Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kunipatia nafasi hii na mimi niweze kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ulinzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Amiri Jeshi Mkuu Rais wetu wa Jamhuri ya Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya na niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwa heshima na taadhima kabisa kwa kutoa heshima kwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tugonge meza mara mbili ili tuonyeshe heshma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ninaomba nimpongeze Jenerali Mabeyo kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya ya kudumisha amani katika nchi yetu hii ya Tanzania. Lakini pia niipongeze Wizara na Waziri Mheshimwia Elias Kwandikwa, jirani yangu, kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya katika Wizara hii ya Ulinzi lakini mwisho kabisa niwapongeze majenerali na mabregedia wote walioko hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sasa na mimi nianze kuchangia katika hotuba ya bajeti hii. Moja kabisa tunafahamu ya kwamba JKT kwa sasa wameingia katika ushindani wa kuwekeza lakini wameenda mbali Zaidi katika kuhakikisha ya kwamba wana-compete zabuni mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kuchangia kwa maana ya kuiomba Wizara hasa JKT kumekuwa na ucheleweshaji wa miradi inayotekelezwa na jeshi letu la JKT. Nimuombe Waziri Mheshimiwa Waziri utakuwa ni shahidi katika Jimbo langu la Msalala tunao mradi mkubwa wa ujenzi wa jengo la Utawala katika Halmashauri ya Msalala ambayo inatekelezwa na JKT na Mheshimiwa Waziri niseme tu kwamba ukiangalia fedha iliyotengwa walitoa certificate ya kiasi cha shilingi milioni 515 kwa ajili ya hatua za awali za ujenzi wa jengo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo ucheleweshaji umeendelea kuimarika jengo hilo mpaka tunapozungumza sasa bado halijakamilika japo kuna jitihada ambazo zinaendelea. Niombe Wizara Mheshimiwa Waziri unanisikia upo hapo ndugu yangu, jirani yangu, tunapata tabu sana wananchi wa jimbo la Msalala Halmashauri yetu tumekaa katika sehemu ya kupanga tumebanana tunahitaji sasa tuhamie kwenye jengo hilo, niiombe Wizara, niwaombe JKT kumaliza mradi huu kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na malalamiko juu ya wastaafu wetu, juu ya namna gani kuiomba Wizara na Serikali waweze kuwaongezea pension. Kama unavyofahamu wastaafu hawa baada ya kustaafu wanarudi vijijini kuja kujumuika na wananchi, kumekuwa na changamoto nyingi juu ya changamoto za kimaisha katika wastaafu hawa. Niiombe Wizara iweze kuona ninamna gani basi wanaweza kuongeza walau pension kidogo ili wasaidie wastaafu wetu hawa kuendesha maisha yao huko walipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kwa kuwa Jeshi linatoa mafunzo mbalimbali, nikuombe kabla wastaafu wetu hawa hawajastaafu basi ni vyema Wizara ikae na kupanga waone namna gani basi wanaweza wakaanzisha short course ya kuwaandaa wastaafu wetu hawa wanapostaafu waende wakakabiliane na maisha ya huko vijijini. (Makofi)

Kwa hiyo, ni ukweli usiopingika kwamba wazee hawa, wastaafu hawa wanapokuja kule ni kweli usiopingika kwamba wanazalilika sana maisha ni magumu mno, wanapokuja kuanza ku-adopt mazingira ya kule vijijini wanapata taabu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona kwamba kumekuwa na malalamiko kwamba Mbunge mwenzangu amechangia hapa juu ya namna gani askari wetu wanajeshi wetu hawa wanapatiwa mavazi pair chache na ameshauri kwamba ikiwezekana walau waweze kupatiwa pair tatu. Lakini ni ukweli usiopingika kwamba Jeshi lina taratibu zake na taratibu za namna gani kuweza kutoa mavazi haya unaona kabisa hapa wanatakiwa wapewe mavazi mapya ya ndani ya miezi sita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa ninavyozungumza bado baadhi ya wanajeshi hawa hawajapatiwa mavazi hayo mapya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe Mheshimiwa Waziri, vijana wetu hawa wanafanya kazi kubwa sana, lakini pia na wao wanahitaji wapate mavazi haya ili waonekane smart kama watu wengine, niiombe Wizara kama kunauwezekano basi Wizara ione namna gani inaenda kuwapa mtaji Jeshi la JKT, ili wafungue kiwanda cha kushona mavazi hawa wanajeshi wetu. Kwa kufanya hivyo tutasaidia kutengeneza ajira, lakini tutakuwa tumewajengea vijana wetu ili tuweze kuondokana na adha ya upungufu wa mavazi na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho nimalizie kusema kwamba kumekuwa hakuna usawa juu ya usaili wa vijana wetu huko chini katika ngazi za chini katika kujiunga na Jeshi letu. Taarifa katika baadhi ya maeneo zinakuja leo kesho usaili umekwisha, kwa hiyo, niiombe Wizara ione namna gani inapotoa taarifa za usaili za vijana wetu hawa wapeleke mapema kule, lakini kumekuwa kuna urasimu pale mikoani, vijana wetu hawa baadhi wanaobahatika kuingia katika nafasi hizo wanapofika mkoani wanapewa vikwazo vingi vingi na wengine wanatolewa majina yanakuwa yameandaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe Mheshimiwa Waziri, sisi wana Mkoa wa Shinyanga ni waathirika wa hilo, hebu tuangalie tuone namna gani sasa Wizara inaenda kujipanga kuonesha ya kwamba inaondoa urasimu huo ili vijana na wao wapate sifa ya kujiunga na Jeshi letu hili la wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia naomba niendele kuwapongeza na ninaunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)