Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Dr. Christina Christopher Mnzava

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipatia nafasi ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Afya. Kwanza niwapongeze sana Waziri pamoja na Naibu Waziri wa Afya na Watendaji wote kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitajikita katika suala zima la miundombinu. Ni dhahiri kwamba Serikali yetu imekuwa ikifanya vizuri sana katika miundombinu ya afya hususani majengo. Ukiangalia katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kulikuwa hakuna hospitali, lakini Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeweza kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo. Hivi ninavyoongea majengo matatu yanaendelea kukamilika, Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi huo. Pamoja na kwamba ili hospitali iweze kukamilika majengo yanayohitajika ni 22 hivyo, tutaendelea kuiomba Serikali yetu sikivu iendelee kutenga fedha za kutosha ili kuweza kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa masikitiko makubwa sana katika Halmashauri ya Msalala kuna Kituo cha Afya cha Ngaya, kimekamilika mwaka 2018, kina wataalam lakini hakuna vifaa tiba. Kwa hiyo, naomba Wizara ya Afya pamoja na taasisi ambazo zinahusika ziweze kukamilisha kutoa vifaa tiba ili Kituo cha Afya cha Ngaya kiweze kuhudumia wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza na kumkumbuka sana Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa aliyoifanya katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama. Halmashauri ya Manispaa ya Kahama imejenga jengo la OPD kwa fedha za ndani, imekwisha kutumia zaidi ya shilingi bilioni 2.7 na inaendelea na ujenzi na tunategemea kufikia mwezi Juni, jengo la hili liwe limekwishakamilika ambalo litatumia zaidi ya shilingi bilioni 3.2.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli, nawapongeza sana viongozi wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama kwa juhudi kubwa walizofanya kuhakikisha kwamba wanajenga hospitali kubwa ya kisasa kwa kutumia mapato ya ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka Mheshimiwa Waziri wa Afya aliahidi mbele ya Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwamba hospitali ile itapandishwa hadhi iwe na hadhi ya hospitali ya mkoa kutokana na kwamba inatibu watu wengi sana kutoka kwenye Wilaya mbalimbali ikiwemo Urambo na Wilaya za Kigoma zote zinakuja Kahama. Hospitali ya Kahama wagonjwa wa nje (outpatient) kila siku wana-attend wagonjwa 800-1,000. Kama hiyo haitoshi, Hospitali ya Kahama ina vitanda 218 lakini wagonjwa wanaolazwa kila siku kwenye ni zaidi ya 300. Kwa hiyo, bado tuna upungufu mkubwa sana wa vitanda katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiaangalia kwa muundo wa Halmashauri ya Hospitali ya Wilaya ya Kahama, kwa ikama inaonekana watumishi wanatosha, lakini kwa uhalisia idadi ya watumishi hospitali ya Kahama hawatoshi. Kwa sababu ya hiyo takwimu niliyoitoa kwamba wana-attend wagonjwa wengi kwa siku kuanzia 800 mpaka 1,000, lakini wanalaza wagonjwa wengi na vitanda ni vichache. Kwa hiyo, bado tunahitaji watumishi wa kutosha kukidhi mahitaji ya Hospitali ya Wilaya ya Kahama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa mama na mtoto, Hospitali ya Kahama ina vitanda 18 vya kujifungulia wanawake, lakini kwa siku wanawake wanaojifungua katika Hospitali ya Kahama ni 35 mpaka 55. Tunaona jinsi ambavyo kuna uhitaji mkubwa wa kuboresha miundombinu katika hospitali ya Kahama.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke Kahama ipo barabara kuu ya kwenda Burundi na kwenda mikoa mingine ya Geita; Kagera pamoja na Kigoma. Pale pana msongamano mkubwa sana wa watu. Kwa hiyo, inachukua idadi kubwa sana kuhudumia watu wengi kutoka sehemu nyingine mbalimbali. Kwa hiyo, napenda Wizara ya Afya iiangalie Hospitali ya Manispaa ya Kahama kwa jicho la kipekee kutokana na idadi ya watu wengi waliopo mahali pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazidi kuipongeza Serikali na kukumbusha kwamba kuna ahadi ilitolewa na Mheshimiwa Rais ya shilingi milioni 500 kama mwanzo wa kununua vifaa tiba. Tunaomba fedha hiyo Serikali yetu sikivu iweze kutoa ili wananchi wa Wilaya ya Kahama waweze kupata vifaa tiba na hospitali iweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaipongeza Serikali, kwa kweli imeweza kujenga vituo vya afya kama Mwendakulima, Nyasubi, kuna waganga, kuna waunguzi, lakini tatizo linarudi pale pale kwenye vifaa tiba. Tunaomba sana vifaa tiba viweze kutolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo haitoshi, katika Halmshauri ya Wilaya ya Kishapu, tuna Kituo cha Afya cha Nobola cha toka enzi za Mwalimu. Kituo kile kinahudumia Kata tisa na pembeni yake hakuna kituo kingine chochote cha afya. Vile vile kutoka pale Nobola kwenye Makao Makuu ya Wilaya ni zaidi ya kilometa 40 mpaka 50. Naiomba Serikali iweze kuboresha na kujenga kituo cha afya kingine katika Kata nyingine aidha Talaga au Lagana ili wananchi wa Wilaya ya Kishapu nao waweze kupata huduma ya afya kwa usahihi na kwa manufaa mazima ya afya zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine, katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini, kuna Health center ambazo zimejengwa vizuri, tunamshukuru Mwenyezi Mungu, tunawashukuru wataalam wetu na tunaishukuru Serikali kwa kutukumbuka watu wa Shinyanga. Kituo cha Afya Samuye pamoja na Tinde vinafanya kazi. Tinde kinafanya kazi vizuri sana, lakini Samuye kimejengwa, kina theatre, kina wafanyakazi, lakini hakuna vifaa, huu ni mwaka wa tatu sasa. Kwa hiyo, tunaona Serikali iweze kukukumba.

Mheshimiwa Naibuy Spika, kuna wananchi wa Kata ya Solwa, wamejenga kituo cha afya kwa nguvu zao, kuna wodi mbili wameshajenga, kuna OPD nzuri, lakini kupandishwa hadhi kutoka kwenye zahanati kuwa kituo cha afya bado Wizara inasuasua. Tunaomba mwafikirie wananchi hawa ambao wametumia fedha zao nyingi kujenga miundombinu hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nitapenda kuzungumzia suala la magonjwa yasiyoambukiza. Kumekuwa kuna mlipuko wa magonjwa yasiyoambukiza kwa wananchi, mengi sana. Mfano, kisukari, magonjwa ya moyo na magonjwa mengine, lakini afua ambazo zinatekeleza intervention hizo zimekuwa zikisuasua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza sana Wizara ya Afya kupitia Kitengo cha Tiba Mbadala. Tunaomba sasa dawa ambazo zinagundulika kwamba zinafanya kazi, ziweze kutolewa kwa bei nafuu, ziweze kupewa vibali ambavyo vinastahiki. Mfano hiyo Phyt Exponent, tunaomba hiyo dawa iweze kupunguziwa masharti, iweze kupunguziwa masharti, iweze kusajiliwa kama dawa ya tiba mbadala kuliko kuwa na Dietary supplement. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, Mheshimiwa.

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)