Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi niungane na wenzangu nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niwe mmoja wapo wa kuchangia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze sana kwa kumpongeza Jemedari Mkuu Samia kwa kazi nzuri ambayo anaifanya ndani ya nchi yetu. Lakini nimpongeze sana Waziri Kwandikwa kwa kazi nzuri ambayo anaifanya katika Wizara hii ya Ulinzi. Jeshi la Wananchi ni mali ya wananchi na wananchi ni mali yao sasa Kwandikwa namna anavyojichanganya anaendana na jeshi la wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Kwandikwa tunakupongesa sana kwa namna unavyojichanganya na sisi Wabunge wenzako, umekuwa karibu na sisi hongera sana kwa kazi ambayo unaliongoza jeshi hili. (Makofi)

Lakini pili nimpongeze sana CDF Mabeyo, pamoja Makamishna wake wote, kwa kazi nzuri wanayetulinda mipaka yetu na kadhalika, tuko salama tuko kwa sababu wao wapo, wanaliongoza jeshi vizuri kupitia wewe tunakushukuru sana Mabeyo na wenzako kwa kazi nzuri ambayo unaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile niungane na wenzangu kwamba Mabeyo na timu yake na wewe Waziri baada ya kifo cha Jemedari wetu….

NAIBU SPIKA: Jenerali Mabeyo.

MHE. DEO K. SANGA: …kwa kazi nzuri aliyoiongoza kuituliza nchi, juu ya kifo cha kilichotokea cha Dkt. Magufuli amefanya kazi kubwa sana na nitampongeza sana kwa kusimamia mazishi yale chini ya Waziri Mkuu ambaye naye pamoja akisaidiana na Mheshimiwa Jenista, dada yetu kwa kazi nzuri ya kuongoza mazishi yale Jenista tunakupongeza sana kwa kazi nzuri ile ambayo umeifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizo, mimi nina mambo machache, nimesikiliza sana michango ya Wabunge, kuna migogoro baina ya mipaka ya wananchi na jeshi. Ombi langu Mheshimiwa Waziri na timu yako mkae na Waziri Lukuvi na timu yake ili muone muorodheshe maeneo yenye migogoro kati ya wananchi, na jeshi hili yatatuliwe. Litakuwa ni jambo jema sana nitoe mfano mdogo tu pale kwangu Makambako, Mkuu wa Kikosi cha Jeshi la Makambako anafanya kazi nzuri haijapata kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yuko jirani na wananchi, anashiriki maendeleo na wananchi, anashiriki kuchangia maendeleo ya shule yetu iko jirani pale ya Kipagamo na maendeleo mengine anafanya, kwa kweli tunampongeza sana Mkuu wa Kikosi chetu cha jeshi pale. (Makofi)

Ombi langu kuna eneo dogo ambalo wananchi walipanda vitindi vya ulanzi. Vitindi ndugu zangu kule kwetu ulanzi ule unagemwa, unaota kutoka chini unagemwa wananchi wanauza, wanapata riziki. Kwa hiyo, sasa wananchi wamekosa kwa sababu jeshi eneo lile wanasema ni mali yao. Ombi langu Mheshimiwa waziri na timu yako tafuta muda, njoo uone eneo linalozungumzwa hili paweze kutatuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nilikuwa na ombi lingine Mheshimiwa Waziri wamezungumzia wenzangu Waheshimiwa Wabunge hapa kwamba Jeshi kwa sababu wanafanya kazi nzuri, wajengewe nyumba nzuri za kuishi. Sasa na mimi nazungumzia juu ya jeshi lililopa Makambako, tuna nyumba ambazo mlizijenga miaka mingi sana za kuishi wanajeshi pale, nyumba hizi hazijamaliziwa zaidi ya miaka 15; nikuombe Waziri fedha ya Serikali iko pale, kuna nyumba zaidi ya tisa, ombi langu nyumba hizi zimalizwe ili wanajeshi waweze kukuaa kwenye nyumba zile. kwa sababu zimekaa hazimaliziwi kwa hiyo niombe sana jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ni kuhusu vijana wanaojiunga kwenda JKT nilikuwa nadhani Serikali itafute namna ambavyo vijana hawa wanapokwenda kujiunga kule, kazi ya JKT ninavyojua mimi ni kwenda kujenga uzalendo wa nchi yao. Sasa tutafute namna ambavyo tuongeze hela/bajeti hili vijana hawa wajiunge kule kwa ajili ya kwenda kujenga uzalendo, tukiacha miaka kadhaa bila ya kupeleka vijana JKT mimi naiona kwamba itakuwa hatari. Waende huko ili wakajenge uzalendo juu ya nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la mwisho Mheshimiwa Kwandikwa na timu yako juu ya Jemedari wetu Mama Samia Suluhu Hassan, mimi nawaombea sana kwa Mungu, kwa kazi ambayo mnaifanya ya kulinda nchi hii, mipaka yetu na sisi kwa kweli tuko salama ni kwa sababu yenu. Lakini vilevile pamoja na kwamba si Wizara yake leo pamoja na IGP Sirro na Jeshi lake la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi tuko salama ni kwa sababu yao, Mungu akubariki endelea na kazi nzuri ambayo unaifanya ndugu yangu Kwandikwa, ahsanteni sana. (Makofi)