ya Utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, pia nishauri hapo waongeze juhudi ya kuwatafuta wataalamu zaidi kwa sababu, tunahitaji samaki na bado samaki hawatutoshi wanakwenda mbali kwa hiyo, imekuwa ni shida na hasa kwa hawa Ndugu zetu ambao wanafanya kazi za bahari kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kwenye mafunzo kwa wavuvi wetu, tuna wavuvi ambao wanaamka asubuhi majumbani wanakwenda baharini, na wanakwenda kwa sababu ya njaa ya maisha, lakini hawaendi kwa sababu hii kazi wanataaluma nayo. Mwingine anakwenda kwa sababu ameirithi, labda babu yake alikuwa mvuvi, leo atamchukua apige kasia, kesho wataingia baharini kwa hiyo na yeye anakwenda kwa kufikiri babu hapa alikuwa akitupa ndoana ndio wanapatikana samaki, lakini sivyo dunia imebadilika. Mabadiliko ya tabia ya nchi yapo mengi, halikadhalika bahari imekuwa na kina kikubwa cha maji, matumbawe ndio kama hivyo yanapotea kipindi hicho kulikuwa hakuna uchafuzi wa mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa wavuvi wetu wanakwenda kuvua wanarudi hakuna. Na wanarudi maisha yanaendelea kuwa magumu sana, lakini la pili pia wakipatiwa mafunzo wavuvi wetu itawasaidia watakwenda sehemu salama za kuweza kuvua, lakini la mwisho kabisa wakipatiwa mafunzo watakwenda sehemu ambazo wana uhakika leo tukienda siku ya leo tunapokwenda sehemu kadhaa basi hatuwezi kukutwa na changamoto yoyote ya kiuvuvi, lakini na watasikia moyo watasema kwamba, leo kama fulani ni mvuvi na mwingine atakwenda. (Makofi/Vigelele)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Asya.

MHE. ASYA MWADINI MOHAMED: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)