Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. William Vangimembe Lukuvi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ismani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kushukuru kupata nafasi ya pili ya leo angalau nihitimishe hii hoja. Kwanza nianze kwa kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa kusema ambao katika orodha yangu hii wapo 25 akiwepo Naibu Waziri wa Ardhi. Majina yenu nayajua kuanzia msemaji wa kwanza Mheshimiwa Silaa mpaka msemaji wa Mwisho Mheshimiwa Malembeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nawashukuru wachangiaji wengine ambao wamechangia kwa maandishi ambao wapo tisa. Maandishi yenu tunayo, tunatafakari na tumezijua hoja zenu na tutazijibu vile vile kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii baada ya maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri, namshukuru sana. Nitumie muda mfupi kwanza kutoa maelezo juu ya sheria. Wengi mmezungumzia juu ya masuala ya upangaji wa miji. Kwanza kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji Na. 8 ya Mwaka 2007 inatamka wazi kwamba Mamlaka za Upangaji wa Ardhi ni Halmashauri za Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge tujue kwamba sisi kama Wabunge na wenzetu Madiwani kwenye Halmashauri ndiyo Mamlaka halali ya kisheria ya kupanga ardhi ndani ya Wilaya yetu. Waziri wa Ardhi hatakuja kukupangia ardhi ya Tarime hata mahali pamoja. Sisi tunafanya tu udhibiti wa ile michoro, kuhakikisha kwamba mkishapanga, tukishakubaliana hambadilishibadilishi kila mara, lakini Mamlaka ya Upangaji ni Halmashauri. Kwa hiyo, wewe ndio mwenye kitambaa unapeleka kwa fundi ushonewe suti kwa mshono unaoutaka, haiwezi kuwa Wizara. Kwa hiyo, nataka hilo tuelewane kuhusu Mamlaka ya Upangaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ujenzi holela, mdhibiti ni Halmashauri. Baada ya kutunga sheria hii, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Kamati ya TAMISEMI bila shaka mnajua ipo kanuni za Udhibiti na Uendeshaji Miji Sura 244, ni kanuni za TAMISEMI. TAMISEMI ndiyo anayepaswa kudhibiti. Mamlaka za Upangaji ndizo zinazopaswa kudhibiti masuala yote ya ujenzi na uendelezaji wa miji. Kwa sababu ukishapanga, kama hili ni eneo la makaburi, mtu akijenga si wewe uliyepanga ndiyo lazima umwondoe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, suala la udhibiti na suala la upangaji ni mamlaka. Yaani Jiji, Manispaa, Miji na Halmashauri, hii ni ardhi yenu. Yaani ukipewa kipande kile cha utawala, ni ardhi yenu; na vijijini kupanga matumizi bora ya ardhi ya vijiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa namwona kule Mheshimiwa Aleksia, amezungumzia habari ya ardhi za vijiji, pengine akapendekeza lichimbwe shimo, yaani mpaka; wakulima wawe huku na wafugaji wawe huku. Bahati mbaya kuna rafiki yangu mmoja ameondoka hapa, aliwahi kujaribu pale Mvomero, tukachimba tuta wakulima wawe huku na wafugaji kule, ilishindikana. Hivi binadamu unamwekeaje mpaka, kwamba umwekee shimo hapa asiende upande huu, asiende huko, ilishindikana kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawaambia ndugu zangu, dawa ni kupanga matumizi bora ya ardhi ya vijiji. Kwa mujibu wa Sheria Na. 5 ya Mwaka 1999 ya Vijiji, ardhi na yenyewe kijiji ndiyo mali yao chini ya usimamizi wa Halmashauri. Wao katika mkutano wao wakiamua kwamba eneo hili ni la kufuga, eneo hili ni la makazi, eneo hili ni la kilimo, ile ni sheria tayari. Wakishaileta kwangu maana yake hawaruhusiwi kubadilisha mpaka waombe kibali kwangu. Kwa hiyo, wanaopanga matumizi bora ya ardhi ni vijiji husika, lakini chini ya usimamizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ningefurahi bajeti ijayo mwulize vijiji vimepanga bajeti kiasi gani ya kupanga matumizi bora ya ardhi? Kwa sababu ardhi ni mali yao. Halmashauri nazo lazima zijue ardhi ile waliyokasimiwa na wale viongozi waliochaguliwa kwa ardhi ile na viongozi wa kuteuliwa walioteuliwa kusimamia ardhi, wajue kwamba Mamlaka ya Sheria ya Mipango Miji imewapa kupanga ardhi yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, wengi wamejua hilo, wamepanga ardhi yao na imewanufaisha. Wananchi wamejenga kwenye viwanja vilivyopangwa na kupimwa na Halmashauri zimepata mapato kwa sababu wametekeleza vizuri sheria hiyo. Nilitaka nianzie hapo ili tujue.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi kama wasimamizi wa sera tumeona haiwezekani kuacha Mamlaka za Upangaji peke yake ndiyo maana tunashirikiana kupanga mipango mikubwa. Bajeti ile iliyopita tulikuwa tumetengewa fedha za World Bank nyingi, zaidi ya shilingi bilioni 60, sasa bahati mbaya mazungumzo hayajamalizika, mnajua tena mambo ya Corona watu wanafanyia majumbani, lakini lengo letu ilikuwa ni kushirikiana na Halmashauri ili kukamilisha zoezi la Upangaji na Upimaji nchi nzima; kwa vijijini kuweka mipango ya matumizi bora ya ardhi na kwa mijini kwa kutumia Sheria Na. 4 kupanga miji yetu kwa kushirikisha watalaam wetu. Hayo makampuni binafsi, tulitaka yashiriki kikamilifu kwa sababu tunajua kweli hayana hela, lakini tungeyashirikisha na kupeana maeneo ya kusimamia upangaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka huu tunashukuru, mmeona kwenye vitabu vya fedha, tuna fedha nyingine ambazo Serikali imetupatia kutoka Korea, bado tunaendelea. Hizi fedha zinapita kwetu tu, lakini washiriki wakubwa wa upangaji ni Mamlaka za Upangaji ambazo ni Halmashauri. Kwa hiyo, bado zikitokea hizi fedha tutashirikiana. Moja ya gharama kubwa ambayo inawapata Halmashauri katika upangaji ni ununuzi wa vifaa. Tunataka fedha hizi zitusaidie kidogo kununua vifaa, vipatikane vifaa vya kisasa vya kupima ili wasiwe wanakodisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya gharama kubwa ya upimaji, huwezi kupanga mezani, kuchora kwamba hapa nitaweka makaburi, nitajenga nyumba, lazima upige picha juu ya ardhi, picha ya anga ili ikupe sura hapo chini unapotaka kupanga pakoje? Hiyo ni gharama kubwa sana. Wengine wanatumia hizi za kwenye mtandao, copy, copy hizi, lakini hazitoi taswira nzuri. Kwa hiyo, tunanunua vifaa mtaona; tunanunua drone na ndege kwa ajili ya kurahisisha kazi ya wapangaji Halmashauri ili tuwasaidie kuwapa picha za anga zirahisishe ununuzi na upigaji wa picha zile ambao ni gharama sana ili kupata picha zenye sura halisi ili wapangaji waweze kupanga jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunashirikiana na Mamlaka za Upangaji ili kurahisisha kazi hizi. Ndiyo maana katika fedha za Maendeleo tulizozipata sisi Wizara tuliona siyo vizuri kufanya ziara tu, tukafikiri tuwarudishie Halmashauri wajitahidi kupanga maeneo yao. Watatafuta maeneo mazuri ya kupanga, lakini tuwape fedha shilingi 10/=, warudishe shilingi 10/=. Ndiyo maana wengine kama Jiji la Mbeya na wengine wamechukua zaidi ya bilioni, wamepima viwanja wamerudisha bilioni, wamepata zaidi ya bilioni nao wanaendelea vilevile. Wengine wamefanya bila pesa ya Serikali, lakini wameendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tumeona hili jambo ni jema. Badala ya kuzipeleka fedha kwa miradi ambayo itasimamiwa na Wizara, sisi wataalam wa Wizara tupeleke Wilayani kule kwenye ardhi ili Mamlaka za Upangaji zifanye. Nataka kuahidi, fedha zozote nitakazopewa na Mheshimiwa Mwigulu mwaka huu, zote zitakuja Wilayani, hazitabaki Wizarani. Hazitabaki kwa sababu sisi ni Wizara ndiyo, lakini hatuwezi kwenda kufanya kazi Halmashauri wakati Halmashauri ina wataalam wenye weledi na waliosoma kama sisi na wale wanasimamiwa na mamlaka ya upangaji. Mamlaka ya Upangaji, Halmashauri ndiyo wanaojua, wanaotaka kujua na wanaotakiwa kuwaambiwa hawa wanataka kupimiwa viwanja vya namna gani; na mji wao uwe namna gani? kwa hiyo tutaendelea kushirikiana ndugu zangu Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nachotaka tu niwaambie kwamba safari hii Kamati hizi mbili za TAMISEMI na Ardhi tumekubaliana tuunde timu ya pamoja ambayo itaweka masharti na mwongozo ili ijulikane nani mwenye sifa ya kupata na asipopata afanywe nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kila Halmashauri ina uwezo wa kuomba. Kwa hiyo, kama Mbunge hapa unatamani Halmashauri yako ingependa kuingia katika program hii, mwambie Mkurugenzi aombe tu. Zikifika hizi fedha, ninyi mnajua kona hii nikipanga leo viwanja vitanunulika kesho. Msianze kupanga maeneo ya makaburi, hutapata hela. Anza kwanza kupanga maeneo mazuri ili upate hela ya kurudisha, halafu baadaye ndiyo utakuja kupanga maeneo ya makaburi. Sasa wengine wameanza kupanga maeneo ya makaburi; nani atanunua makaburi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni jukumu la Halmashauri kujua fedha za mwanzo upeleke wapi ili upate mtaji, baadaye ujitegemee? Kwa hiyo, mipango hiyo mtafanya wenyewe. Kwa hiyo, waambieni Wakurugenzi waombe kwa Katibu Mkuu, vigezo vitawekwa wazi na Wizara yangu wataalam wangu, wa Katibu Mkuu wa TAMISEMI na Katibu Mkuu wangu, wataunda timu, wataweka vigezo na ikiwezekana baadaye hata Kamati ya TAMISEMI mkienda kukagua miradi, mtakagua pamoja na miradi hii inayotekelezwa katika hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawaombeni ndugu zangu tukumbushane tu huko kwenye Halmashauri, tujitahidi angalau Halmashauri kwa mwaka iweke bajeti hata ya kupanga matumizi bora ya ardhi ya vijiji viwili, vitatu, kumi; Inshallah Mwenyezi Mungu akitupa hizi fedha tulizobajeti mtakuta kama tulivyofanya katika wilaya tatu za Mkoa wa Morogoro, tulipata fedha kidogo tukaenda kufanyafanya vijiji vingi zaidi. Vinginevyo kwa kweli, kazi ya msingi hii ya kupanga matumizi bora na kusimamia kwenye Halmashauri ni kazi ya Mamlaka ya Upangaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni tulikuwa tumependekeza kwamba zamani tulikuwa na ikama ya mtu anaitwa Land Ranger kwenye mitaa huko; kama kiherehere hivi, akiona mtu amechimba msingi, basi ameshatoa ripoti, watu wamebomoa. Sasa hivi hawa watu hawapo. Dodoma walikuwa wengi sana. Tunafikiria namna ya kutumia Watendaji wa Mitaa, kwa sababu Watendaji wa Mitaa wapo pale, yule anaweza akamwona kila mtu anayevunja kanuni za Mipango Miji na akatoa taarifa. Kwa hiyo, tunafikiria namna ya kuwatumia hawa ili angalau wasimamie mambo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, urasimishaji limezungumzwa sana. Jambo hili ni jema, nimelipigia debe kwa nguvu tangu nimeingia. Haya makampuni nimeruhusu mimi yakasajiliwa na tumeyasimia. Ni kweli mwanzo walikuwa wanapanga bei vibaya, tukarudi na hivi, tumeenda mbele nyuma, lakini kidogo wengine wanafanya kazi nzuri, lakini kweli ni masikini, hawana fedha. Pia namna ya uendeshaji wake ulikuwa wa ovyo, ovyo siku za mwanzo. Ilikuwa wanakwenda kuomba kazi kwa Mwenyekiti wa Mtaa, wanapatana, kumi, ishirini, wanachukua fedha kwa masikini halafu hawafanyi kazi. Tumedhibiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaambie, mpaka sasa makampuni yaliyochukua fedha za wananchi na hawajafanya kazi inafikia shilingi bilioni 45. Mmoja amesema hapa, makampuni yanadai wananchi shilingi bilioni 70, lakini kwa sababu michoro wanayo, wananchi watalipia tu; lakini makampuni yamechukua amana hizi laki moja na nusu, laki moja na nusu, karibu shilingi bilioni 45 na hawajapima hivyo viwanja. Ndiyo hao wa Kimamba tunaopambana nao. Nataka kuwahakikishia watazirudisha hizi fedha na kazi watafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sina nia kuwafukuza, najua wamegawa gawa barua humu; wameandika barua, wametia kwenye box za watu wanaofikiri watawasaidia, bahati nzuri wengi wao wamenirushia zile barua ninazo. Ila wengine wamezitumia kusema humu, lakini wengine wamenirudishia, haiwasaidii sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, watendaji wangu walitoa taarifa fulani, nataka wajue zile kampuni za kupima wangekuja kwangu kuniambia badala ya kuandika barua. Sasa Mtendaji wangu kasema atawafuta badala ya kuja kwa Waziri ku-appeal, ninyi mnaandika barua mitaani, itawasaidia nini? Mimi ndio niliyetoa fursa hii ya makampuni kufanya urasimishaji. Mimi ndio niliyepanga hata bei na ndio niliyewasha moto mpaka wakasambaa kufanya kazi zote pamoja na Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ndugu zangu wenye makampuni binafsi, njooni tuzungumze, nitawaita tena, nitakuja kila mkoa nizungumze na makampuni yanayoshiriki na kazi ya urasimishaji kila mkoa tuzungumze kulikoni? Ni kweli hatuwezi kufanya kazi hii ya urasimishaji Serikali peke yetu, hatutaweza, lazima tushirikiane na hawa jamaa, hatuwezi. Hiyo lazima niwaambie ukweli, hatuwezi. Hata tungepata ikama ya kuweka mpima mmoja mmoja kila wilaya hatutaweza. Kazi ni tushirikiane sasa na ninyi mmeshapata ufahamu, tushirikiane katika udhibiti; win, win situation.

Mheshimiwa Naibu Spika, watendaji wangu wasiombe rushwa kwa hawa jamaa, wapitishe michoro bila bahasha, lakini na hawa wafanye kazi kwa uadilifu. Hata mabenki wajue hapa kuna fedha, wangeweza kuwakopesha hawa, wakabaki na michoro halafu watu wakawa wanalipa benki kuchukua hati zao. Hili tunaendelea nalo, najua litakwisha, tutaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka niwaambie urasimishaji utaendelea, tutashirikiana. Nitakuja Mkoa wa Dar es Salaam, nitapiga kambi pale mwezi mmoja tufanye kazi yote iishe. Tupite maeneo yote yenye kero tumalize hili jambo, tuzungumze tuone namna ya kuwasaidia hawa. Ni lazima wananchi wapate haki yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika na ndugu zangu wote, najua wengi katika hotuba zenu mmenipa mialiko. Mheshimiwa Jerry Silaa nakuja kumalizia kazi yangu kule;

Mheshimiwa Massay ingawa umeomba mambo mengi, lakini nilikuwa na mpango wa kuja Mbulu, nitakuja; Mheshimiwa Halima Mdee lile jambo la Chasimba, Chatembo na Chachui, wewe unalijua sana, ila leo umepiga chenga, hukusema mpaka mwisho. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie Waheshimiwa Wabunge, hili analolizungumza siwezi kulisema sana, ni la kimahakama. Wale watu wa Chasimba, Chatembo na Chachui ipo hukumu ya Mahakama ya Rufaa kabisa iliyowataka zile kaya 4,000 lazima waondoke. Sasa mimi kuwa Waziri wa Makazi nikaona watu 4,000 waondoke kweli nyumba zibomelewe! Ndiyo nikawa-engage wale wazungu wa kiwanda, ee bwana, kwani wewe unataka nini? Akasema bwana mimi nina madini hapa, lakini nina-surface right. Kama watu wako wataweza kunirudishia kidogo, mimi nitawaacha wakae hapo hapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukaenda kutangaza na aliyekuwa Mbunge pale, watu hawatoki. Tuelewane sasa kiasi gani nikurudishie ili anunue ile raw material mahali pengine kiwanda kiendelee. Sasa ile naona Mheshimiwa Halima hakuisema. Hawawezi. Nataka kuwaambia hivi, hawataweza kubaki pale kwa sababu kuna hukumu ya Mahakama ya Rufaa na hakuna mtu ambaye yupo juu ya Mahakama. Ni lazima tuelewane; na ndiyo maana thamani ya ardhi pale ni square meter moja ni shilingi 20,000 wakati ule; hawa kiwanda wamesema wawape shilingi 6,400/= wawapimie wawabakize pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, ingawa sehemu nyingine ya pili kuna wengine wenye mashamba, wanachaji mpaka shilingi 100,000/= per square meter. Hawa Wazungu wana hati. Siwezi kuwapa hati hawa wananchi wa Chasimba ya mtu mmoja, mmoja juu ya hati ya kiwanda. Maana yule Mzungu lazima nimlipe hii fidia ndipo arudishe ile hati. Fursa ya kubaki, watabaki, hawaondoki, wale Wazungu wameshakubali, lakini wawalipe kidogo fidia ya ardhi. Hivi nani huyo Dar es Salaam anaweza kupata kiwanja bure kulipa chochote? Nani? Sasa mvamizi ndio apate privilege ya kubaki na kiwanja bure! Ilitokea wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Halima ulisahau element ya fidia. Sasa hapa tusifungue mjadala, mara nyingi wewe tunakutana Dar es Salaam. Mimi nitakukumbusha yale makaratasi ya Kamati ile ya mwanzo ambayo tulikuwa tunazungumza tulikwama wapi na ndiyo maana mgogoro huu umenichukua miaka sita. Nitakukumbusha Dar es Salaam. Tusiwape faida, maana Mahakama wasije wakafiri Bunge huwa linatafsiri hukumu zao, maana hii ni hukumu; nawe ni mwanasheria, wakili. Kwa hiyo, tuzungumze Dar es Salaam, nitakupa ushirikiano, nitakupa makaratasi ili usome vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaahidi kwamba Mheshimiwa Mtemvu, Mheshimiwa Gambo nitafika Arusha na Arumeru zote mbili, nitakuja. Pia Mheshimiwa Mbunge wa Mtama, timu ile uliyoomba ya kuja kuangalia ule mpaka itakuja ili tuone namna gani, halafu baadaye tutashirikiana na Waziri wa TAMISEMI namna ya kumshauri Mheshimiwa Rais ikibidi, tukiona kama kuna sababu juu ya mipaka hiyo. Lakini kule…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, kengele ya pili imegonga.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuwaahidi tu Wabunge wote mliozungumza hapa, mliohitaji migogoro yenu kutatuliwa kwenye site, mimi mmenipa mwaliko, nitafika; na ratiba hii naanza wiki ijayo. Kote huko nitakuja. Nitaenda Mtama, nitaenda Mbogwe, nitaenda Hanang, Arumeru zote, Nyamagana narudi tena na Kaliua nitakwenda. Kaliua kulikuwa na ratiba ambayo tulishaombwa na Mheshimiwa Mama Sitta na Waziri wa Utalii, tutakuja huko. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, omba fedha, kwa sababu hata mimi nitataja hapo kwamba uje na Mbeya. Orodha ni ndefu, wewe omba hela tukupe halafu uje tuonane huko.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuruni sana kwa kunisikiliza. Naomba mnipe pesa na yote haya mliyoyasema watu wote yatatimizwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.