Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Deodatus Philip Mwanyika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hoja iliyopo Mezani. Nianze kwanza kwa kuunga mkono hoja, lakini niseme sekta hii ya kilimo ndiyo inabeba maisha ya Watanzania walio wengi. Kwa hiyo, ningetegemea labda wangekuwa na bajeti kubwa ya kutosha, lakini matarajio hayo na bajeti iliyopangwa ni sidhani kama itakidhi matarajio ya wengi.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, nianze kwa kusema bado nampongeza Waziri na Naibu Waziri na Watendaji kwa juhudi zao mpaka muda huu. Kwenye bajeti hii nilichokiona pamoja na kwamba hakuna pesa za kutosha, lakini wamejaribu kuweka maeneo ya mikakati ambayo yanakwenda kushughulikia baadhi ya matatizo.

Mheshimiwa Spika, napenda kusema, itategemeana sana kama hata hiyo pesa ndogo iliyotengwa kama itapatikana. Kama isipopatikana tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu na sidhani kama kuna mafanikio yoyote ambayo yatapatikana kulinganisha na matarajio.

Mheshimiwa Spika, napenda niongelee mazao mawili ambayo ndiyo yapo katika Jimbo letu la Njombe Mjini, lakini yapo katika Ukanda mzima wa Nyanda za Juu Kusini. Tukianza na chai, wachache wameliongelea humu ndani, lakini ni zao ambalo tuna uhakika na tunaelewa kwamba kwa sasa hivi ni zao ambalo katika soko la dunia bei imetikisika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, nchi yetu uzalishaji wa chai umeshuka chini kwa maana ya majani mabichi ya chai, lakini napenda kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Waziri, walikuja Njombe tarehe 10 mwezi wa Tatu, wakakaa na wadau wa chai, tukawaeleza matatizo yote ya chai, kwa hiyo, tukayajenga tukaweka mikakati.

Mheshimiwa Spika, jambo kubwa ambalo wanalielewa ni kuhusiana na umwagiliaji. Tunahitaji tija kwenye zao la chai, tunahitaji kuwa na bajeti ya kutosha ya umwagiliaji. Nimeona katika bajeti ya leo kwamba umwagiliaji umepewa pesa kidogo. Nina matumaini makubwa kwa sababu Mheshimiwa Waziri alikuja Njombe, akayasikia mwenyewe. Katika pesa hizo atahakikisha kwamba wakulima wa chai wa eneo hilo wanaangaliwa.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ni la muhimu…

T A A R I F A

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa.

MHE. JUSTINE L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nataka nimtaarifu msemaji kwamba, wakati wanahangaika na umwagiliaji pale Kilolo kuna eka zaidi ya 300 za chai. kwa miaka 30 ile michai sasa inachomwa mkaa; na hata hiyo ambayo mvua inanyesha yenyewe, bado haijafanywa kitu chochote na hakuna kiwanda na majani hayachumwi.

Mheshimiwa Spika, nampa taarifa hiyo ili aweze kujenga hoja vizuri. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Deo.

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa yake, nami nilikuwa naenda huko. Najua wanakwenda kuongeza uzalishaji wa chai, lakini nilisema kwamba waanze na maeneo ambayo tayari chai ilishalimwa na imeachwa porini na mojawapo ni hilo la Kilolo. Ndiyo maana naongelea Nyanda za Juu Kusini na chai.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine kubwa ni miundombinu wezeshi katika zao la chai. Ni ukweli usiopingika kwamba kama hatuta-address tatizo la miundombinu wezeshi kwenye zao la chai hatutapata mafanikio wala hatutapata yale malengo yetu ya kuongeza uzalishaji wa chai kutoka tani 37,000 kwenda kule ambako wanataka, hatutafanikiwa.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni ambalo limeongelewa sana hapa, la ugani, ni jambo la muhimu sana. Naelewa kwenye chai kwenye eneo la Njombe kuna Kampuni ya NOSC ambayo imeleta ushirikiano mkubwa na imesaidia, lakini kuna maeneo mengi bado tunahitaji Maafisa Ugani.

Mheshimiwa Spika, naelewa umeliongelea hapa ukielezea kwamba Serikali haiwezi kuajiri. Ni kweli haiwezi kuajiri Maafisa Ugani wa kutosha, lakini kuna wakulima wadogo wadogo wa chai ambao wanahitaji msaada mkubwa wa Maafisa Ugani. Kwa hiyo niombe waendelee kuliangalia na nimeona kwamba bajeti yao imeongezwa.

Mheshimiwa Spika, soko ni tatizo kubwa sana, Njombe na zao la chai soko letu sisi ni viwanda, kiwanda kikifanya kazi maana yake tuna soko. Kinachojitokeza, Njombe tuna viwanda vinne vya chai, tuna uhakika wa hilo soko, lakini kwa bahati mbaya, katika waendeshaji wa viwanda vya chai katika Mkoa wa Njombe na maeneo yote ya Njombe ni mwekezaji mmoja tu ya Unilever ambaye yeye anaendesha kwa ufanisi na anaweza kulipa wakulima. Waendeshaji wengine wa viwanda vya chai ni jambo la kusikitisha sana kwamba wameshindwa kabisa kuwalipa wakulima wa chai. Naelewa jambo hili Waziri Mkuu aliliingilia, Mkuu wa Mkoa ameliingilia, Waziri amelisikia, lakini bado tatizo bado linaendelea. Tunaomba sana Serikali ioneshe kwamba ni Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kiwanda kilichobaki kimoja ambacho kinafanya kazi kina tatizo bado la kupata majani ya chai ya kutosha. Kuna uwezekano kama tatizo hili halitakuwa-addressed, kwa sababu mfumo wa kile kiwanda ilikuwa ni kupata majani ya chai kutoka kwa wakulima wadogo wadogo, majani ya chai hayatoshi. Ni kweli kwamba maeneo mengine yanayozalisha majani ya chai yanaweza yaka-supply kiwanda kile, lakini kwa sababu ya mikataba ambayo imeingiwa, wakulima wale wanatakiwa wapeleke chai kwenye kiwanda au viwanda vya yule mtu ambaye hawezi kulipa ambaye ni Mkenya wa Kampuni inaitwa DL Group.

Mheshimiwa Spika, hili ni jambo ambalo Wananjombe hatulikubali kwa sababu kama wananchi wanaweza wakapeleka majani kwenye Kiwanda cha Unilever ambacho kinalipa kwa nini wazuiwe. Kwa hiyo, naiomba Bodi ya Chai ifanye kazi yake, lakini namwomba vile vile Mheshimiwa Waziri naye aingilie…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Deodatus Mwanyika.

DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)