Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante sana nami nashukuru kwa kunipa fursa niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. Niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara hii kwa kuandaa hotuba hii. Najua muda ni mchache sana lakini nitajitahidi.

Mheshimiwa Spika, niungane na wenzangu kuipongeza sana Serikali, kwa kuifanya sekta ya kilimo iweze kutoa mchango mkubwa sana katika ukuaji wa kilimo, wa uchumi, lakini sambamba na hilo katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri amesema kwamba, kilimo kimechangia asilimia 65 ya malighafi za viwanda niipongeze sana Wizara kwa kufikia hatua hii.

Mheshimiwa Spika, sambamba na pongezi hizo naomba nitoe ushauri kwamba, iwapo bajeti itakuwa ya kutosha ina maana kwamba, uwezekano wa uchumi wetu kukua kutokana na kilimo unaweza ukafika zaidi ya asilimia 90. Lakini sambamba na hilo, hata katika upatikanaji wa malighafi ikipatikana pesa ya kutosha kwamba, kilimo kikawa kina tija ina maana kwamba, uchangiaji katika zile malighafi unaweza ukafika asilimia 100 na hatimaye mwisho wa siku, tunaweza tukapata ziada zaidi na tukaweza kuuza nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kubwa ninachoweza kuishauri Serikali hapa ni kwamba, kuona jinsi gani tunaweza kupata bajeti ya kutosha ili kusudi kuweza kuwekeza katika kilimo. Naomba pia, nizungumzie kuhusu kilimo cha umwagiliaji, wenzangu wengi sana wamezungumzia kuhusu kilimo cha umwagiliaji. Niipongeze sana Serikali kwa kuweza kuwa na hekta 694,715 kwa mwezi Mei, 2020 hadi hekta 695,045 mwezi Machi, 2021 hii iko katika ukurasa wa 10 wa hotuba hii. Kumbe ni kwamba tukiwekeza zaidi katika kilimo tija itakayopatikana ni kubwa sana na sasa kubwa ni kwamba, Wizara ione umuhimu wa kuhamasisha wananchi waweze kujikita zaidi kwenye kilimo cha umwagiliaji kulikoni kilimo cha mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hilo kwamba, wadau wengi zaidi waweze kuingia katika kilimo cha umwagiliaji. Naamini kabisa mapinduzi ya kilimo yanaweza yakawezekana na hatimaye, sisi tukawa ni miongoni mwa nchi ambayo inaweza ikalisha hata nchi mbalimbali katika dunia hii. Lakini pia mazao ya biashara yanaweza yakapatikana.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine nilitaka kuzungumzia ilikuwa ni kuhusu bima ya kilimo, niipongeze sana Serikali kwa kuona umuhimu wa bima ya kilimo. Ninajua kabisa kwamba bima hii kutokana na taarifa ambayo nimeiona katika hotuba hii, inaweza ikasaidia wananchi wengi sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ushauri wangu mkubwa ni kwamba, Serikali sasa iharakishe kukamilisha ule Mpango wa Taifa wa bima, kwa ajili ya kilimo ili kusudi kuwanusuru wananchi wengi zaidi. Na wakulima wengi Zaidi, waweze kuelimishwa kuhusu hii bima ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo natamani kulizungumzia ni zao la zabibu. Kwanza niipongeze sana Serikali kwamba katika hotuba hii, ukiangalia ukurasa wa 27, ukurasa wa 107, ukurasa wa 131 na ukurasa wa 158, kuna element ya zabibu imezungumziwa pale. Kwa hiyo, hapa sasa tunaona mwanga kwamba sasa Serikali inaona kwamba, kuna umuhimu wa kuwekeza katika hili zao la zabibu, lakini sambamba na hilo nilikuwa naomba niishauri Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna mashamba katika maeneo mbalimbali mfano katika Wilaya ya Chamwino kuna shamba, kuna maeneo ya Gawaye kuna shamba, kuna eneo la Hombolo kuna shamba na kuna baadhi ya maeneo ya Bahi na kadhalika. Ushauri wangu, Serikali ingeona umuhimu wa kuweza kufanya block farming katika zabibu na ikiwezekana zabibu nayo iwe ni zao la kimkakati katika Mkoa wa Dodoma. Kwa sababu, unapozungumzia zabibu, zabibu katika Dodoma ni siasa, zabibu katika Dodoma ni uchumi. Kwa hiyo, ushauri wangu ulikuwa ni huo, Serikali ijaribu kuwekeza zaidi na zaidi katika zao la kilimo kwa sababu, sisi wana Dodoma tunaona kabisa kwamba, zabibu ni fahari ya Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na ninasema hivyo kwasababu kwamba zabibu ya Dodoma yenyewe ni unique sana. Kwasababu imekuwa ikizaliwa kwa vipindi viwili, yaani kwa awamu mbili unaweza ukapata zabibu na hii ni very unique. Kwa hiyo, ninachosisitiza ni kwamba, Serikali ione umuhimu wa kulifanya kwamba zao la zabibu liwe ni zao la kimkakati katika Mkoa wa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia niwapongeze sana Wizara kwamba, katika ukurasa wa 89 wa hotuba ya Waziri, amezungumzia hatua ambayo Wizara imekuwa ikichukua, kutoa huduma ya lishe kwa wale wafanyakazi ambao wameonekana na VVU hongera sana kwa Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashauri Wizara zingine, Idara za Serikali na Taasisi za Serikali, zione umuhimu pia wa kuona kwamba, wale wafanyakazi wote ambao wamejidhihirisha na wale ambao hawakujidhihirisha, tunawashauri kwamba wadhihirike, ili kusudi waweze kupata huduma ya lishe kwa ajili ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia nizungumzie kuhusu mazao ya bustani, mazao ya bustani bado bei ya zile mbegu ni kubwa na mbegu zinatoka nje. Kwa hiyo, nilikuwa naomba kushauri kwamba ikiwezekana basi, hebu hizi taasisi zetu za ndani nazo ziweze kuzalisha mazao bustani, kama vile mbegu za nyanya, mbegu za matikiti na nyinginezo ili kusudi sasa, zikiuzwa hapa ndani kwa bei ya ndani itakuwa ni bei nafuu Zaidi, kulikoni ambayo ile inayotoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, ahsante sana kwa kunipa fursa. (Makofi)