Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru sana nami kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni hii kwenye Wizara hii muhimu kabisa kwa maisha ya Watanzania wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kumshukuru Mungu lakini kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu, pamoja na
watendaji wote wa Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Kiukweli Wizara hii pamoja na changamoto nyingi sana tulizonazo kwenye sekta ya ardhi, sina shaka wenzangu watakubaliana nami kazi kubwa sana imefanyika kwenye sekta zote; kupima, kupanga pamoja na kutatua migogoro mingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuishukuru sana Wizara, nawe kama Mbunge wa Mbeya utakubaliana nami kwamba moja ya majiji yenye changamoto kubwa za makazi kwa wananchi na maeneo yake, Jiji la Mwanza ni kama ilivyo kwa Jiji la Mbeya. Namshukuru sana Mheshimiwa Lukuvi, Bunge la Kumi na Moja baada ya maombi ya muda mrefu alihamua kwa dhati kukubali Leseni za Makazi baada ya Dar es Dalaam ziende Mwanza, Arusha pamoja na kwako Mbeya. Sina shaka zoezi hili litafanyika na limeshaanza na inawezekana likawasaidia sana wananchi wa Mbeya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kule Mwanza unafahamu maeneo ya Mabatini, Pamba, Isamilo, Igogo na baadhi ya maeneo ya Mkuyuni, wananchi wote waliozunguka kwenye vilima, walikuwa hawana sifa hata ya kulipa kodi ya ardhi kwa sababu maeneo yao hayatambuliki. Leo naamini Serikali kwa mpango iliyonao wa kurasimisha makazi haya na kupata Leseni za Makazi zaidi ya kaya 15,000 tutakuwa tumeisadia Serikali na Wizara kupata mapato. Hii ndiyo moja kati ya kazi kubwa zilizofanywa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa taarifa tu, nitumie nafasi hii kuwapongeza sana watendaji wa Jiji la Mwanza wa Kitengo cha Ardhi, pamoja na changamoto, wanafanya kazi kubwa. Leo tuko zaidi ya nusu ya kazi ambayo Mheshimiwa Waziri umewaelekeza na wamekusudia kuifanya. Tayari tumeshatambua vipande vya viwanja hivi zaidi ya 9,437. Hii siyo kazi ndogo kati ya viwanja 15,000. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri na niendelee kumwomba asituchoke, aendelee kutusaidia kwa sababu ndilo jukumu aliloaminiwa nalo; na bado Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Mama Samia ameendelea kumwamini. Sina shaka anafanya vizuri kwa sababu ana timu nzuri ya watendaji ambayo imesheheni pamoja na Naibu Waziri ambaye ni msaidizi wake, kwa karibu wanafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, napenda kuzungumzia suala la urasilimishaji wa makazi. Ni mfano ule ule tu, tumekuwa na changamoto kubwa zinazotokana na migogoro. Hii inawezekana ni kwa sababu maeneo mengi yalipimwa na kupangwa zamani. Kwa namna moja au nyingine kutokana na kukosa fedha na changamoto mbalimbali, maeneo haya hayakuendelezwa kwa wakati na badala yake wananchi walio wengi wakaingia kwenye maeneo haya. Sasa Serikali inapoteza kodi katika maeneo yote mawili; mtu aliyemilikishwa mwanzo hajaonekana zaidi ya miaka 30, wananchi wamejenga kwenye lile eneo, wameanza maisha yao, wamejenga majumba na maisha yanaendelea. Siyo rahisi sana kuvunja zaidi ya nyumba 200, 300 au 500 kwa sababu tu eneo hili alipewa mtu mmoja hati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri amekuja Mwanza na Naibu Waziri amekuja kwa wakati tofauti, wamefanya kazi kubwa sana. Mifano iko mingi, ukienda kule Mandu Mtaa wa Sokoni, tumefanya maamuzi ambayo leo yametuweka kwenye hali nzuri ya wananchi waliokuwa wamepoteza matumaini na sasa wana imani kubwa na Serikali yao, chini ya Mheshimiwa Mama Samia wanaamini kwamba wataendelea kuijenga Serikali hii.

Mheshimiwa Naibu Spika na Mheshimiwa Waziri, bado tunayo changamoto kwenye baadhi ya maeneo. Tulikabidhi baadhi karibia maeneo saba, umeshatutatulia maeneo mawili, lakini bado yapo maeneo ya Kata za Isamilo, kuna kiwanja Na. 359 Block D ambayo ni ya Mtaa wa Isamilo Kaskazini A, Kaskazini B pamoja na Neshen.

Mheshimiwa NaibuSpika, pia kipo kiwanja Na. 590 cha Block C kule Nyegezi kati ya Mtaa wa Ibanda, Swila, Igubinya pamoja na Punzenza. Ninaamini maeneo haya yote Mheshimiwa Waziri akitumia utaratibu ule na ikiwezekana hata kwenye ile asilimia moja kama alivyofanya akaongeza asilimia ikawa mbili itasaidia lile deni liendelee kujifidia kule na wananchi wapate uhalali wa kuishi kwenye lile eneo kama walivyojenga na hatimaye waweze kulipa kodi ili tuweze kuondokana na kelele ambazo hazina shida sana.

Mheshimiwa Naibu Spika na Mheshimiwa Waziri, ninaamini kazi hii ambayo umeianza kwa muda mrefu na sasa tukiwa kwenye Awamu ya Sita, sina shaka tutakapofika 2025 kwa timu uliyonayo, wananchi wetu kwenye majiji haya; tunafahamu, ni kweli kwamba zoezi la upimaji na upangaji mara nyingi sana linaangalia maeneo ambayo bado hayajachangamka sana, lakini ukweli ni kwamba, maeneo yaliyochangamka sana kama Jiji la Mwanza la Mbeya na maeneo mengine, yanahitaji sana zoezi hili ili yaweze kuwa bora zaidi na Serikali na Wizara yako pia iweze kuingiza fedha za kutosha kupitia kodi ya ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la mwisho kwa leo, napenda niizungumizie hii premium ambayo inalipwa kwenye masuala mazima ya upatikanaji wa ardhi. Ninafahamu miaka michache iliyopita tulikuwa na utaratibu mzuri sana, ilikuwa fedha hii inatumika kama revolving fund. Pale Halmashauri zinapotumia, zinapopima, kumilikisha na kupanga, zile gharama zote zinazopatikana, Wizara ilikuwa na utaratibu wa kurejesha asilimia 30.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu baadaye mambo yakabadilika fedha hizi zikawa hazirudi, lakini sasa hii Mheshimiwa Waziri naomba niilete kwako kama ombi, Halmashauri hizi ambazo tunazitegemea zilipe fidia kwenye maeneo ya masoko, shule, hospitali, kwenye maeneo mbalimbali ya viwanja na kadhalika, zinakuwa na mzigo mkubwa. Unaweza kukuta Halmashauri kama ya ndugu yangu Mheshimiwa Deo hapa labda inaingiza shilingi bilioni mbili au tatu, atawezaje kulipa fidia? Atawezaje kulipa mapato mbalimbali ili aweze kukamilisha mahitaji haya? Kwa hiyo, mliangalie hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, uzuri Mheshimiwa Waziri anao mpango, aidha aendelee kuturudishia hii asilimia 30 au aendelee kutukopesha ile mikopo ambayo ametukopesha kwa muda mrefu na mifano mizuri ya matumizi bora ya hii fedha yapo. Ukiangalia leo Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, jirani pale kwa Mheshimiwa Mama Angelina Mabula, Mbunge na Naibu Waziri, aliwakopesha karibia shilingi 1,500,000,000/=, wamefanya vizuri hakuna mfano na ninawapongeza sana. Kwa sababu wameweza kurejesha fedha, yote na kupitia fedha hiyo wamepima na wamepata faida. Wamepima kwenya kata nyingi; kwa mfano, wamepima Kata ya Kirumba, Kata ya Shibura, Kata ya Buswelu, Sangabuye na hata Nyamongoro. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Waziri, fedha hizi hebu tuletee. Hata Mwanza Jiji tunazihitaji.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, mwongozo wa Spika.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mwongozo wa Spika.

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Mbeya watakuwa wanazihitaji.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mwongozo wa Spika.

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, tukipata fedha hizi za kutosha, sina shaka tutazitumia vizuri na tutarejesha kama walivyofanya Ilemela. Huu naomba uwe mfano wa kuigwa kwa sababu faida iliyopatikana na kazi iliyofanyika, leo hata wakiomba tena Mheshimiwa Waziri, wape zaidi ya shilingi bilioni 1.5 uliyowapa kwa sababu wameonyesha mfano. Nasi Jiji la Mwanza tumeomba kama shilingi bilioni tatu tu, tupe hizi fedha ili tufanya kazi hiyo na tuweze kupima na kupanga vizuri mji wako ili wananchi wako ikifika 2025 kura zote ziende kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sina shaka na Mheshimiwa Waziri, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, Mungu aendelee kuwabariki Wizara hii kazi nzuri.