Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Amb. Dr. Pindi Hazara Chana

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. DKT. PINDI H. CHANA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza naunga mkono hoja. Nampongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanafanya sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, moja kwa moja nakwenda kwenye kilimo cha kisasa. Kilimo cha kisasa hatuwezi tukafanya kwa kutumia jembe la mkono. Sisi wengine tumesomeshwa kwa jembe la mkono na sasa siyo sawa kusomesha watoto wetu kwa jembe la mkono, tunahitaji vitendea kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miaka 50 baada ya Uhuru Tanzania lazima tuulizane viwanda vya matrekta viko wapi? Wizara itusaidie, Serikali itusaidie tupate viwanda vya matrekta vya kutosha. Leo hii nina invoice hapa, nilikuwa na-compare trekta moja bila jembe siyo chini ya shilingi milioni 50; trekta aina ya Ford, Valmet na hizi zote zinatoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, ni kweli tumetoa ushuru, lakini haiwezekani mkulima wa Makete, Njombe akanunua trekta kwa shilingi milioni 50 bila jembe na kadhalika. Tunahitaji viwanda vya power tiller vya kutosha. Pia Halmashauri zetu zisaidie kuona katika kila Halmashauri kuwepo na wawekezaji wa masuala haya ya kilimo cha kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana, wakati umefika; kama tulivyosema kwenye Ilani kwamba tunataka kwenda kwenye kilimo chenye tija, kilimo cha kisasa cha kuongeza kipato kwa mkulima, lakini leo hii kwa mkulima imekuwa ndiyo changamoto. Yaani mtu ukimwuliza profession, katika kazi mbalimbali; wewe una taaluma gani? Ukisema mkulima, mtu anageuka pembeni. You see!

Mheshimiwa Spika, kwa kweli lazima kilimo kiwe cha kuvutia, chenye tija. Watoto wanapokwenda kusoma University anaulizwa unataka combination gani? Yaani mtu akichagua agriculture wanamwangalia mara mbili; why not business, why not finance? Agriculture, are you serious? Kwa hiyo, lazima tubadilike kwa kweli kilimo hiki kiwe ni chenye tija. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Wizara ifuatilie takwimu kwa kila Halmashauri kuna matrekta mangapi? Mtashangaa kuna baadhi ya Halmashauri matrekta ya kuongeza tija kwenye kilimo cha kisasa hazipo; ziwe ni mbovu au mpya, hazipo. Hapa tunahitaji Government intervention. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo nimetumwa na wananchi wa Mkoa wa Njombe ni lumbesa katika mahindi na viazi. Unakuta magunia mawili yanashonwa linatafsiriwa ni gunia moja. Eneo hili pia imekuwa ni changamoto ya kutosha.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo limezungumzwa hapa ni suala zima la masoko. Kwa kweli masoko ni changamoto. Naipongeza Wizara, imeshirikisha sana balozi zetu mbalimbali, kwa hiyo, katika balozi zetu tuwape takwimu za kutosha. Hizi balozi zetu, hususan zinazozunguka mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nchi zinazotuzunguka wanahitaji sana bidhaa za mazao; maharage, mbao, viazi, chai, alizeti na kadhalika. Mara nyingi wanauliza, mna tani ngapi ambazo tunaweza tuka-import kutoka Tanzania. Yaani Tanzania inakuwa ina- export.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, takwimu lazima ziwepo na ziwe zinapatikana mara moja. Unakuta hizi takwimu mpaka taarifa itoke ubalozini iende Foreign, ikitoka Foreign iende Kilimo, tena itoke Kilimo irudi Foreign ifike kule; huyu mwekezaji hawezi kusubiri, ataenda Brazil kuchukua mahindi. Kwa hiyo, taarifa hizi za kutafuta masoko ziwepo na tushirikishe taasisi binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna taasisi kama East Africa Grain Council, wao wanachukua takwimu kwamba nafaka ziko wapi; mahindi, maharage, njegere na nani anahitaji? Wanachofanya ni kuwaunganisha kwenye mtandao, you see! Kwa hiyo, lazima sasa tushirikishe sekta binafsi katika suala zima la utafutaji wa masoko na uwekezaji katika kilimo.

Mheshimiwa Spika, tuwe na masoko ya mipakani. Wakati mwingine wakulima wetu wakipeleka mazao nje ya nchi, wanasumbuliwa sana na madalali, hawapati haki zao kwa wakati. Kwa hiyo, tukiwa na masoko haya katika mipaka ya nchi zetu mbalimbali, wanaweza wakapata mazao haya kiurahisi zaidi. Kwa hiyo, nchi mbalimbali ambazo ni nchi jirani haziwezi kuhangaika kusafiri kwenda mpaka mikoa ya kusini; pale pale mpakani anapata anachohitaji.

Mheshimiwa Spika, parachichi ni zao muhimu sana. Mkoa wa Njombe wamenituma, iko changamoto ya madawa ya parachichi, iko changamoto ya cold rooms za kuhifadhia parachichi. Pia hii parachichi inatakiwa iwe certified. Ili mkulima auze nje lazima u-certify zao la parachichi.

Mheshimiwa Spika, zile taasisi zinazo-certify zinatoka nje ya nchi…

T A A R I F A

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa, Mheshimiwa nimekuona.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, mzungumzaji anayezungumza, mimi Mbunge mwenzake wa Njombe, pia tumetumwa kwenye suala la pamba, kwa sababu miche ya michikichi inatolewa bure, mbegu za pamba zinatolewa bure na mbegu za mazao mengine tofautitofauti Serikali imekuwa ikitoa bure. Je, ni lini Serikali itaanza kutoa mbegu za parachichi bure?

Mheshimiwa Spika, hii ni taarifa ambayo wamenipa wananchi wa Njombe nije niulize Bungeni. Ahsante. (Kicheko)

SPIKA: Chief Whip, inabidi uandae semina, maana mambo haya ya Wabunge wako. (Kicheko)

Mheshimiwa mchangiaji, endelea.

MHE. DKT. PINDI H. CHANA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naendelea. Hiyo taarifa naikubali kwamba mbegu ya parachichi ni lazima itolewe bure. Kwa hiyo, eneo hili ni muhimu liangaliwe kinagaubaga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Makete kwa kweli tunalima viazi, lakini jembe la mkono linamtoa mkulima. Leo hii ukiangalia mikono yetu sisi wakulima wa Njombe tunatumia jembe la mkono. Wananchi wa Makete, akina mama wa Njombe wamenituma, wanasema haiwezekani tukapata vitendeakazi vya kulima viazi hizi kwa mashine? Miaka 50 baada ya Uhuru, kweli jembe la mkono! Kwa hiyo, tupate vitendeakazi. Kuwe na mashine maalum ya kuweka matuta tuachane na jembe la mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, akina mama, wananchi wa Lupembe kwa kweli wanafanya kazi kubwa sana ya kuzalisha chai, lakini msimu wa kiangazi kutokana na upungufu wa maji, unakuta mazao yanapatikana machache. Kwa hiyo, tunahitaji umwagiliaji katika chai na wakulima walipwe kwa wakati. Kuna wakati viwanda vya chai vinachelewa kuwalipa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kilimo kinakwenda sambamba na miundombinu, barabara. Naungana na Taarifa ya Kamati ya Kilimo, imesema TARURA waongezewe fedha. Sisi pale Njombe pia tuna uwanja wa ndege, kuna wawekezaji wanatoka nchi za jirani wanakwenda Njombe, wanahitaji kusafiri kwa haraka…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. DKT. PINDI H. CHANA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.