Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. JUMANNE A. SAGINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa hatua mbalimbali zilizochukuliwa ili kuboresha maendeleo na usimamizi wa ardhi hapa nchini likiwemo suala la usimamizi wa wataalam wa sekta ya ardhi. Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Waziri, Naibu Waziri na wataalam wakiongozwa na Katibu Mkuu, naomba kushauri kuhusu maeneo yanayohitajika kufanyiwa kazi zaidi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, mamlaka ya upangaji ni Mamlaka za Serikali za Mitaa lakini ushirikiano wao na wataalam wa Wizara kwenye baadhi ya maeneo si wa kuridhisha. Bahati mbaya wataalam wa ardhi kwa baadhi ya maeneo hawana ushirikiano miongoni mwao. Surveyors wanafanya kazi bila kushirikiana na wataalam wengine. Hali hii inadhoofisha uendelezaji bora wa ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ili kuondoa kuendelea kuwepo kwa makazi holela yasiyopangwa, nashauri kuwepo maamuzi ya kisera na kuandaliwe miongozo ya upangaji wa vijiji na miji midogo ambayo haijapangwa. Viongozi wa ngazi za kata na vijiji wapewe mafunzo ya namna wanavyoweza kupanga vijiji vyao na kusimamia mipango hiyo. Ikiwa wakati wa operation vijiji, vijiji vingi vilipangwa vizuri, hatuna sababu kuwa na vijiji visivyopangwa leo wakati wasomi wameongezeka, na vitendea kazi vimeongezeka. Vijiji hivi vinapozidi kukua vinasababisha kuwa na miji isiyopangiliwa yenye makazi holela, miji isiyokuwa na maeneo ya masoko, vituo vya mabasi, viwanja vya michezo, shule, vituo vya afya na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi inaongozwa na mtaalam kijana msomi, Profesa Magigi, lakini tume hii haijawezeshwa vya kutosha kifedha ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Tume hii inapaswa kuzisaidia mamlaka zote za upangaji ambazo ni Halmashauri 184. Lakini kwa bajeti iliyopo na kwa kutegemea uhisani wa World Bank itakuwa vigumu kuzifikia Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ufanisi. Ushauri wangu hapa ni kwamba Tume hii itengewe fedha za ndani za kutosha ili ifanye kazi muda wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru na ninaunga mkono hoja.