Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Dr. Paulina Daniel Nahato

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ili nichangie katika Wizara ya Afya. Awali ya yote napenda kumshukuru Waziri wa Afya kwa kutuwasilishia taarifa yake nzuri. Naomba nichangie katika sehemu moja tu ambayo ni elimu ya afya kwa jamii na hususani nitachangia katika sehemu ya tabia au tuna sema behavior change.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kabisa kwamba magonjwa mengi ambayo yanaikumba jamii yetu yanaepukika. Tatizo kubwa ni kwamba wananchi wengi hawajui na kwamba kwa sababu hawajui hata tabia zile ambazo ni tabia hatarishi ambazo zinaweka katika mazingira ya kupata magonjwa, wananchi wengi hawajui hususani wananchi wanaoishi vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, magonjwa yapo, lakini watu hawajui, hawajui kwa kiwango gani magonjwa yapo na hata kama yapo hawajui yaani hakuna ufahamu wa kutosha kuhusu aina mbalimbali za magonjwa. Magonjwa aina zote; magonjwa ya kuambukiza na yale yasiyo ya kuambukiza. Kwa hiyo, watu wanaishi tu kwa sababu hawajui, mpaka mtu anapofikia sasa anaumwa ndiyo anaanza kushtuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba niishauri Serikali kuimarisha kitengo hiki Elimu ya Afya ya Jamii (public health), watu sasa wafikie kupata taarifa sahihi kwamba magonjwa yako kwa kiasi gani. Elimu itolewe; kwanza watu wajue kuna aina gani ya magonjwa na nini kisababishi cha haya magonjwa, tuna magonjwa mengi ambayo yanayosababishwa kutoka kwa mtu, mengine ni kutokana na mawasiliano ya wanyama na watu, mengine ni wadudu wengine ya kwenda kwa watu, lakini watu hawajui. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wanaishi na Wanyama, hawajui kwamba wanyama wanaambukiza magonjwa zoonotic diseases watu hawajui na kwamba hata yale magonjwa mengine ambayo yanatokana na maziwa, watu wanakunywa maziwa bila kuchemsha, hawajui kwamba ni rahisi kupata magonjwa fulani. Kwa hiyo, kunahitajika elimu kwanza ya kujua kuna aina gani ya magonjwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni kwamba pia elimu itolewe ya kutosha kuhusu watu kubadili tabia zao, tabia ambazo zinaweza kuwaweka katika mazingira hatarishi ya kupata magonjwa. Kila mtu akishajua hivyo ni rahisi kujichunga na kama mtu mmoja atajichunga basi jamii yote ni rahisi kujikuta kwamba inakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu magonjwa. Kwa hiyo hatutalalamika sana kuhusu tiba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ni kwamba, watu wanaweza kujua juu ya magonjwa, lakini hawajui faida za kwenda hospitali. Wengi wanakwenda hospitali wakati magonjwa mengi yameshafikia katika stage fulani ambayo ni mbali. Kwa mfano magonjwa labda ya kansa hivi, magonjwa mengine, mtu anakwenda hospitalini akifika kule unakuta imeshakwenda imefikia stage four, sasa pale ndiyo tiba inakuwa ni ghali sana, wakati ambapo huyu mtu angejua dalili za awali, akaenda hospitali huyu mtu angetumia pesa kidogo tu kwa matibabu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo utamaduni wa tabia ya kwenda hospitalini ya kucheki afya mara kwa mara unakuwa haupo hata kwa watu wenye kipato hasa wenye kipato cha juu. Kwa hiyo matatizo haya ya ukosefu wa dawa yanakuja kwa sababu watu wanakwenda hospitali wakati tayari hali imekuwa ni mbaya. Kama ni presha imeshafika juu, kama mtu angekuwa na tabia ya kucheki afya mara kwa mara huenda angeshajigundua ana BP mapema, angechukua hatua mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusisitiza juu ya behavior change, kubadili tabia. Hivyo, basi vitengo katika Wizara ya Afya vijikite katika kuimarisha kubadili tabia behavior change aspect. Baada ya hii watu kujua faida zake pia wajue changamoto ambazo wanaweza kuwa nazo. Mtu akiwa na afya anaweza kwenda hata Mumbai kwenda kucheki afya yake na mtakubaliana na mimi kwamba mtu anaweza akawa anaumwa kichwa, kuumwa kichwa siyo ugonjwa, ni dalili ya ugonjwa fulani, hasa huyu mtu anaumwa kichwa anakunywa panadol anajiona yuko sawa, hafanyi mazoezi anaendelea na shughuli zake, akisikia usingizi anakwenda analala, kumbe huyu mtu ana tatizo kubwa. Anapokuja wanashangaa huyu mtu ameanguka akiletwa hospitalini, huyu mtu yuko ICU matibabu ni makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tujaribu pia kuimarisha hivi vitengo vya kuangalia tabia za watu, wajue pia ni changamoto gani watakazokumbana nazo wanapokwenda hospitali. Kwa hiyo kujengwe na hiyo tabia ya watu kucheki afya zao. Pia wanahitaji kukumbushwa mara kwa mara, watu wakumbushwe mara kwa mara. Hapa sasa siyo Wizara ya Afya tu, tunaingia Wizara ya Maji, yaani Wizarani ichanganyike na Wizara nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Michezo iwakumbushe watu faida za michezo; Wizara ya Maji iwakumbushe watu, Wizara ya Mifugo iwakumbushe watu kutokuchangamana na mifugo; na Wizara ya Uvuvi iwakumbushe watu kutokutumia yale maji ambayo ni machafu. Kwa hiyo watu wapate kukumbushwa mara kwa mara na hivi vyombo vya habari vitumike hususani television, radio, simu, mawasiliano ya mara kwa mara ili watu wakumbushwe wajue hatari na mazingira yaliyoko kwamba ni hatarishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho Wizara pia iangalie suala la kuhakikishwa kwamba watu wanabadili tabia zao na kuwa na tabia zile ambazo zitawafanya wawe na afya ambayo tunaita safe efficacy, ni muhimu sana. Kama hivi vitu vyote Wizara itaviangalia kwa macho matatu, basi uwezekano wa kupunguza magonjwa mengi katika jamii zetu utakuwa ni mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sisi Wabunge ni vizuri kusoma mara kwa mara ili pia tutumike kama chombo cha kufikisha ujumbe wa masuala ya afya kwa jamii. Katika mikutano yetu, tusiongelee mambo yetu ya siasa tu, tuweke kipaumbele katika elimu na sisi tupate elimu, tuwe na shauku ya kujua magonjwa, maambukizi na jinsi magonjwa yanavyokuja na hatua za magonjwa ili watu wetu katika majimbo yetu iwe ni gumzo. Itakapokua ni gumzo tutajenga jamii ambayo itakua na afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kutenga fedha za kutosha katika Idara hii ya Health Promotion and Health Education ili iweze kupata fedha za kutosha na pesa hizi zitumike katika kufikisha elimu ya afya kwa jamii ili watu waweze kuchukua hatua za kubadili tabia ambazo zinawaweka katika mazingira hatarishi ya kupata magonjwa, tutaweza kuokoa fedha nyingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia katika Wizara hii. Naunga mkono hoja. (Makofi)