Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Tecla Mohamedi Ungele

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia hoja kwenye Wizara hii muhimu sana Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kupongeza kazi kubwa inayofanywa na Wizara hii. Mheshimiwa Waziri Dkt. Dorothy Gwajima na timu yake yote, Katibu Mkuu na timu yote mpaka kule kwenye vituo vya afya na zahanati wanafanya kazi kubwa sana kuokoa maisha ya watoto, akina mama na wananchi wote kwa ujumla. Pia naipongeza Serikali nzima kwa ujumla kwa kazi kubwa inayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia muda, naomba nijikite kwenye mambo makuu mawili. La kwanza, upungufu wa watoa huduma katika sekta ya afya lakini la pili, uhaba wa vitendea ikiwepo ambulance na vifaa vingine katika hospitali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kwa ufupi hii suala la ambulance. Tunaona maeneo mengi yako mbali na hospitali za wilaya na huko kwenye maeneo hayo ya vijijini na kwenye kata kunatoa huduma mbalimbali lakini hakuna huduma ya ambulance. Nikitolea mfano kuna sehemu ambayo kuna zaidi ya kilomita 70 lakini inapotokea tatizo hakuna ambulance, mfano Nachingwea tuna ambulance moja ambayo ni mpya kwenye Kituo cha Afya Kilimarondo lakini zile ambulance zilizoko katika Hospitali ya Wilaya ni chakavu, hapa na hapa zinapata breakdown kiasi kwamba hata mgonjwa mwenyewe anaweza akafia njiani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye upungufu wa watumishi kwenye sekta ya afya, tumeona hapa Kitaifa kuna upungufu zaidi ya asilimia 53, hicho ni kiasi kikubwa sana. Nikienda kwenye Mkoa wa Lindi nikitolea mfano Wilaya kadhaa, Wilaya ya Ruangwa tulipaswa tuwe na watoa huduma 840 lakini waliopo ni 257 sawasawa na asilimia 31, upungufu ni asilimia 69. Nachingwea mahitaji ni 1,077 waliopo sasa hivi ni 305 tu upungufu ni 772. Wilaya ya Liwale wafanyakazi wa sekta ya afya ni 510 lakini waliopo ni 221 tu, upungufu ni 289. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama nilivyokuwa nimesema siku moja nilivyochangia mchango wangu hapa kwamba zahanati nyingi zinahudumiwa na medical attendants. Nasema hivi pamoja na upungufu huo, kwa mfano Wilaya ya Liwale mpaka kufika Hospitali ya Wilaya zahanati na vituo vya afya vingine viko mbali sana na ndipo pale tunapokuja kutoa mchango kwa kusema kwamba kuna tembo huko na kadhalika. Kwa hiyo, anapokuwepo mtoa huduma mmoja kwenye health facility fulani anapokuja kupata mshahara na kupeleka taarifa mbalimbali kwenye Hospitali ya Wilaya, humo njiani anakabiliana na mambo mbalimbali ikiwepo na wanyama wakali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huduma ya afya kunapokuwa na upungufu wa rasilimali watu matokeo yake ni kutokutoa huduma nzuri au huduma hafifu matokeo yake yanatokea pale pale, haisubiri baadaye. Labda ni mtu kutokuhudumiwa jambo fulani ni pale pale. Naamini kabisa kuna sekta zingine kama leo kukitokea kupata huduma hafifu matokeo au madhara yake yanatokea baadaye lakini kwenye sekta ya afya kama hakuna huduma nzuri matokeo yake yanatokea pale pale. Kama ni vifo vitatokea pale, kama ni mtu ana changamoto gani ni pale pale haisubiri baadaye. Kwa hiyo, jambo hili la kuwa na rasilimali watu wa kutosha kwenye health facilities ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Nimeona baada ya kutoa changamoto hiyo niseme nini kifanyike? Ya kwanza nimeona, Waziri wa TAMISEMI ametangaza hapa ajira kama zaidi ya elfu mbili kwenye sekta ya afya. Naona jambo hili likitekelezwa kwangu ni faraja kubwa kweli na naamini kabisa Waziri wa TAMISEMI akiungana na Waziri wa Afya watasaidia kuangalia Mikoa ya Lindi na Mtwara na kwingineko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suluhisho lingine ni mikataba ya ajira. Miaka iliyopita Wizara ya Afya iliungana na sekta binafsi kama vile bima na HITECH kupata ajira ya mkataba kwa ajili ya maeneo ya pembezoni, ile ilisaidia sana sijui ile program inaendelea au namna gani? Naomba Wizara ya Afya wajipange kutafuta kama ni wadau wengine kunusuru tatizo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine naomba Wizara husika itoe vibali kwa halmashauri zetu ziajiri kwa mkataba lakini pia kutumia own source kwa ajili ya kuwa-retain wale wafanyakazi. Mara nyingi vijana wanaajiriwa kwenye maeneo yetu lakini kutokana na mazingira fulani baada ya miaka miwili au mitatu wanaomba kuhama. Kwa hiyo, naomba jambo hili la retention liangaliwe sana. (Makofi)

Sisi tulifanya research kuangalia ni jinsi gani itasaidia kuwa na retention mechanism Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa kutumia vyuo vyetu vya afya na halmashauri husika na hili jambo liliwezekana. Naomba jambo hilo liwezekane Wizara husika ya Utumishi itoe vibali vya kutumia own source kwa ajili ya retention mechanism. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)