Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Eng. Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kuwepo ndani ya Bunge lako hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda niwapongeze Menejimenti ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ikiongozwa na Mheshimiwa Waziri, Dkt. Faustine Ndugulile; Katibu Mkuu, Dkt. Zainab Chaula; na Dkt. Jim Yonazi, kwa ajili ya kazi hii kubwa ambayo imefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwapongeze Waheshimiwa Wabunge kwa michango, maoni na ushauri walioutoa, hakika imeonesha namna gani sote tunatembea katika njia moja ya kuhakikisha kwamba sekta yetu na Wizara yetu ya Mawasiliano inazidi kwenda mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite katika baadhi ya maeneo ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyagusia. Tukianza na masuala ya minara ambapo baadhi ya Wabunge wameweza kuonesha kwamba katika maeneo yao kuna changamoto ya minara; mingine ambayo haijawaka, pia ambapo inasababisha na wengine wanasema kwamba ndoa zinavunjika na wengine wanatumia miti kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanapata mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niongelee suala ambalo linahusika na masuala ya mipakani ambapo kuna changamoto ya gharama za mawasiliano kupitia roaming ambayo inafanyika katika mipaka. Naomba nikufahamishe kuwa suala la roaming tayari Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano tumeshalifanyia kazi na tayari tumeshaingia mkataba, Roaming Agreement na wenzetu wa East Africa ili kuhakikisha kwamba gharama za kupiga simu ukiwa katika maeneo ya mipakani zinashuka. Hivyo basi, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wakiwepo katika maeneo hayo, basi hili ndilo ambalo linakwenda kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunafahamu tuna changamoto ya mawasiliano mipakani. Changamoto hii inatokana na mwingiliano wa mawasiliano na kuna maeneo mengine ambayo hakuna kabisa mawasiliano, lakini kupitia Mfuko wa Mawasiliano wa Wote, tumeshafanya tathmini na tunakwenda kuhakikisha kwamba mipaka yetu yote inakwenda kufikishiwa mawasiliano ili kuhakikisha kwamba changamoto hii inaondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na mipaka hiyo takribani minara 160 ambayo itajengwa katika kuzunguka nchi yetu yote katika maeneo ya mipaka, tunafahamu pia kuna baadhi ya ofisi za Halmashauri ambazo ni mpya lakini bado zina changamoto ya mawasiliano ikiwepo Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe ambapo tunakwenda kuweka huduma ya mawasiliano; tuna Wilaya ya Tanganyika, Kakonko, Malinyi, Mtwara DC, Msalala DC, Bariadi, Nzega, Kilindi pamoja na Pangani. Maeneo haya tunakwenda kuhakikisha kwamba katika zabuni ya awamu ya sita yanaingizwa na utekelezaji wake utaanza mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kabisa kwamba Waheshimiwa Wabunge wameongelea masuala ya co- location. Nasi tangu tulivyoteuliwa tarehe 5 Desemba, 2020 na kwa maelekezo mahususi kabisa, mimi pamoja na Mheshimiwa Waziri tulitoa maelekezo kwamba kuanzia sasa hatutajenga mnara ambao utakuwa unatoa huduma ya operator mmoja. Kuanzia sasa tutakuwa na cost sharing, maana yake kutakuwa na co-location, mnara mmoja uweze kuhudumia makampuni mawili au matatu kulingana na uhitaji wa eneo husika. Kwa hiyo, hayo tunakwenda kuyafanyia kazi kwa utaratibu huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo haya yameendana sambamba na kuhakikisha kwamba tunatoa maelekezo kwa watoa huduma kuhakikisha minara yote ambayo ilijengwa ikiwa inatumia teknolojia ya 2G, yote inakuwa upgraded na inatoa huduma ya 3G na 4G. Pia Serikali bado inaendelea kujiridhisha na uhitaji iwapo tutahitaji 5G na pia soko litaamua ni nani atahitaji kutumia. Serikali kazi yetu ni kuhakikisha kwamba tunaweka miundombinu na sera safi za kuhakikisha kwamba wawekezaji wetu wanaweza kufanya biashara bila kuwa na changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunafahamu kabisa kwamba tuna changamoto; na Waheshimiwa Wabunge wamegusia masuala ya vifurushi. Katika suala la vifurushi Waheshimiwa Wabunge wameuliza kwa nini tuwe na bundles? Kwa nini tusiwe na utaratibu wa kutumia mpaka ukamaliza salio lako wewe mwenyewe? Kwa kutumia nafasi hii, naomba nikufahamishe kwamba suala la bundles ni sawa sawa na gharama au biashara ya jumla, lakini Mtanzania hajalazimishwa kununua vifurushi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna huduma ya aina mbili; pay as you go, maana yake ni kwamba unatumia kwa kadri wewe mwenyewe unavyohitaji, lakini pia tuna huduma ambayo ndiyo ya vifurushi sasa ambapo utaamua kuchagua kifurushi cha siku moja, siku mbili, siku tano, ni wewe mwenyewe. Changamoto ambayo tumeiona, siyo kwamba ni kwa nini tununue vifurushi? Watanzania hawajui matumizi, namna gani yanatumika katika simu zao? Sasa hilo Serikali tumeanza kulifanyia kazi kuhakikisha kwamba Mtanzania awe anajua bundle lake limetumika wapi; na ametumia kiasi gani na kwa nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumekuja na utaratibu ambao tunakwenda kuhakikisha kwamba ukishanunua bundle lako kuna njia mbili za kuhakikisha kwamba halipotei. Iwapo muda wa matumizi, kwa mfano, umenunua bundle la siku saba, lakini inafika siku ya saba umeshatumia GB labda tatu na ulikuwa umenunua GB kumi, utakuwa na fursa mbili; ya kwanza ni ku-top up, maana yake utanunua bundle lile lile ambalo ulikuwa umenunua hapo awali maana yake tuta- carry forward ile balance ya bundle lako la hapo awali, maana yake ni kwamba utalitumia. Kama ulikuwa umebakiza saba, maana yake ni kwamba ukinunua 10 utakuwa na 17.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukajua kwamba kuna changamoto nyingine, mwingine atakutwa hana salio la kununua hilo bundle au ku-top up, maana yake ni kwamba utakuwa unaruhusiwa sasa kuhakikisha kwamba unamhamishia rafiki yako ambaye ataweza kuitumia hiyo bundle, nafikiri itakuwa kwa maelewano yenu ninyi binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utakuwa umehakikisha kwamba bundle lako, kama ni 10 GB utakuwa umeweza kuzitumia zote. Kama utashindwa kuzitumia zote, basi rafiki yako. Tutakuwa na utaratibu wa kuhakikisha kwamba kiwango cha chini cha kuhamisha bundle ni MB 250, lakini utakayemhamishia hataruhusiwa yeye kumhamishia mtu mwingine. Utakayemhamishia, yeye ataruhusiwa kuitumia mpaka itakapokwisha. Haya yote tunaendelea kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunafahamu kwamba kuna changamoto ya masuala ya gharama. Serikali ni Sikivu; na hili tunaendelea kulifanyia mchakato, tutakapokuwa tumejiridhisha, kwa sababu biashara hii inahusisha pande tatu; Serikali, watumiaji na watoa huduma, pale ambapo tutaamini sasa kwamba tumefikia maelewano ya kutosha, basi tutakuja na mpango ambao utahakikisha kwamba unawasaidia Watanzania ili waendelee kufanya biashara mtandao na kufanya mambo mengine ya msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kwamba tunaelekea katika uchumi wa kidigitali. Uchumi huu wa kidigitali tunahitaji kuwa na uwezo wa kufanya biashara mtandao, biashara mtandao hii inatokana na miundombinu ambayo tutakuwa nayo sisi Watanzania, miundombinu ambayo itakuwa wezeshi ambazo ndiyo drivers za kutufikisha sasa kwenye uchumi wa kidigitali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa tuna miundombinu ya aina tofauti; kuna Mkongo wa Taifa ambao mpaka sasa tumeshajenga takribani kilometa 7,910 na tayari kuna zingine tena tunaelekea kujenga kilometa 409. Vilevile katika mwaka fedha huu ambao tunaombea bajeti hii tunaenda kujenga kilometa 1,880. Kadri ambavyo muda unaenda, tutakuwa tunahakikisha kwamba baadhi ya changamoto tunazifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nashukuru Waheshimiwa Wabunge wamegusia suala la National Internet Data Center, kwa kweli Data Center yetu ina uwezo mkubwa ni three tier kama walivyosema ambayo ina interruption ambayo inaenda kwenye 99.82 ambapo kwa kweli hii ni ya kiwango cha juu, kwa sababu kiwango cha juu kabisa katika ubora wa Data Center ni tier four. Sasa tunaamini kabisa kwamba katika Afrika Mashariki na Kati Data Center yetu inatosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wakiwa na biashara zao, wakiwa na makampuni yao, Data Center yetu ni sehemu sahihi kwa ajili ya kutunza taarifa zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna miundombinu ya anuani za makazi na postikodi; ili tuweze kufanya biashara mtandao kuna mazingira ambayo yatatufanya sasa tuweze kufanya biashara yetu bila kuwa na changamoto yoyote. Wizara yetu tayari imeshatenga bilioni tatu katika mwaka wa fedha 2020/2021, lakini imetengewa kiasi kingine katika bajeti hii inayokuja kwa ajili ya kuhakikisha kwamba anuani za makazi na postikodi zinakuwa vizuri. Hii faida yake ni kwamba; wenzetu wa halmashauri itawasaidia kupanua wigo katika ukusanyaji wa mapato. Pia Mamlaka ya Mapato Tanzania itawasaidia kuwajua walipakodi wao na wafanyabiashara wao ili kuweza kuhakikisha kwamba wanapofikia hatua ya kukusanya kodi, basi watawafikia kiurahisi, kwa sababu hii itaweza kutoa anuani pale ambapo mlipa kodi alipo na nyumba anayokaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumekuja na mfumo wa kuhakikisha kwamba una uwezo wa kumfikia mwenzako pale alipo kwa kutumia application inaitwa NAPA, ambapo sasa badala ya kutumia Google Map, sisi tumejiongeza na kuhakikisha kwamba tunatumia mfumo wetu ambao umejengwa na vijana wa Kitanzania, ambao ni vijana wetu, kwa sababu sisi kama Serikali tumeamua kuhakikisha kwamba tunawekeza zaidi katika local content.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo local content ambayo ni ya watu wa kutoka nje, ni local content ikiwa na maana anayeifanya kazi ni Mtanzania mwenyewe na vilevile anaye- deploy ni Mtanzania mwenyewe. Kwa hiyo tunaamini kabisa iwapo anuani za makazi, mradi huu utakapokamilika na niwaombe Waheshimiwa Wabunge tutakapofika katika halmashauri zao waweze kutupa ushirikiano pale ambapo tutakuwa tunaweka hizi alama na majina ya mitaa, basi tusiwe na changamoto yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu tunautekeleza kwa ushirikiano mzuri sana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Pia tunawapongeza sana Wakurugenzi nchini kote wamekuwa wakitoa ushirikiano wa kutosha. Tunaamini kwamba tukishafikia hapa basi tutakuwa tuna uwezo wa kufanya biashara mtandao, tutaweza kuagiza bidhaa yoyote ukiwa umekaa nyumbani na ukaweza kufikishiwa nyumbani bila kuwa na changamoto yoyote. Tunaendelea vile vile kuimarisha mifumo yetu ya kifedha ambayo haitotoa nafasi ya udanganyifu wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kabisa kwamba teknolojia inakimbia kwelikweli lakini na sisi tumejipanga kwelikweli kuhakikisha kwamba iwe kama mwizi na Polisi, kwamba hatutaki kuachwa nyuma, kama itafikia sasa wakati ambapo itabidi tutumie block chain technology huu ndiyo wakati wenyewe. Tutajiridhisha wapi tutumie na tutakapokuwa tayari Waheshimiwa Wabunge, basi tutakuwa tumefikia katika lengo ambalo litakuwa linasaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge pia wameongelea suala la utapeli mtandaoni, hasa tuma pesa kwa fulani, tuma kwenye namba hii. Naomba nikujulishe, tumeunda Kamati, ambapo kikao cha Makatibu Wakuu ambao tunalenga katika hii sekta sana sana katika masuala ya cybercrime, maana kwamba nani hii makosa ya kimtandao, wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia Habari na watu wa Sheria watakaa tarehe 20 kwa ajili ya kujadili namna bora ya kuhakikisha kwamba haya masuala tunayatatua. Ikiendana sambamba na hiyo, tarehe 26 kikao cha Mawaziri pia kitakaa kwa ajili ya ku-finalize na kujua kwamba tufanye jambo gani. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Waziri.

NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)