Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika Wizara hii. Kwanza kabisa ningependa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia uhai na afya tele nimeweza kusimama hapa muda huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ningependa kuzungumzia utekelezaji wa bajeti ya maendeleo katika Wizara hii kwa miaka mitatu iliyopita. Utekelezaji wa bajeti ya maendeleo katika Wizara hii umekuwa hafifu mno kwa miaka mitatu iliyopita. Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya 2018/2019 fedha za miradi ya maendeleo hadi kufikia mwezi Machi, 2019 zilikuwa zimepelekwa kwa asilimia 16 peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2019/2020, na haya sio maneno yangu yapo kwenye randama za Wizara ya Afya za miaka hii mitatu, fedha zilizotengwa zilikuwa jumla ya shilingi bilioni 544.137 lakini hadi kufikia mwezi Machi mwaka 2020 kiasi cha fedha kilichokuwa kimetolewa ni shilingi bilioni 83.06 peke yake sawa na asilimia 15.3 tu. Mwaka 2020/2021 bajeti iliyotengwa ilikuwa ni kiasi cha shilingi bilioni 360.9 lakini mpaka mwezi Machi mwaka 2021, mwaka huu, fedha zilizokuwa zimepelekwa ni shilingi bilioni 83.1 peke yake. Kwa hiyo, utaona ni kwa namna gani fedha zinatengwa lakini haziendi kutekeleza yale ambayo tumekubaliana katika Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na hii inaonesha kwa miaka yote mitatu fedha zimekuwa zikipelekwa angalao kwa asilimia 18 tu kila mwaka. Sasa uone ni namna gani changamoto za afya zinavyozidi kujitokeza kwasababu, fedha zile zilizokusudiwa haziendi kama ambavyo tumezipangia bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na changamoto kubwa sana katika maeneo yetu. Mimi natokea Mkoa wa Tabora, Jimbo la Tabora Mjini; kuna suala la wanawake kwenda kujifungua na kulipa gharama. Unapojifungua mtoto wa kiume utalipa 50,000/= na unapojifungua mtoto wa kike utalipa 40,000/=. Hili jambo lipo katika hospitali za Mkoa wa Tabora, ikiwepo Hospitali ya Kitete ya Rufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na hata juzi hivi ninavyozungumza kuna ndugu yangu katoka kujifungua, amelipa 50,000. Sasa huyo amejifungua mtoto wa kiume, sasa huyo ana uwezo wa kulipa hiyo 50,000/= lakini kuna mwananchi mwingine wa kawaida ambaye uchungu umempata, anakwenda hospitali hana hiyo fedha ya kulipa, vifo vinatokea. Na hii sio uwongo ndio ukweli uliopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ningeomba sana Serikali atakapokuja kwenye majumuisho Mheshimiwa Waziri aje na majibu, hii ni sheria? Ni utaratibu? Ama ni waraka wa Wizara uliokwenda kwenye baadhi ya hospitali wanatakiwa wachangie fedha hizi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwasababu hata sisi wawakilishi wa wananchi tukihoji tunaambiwa hay ani maelekezo. Sasa tunataka tujue hayo ni maelekezo kutoka wapi? Mheshimiwa Waziri aje aseme hapa, ili wananchi wa Tabora wapate kupona kwasababu hii imekuwa kero kubwa sana katika Jimbo la Tabora Mjini na Mkoa mzima wa Tabora. Na ninaamini kabisa kuna baadhi ya mikoa mingine fedha hizi wanalipa wakati wanawake wanakwenda kujifungua. Hii ni kero kubwa sana kwa wananchi wa Jimbo la Tabora na Mkoa mzima wa Tabora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Tabora Mjini hatuna hospitali ya wilaya, lakini tuna kituo cha afya. Kituo hiki cha afya hakina vifaa tiba, hakina wauguzi, hakina madaktari, hakina dawa. Hivyo, inasababisha wananchi wa Jimbo la Tabora Mjini wengi kwenda kusongamana katika Hospitali ya Rufaa ya Kitete na hivyo kusababisha msongamano kuwa mkubwa zaidi kwa sababu, ile ni hospitali ya rufaa. Sasa tunaiomba sana Serikali iweze kusaidia kituo kile cha afya, tunaomba mkakiboreshe, muweze kuweka vitu kwa ajili ya wanawake kujifungua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu anatoka kwenye Kata kwa mfano ya Ikomwa, Ikomwa ni kata ambayo iko mbali sana na pale maili tano. Kwa hiyo, mtu anatoka pale anafika pale maili tano anaambiwa dawa hakuna, anaambiwa hakuna vipimo, anaambiwa hakuna, kwa hiyo, mwananchi anajikuta amechoka kwelikweli kiasi kwamba, anakuwa hana jinsi inabidi arudi jinsi ilivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ningeomba sana Serikali itusaidie iende ikaboreshe kile kituo cha afya. Mnafahamu kabisa Jimbo la Tabora Mjini limegawanyika katika sehemu mbili, kuna kata za mjini kuna kata za vijijini na kituo cha afya kinachotegemewa ni hicho kilichopo maili tano. Sasa tungeomba kama Wizara kuna uwezekano basi tuongezewe vituo vya afya, ili angalao viendane na maeneo ambayo tupo kwasababu, maeneo mengi yako pembezoni na ni makubwa mno na kuna wananchi wanaishi kule, lakini wanapata changamoto kubwa sana ya huduma za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kule kwenye maeneo mengine ya kata za pembezoni hakuna hata zahanati. Watu wanateseka, watu wanapata shida kwelikweli kwasababu ya ukosefu wa huduma za afya. Ningeiomba sana Serikali iuangalie mkoa wa Tabora, iangalie Jimbo la Tabora Mjini tuna changamoto kubwa sana katika huduma za afya. Na haya niliyokueleza ni changamoto ambazo zinatukabili siku hadi siku. Hasa hasa pia, hata hii Hospitali yenyewe ya Kitete ambayo nimezungumza haina vifaa tiba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2018/2019, bajeti ilitengwa hapa kwa ajili ya kufanya ukarabati kwenye vituo vya wazee. Pale Tabora tunacho Kituo cha Wazee Ipuli, kwa kweli kinahitaji ukarabati. Tunahitaji kuwasaidia wale wazee ili na wao angalau waweze kuishi kama wapo sehemu ambapo wanalelewa na Serikali. Kwa hiyo, naomba sana zile fedha ambazo zilitengwa na kama zilikuwa hazijafika basi wajitahidi kuweza kuboresha vituo hivi ili viweze kutunza vizuri wale wazee kama ambavyo Serikali tumekusudia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)