Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia jioni ya leo katika sekta hii muhimu sana ambayo ni sekta mtambuka kabisa katika nchi yetu. Nafahamu kwamba mawasiliano ni muhimu sana ndiyo maana hata ukiangalia Waheshimiwa Wabunge wote hapa wameinamia simu zao kuonyesha kwamba mambo mengi hayawezi kwenda pasipo kuwa na mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia eneo moja, mimi niiombe kwanza Serikali iwekeze sana kwenye TTCL kwa sababu kazi yake ni kutoa huduma. Nimeona mara nyingi hapa watu wanamlazimisha Waziri kwamba waambie watu wa mitandao waende wakajenge hap ana pale, watu wa mitandao hawawezi kujenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimefanya kazi kwenye mitandao miaka 20, nilikuwa Mkurugenzi wa Kanda, unaomba minara 50 unaambiwa useme utaturudishia nini (Return on Investments). Kwa hiyo, unless Serikali wakati inatoa ile license ilimwambia yule mtoa huduma kwamba tunataka uende vijijini utujengee minara vijiji 500 lakini kama ulimkaribisha tu ukampa leseni huwezi ukamlazimisha. Kwa hiyo, ni kazi ya Serikali kuona kwamba inaiwezesha hii TTCL ipate pesa ya kutosha. Tukiiambia Serikali itoe pesa hizo ndiyo tutakuwa na haki ya kuiambia Serikali hapa sina mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kushauri ni kwamba TTCL ijiendeshe kibiashara. Kwenye mawasiliano kuna ushindani mkubwa sana, yaani ushindani kwenye mawasiliano katika nchi ya Tanzania ni mkubwa mno. Huwezi ukasema kwamba TTCL ifanye vizuri kama hujaipa pesa! Hata kuajiri kwenye mitandao huwa kunyangana wafanyakazi, mtandao huu ukiona kuna mfanyakazi mahali fulani anafanya vizuri zaidi unapanda dau unamchukua aje kwako. Sasa na sisi kwenye TTCL kama Serikali tunaweza kuamua kubadilisha kanuni kwamba namna tunavyoajiri iwe tofauti na yanavyoajiri mashirika mengine ili tuwe na ushindani wa kweli. Tusipofanya hivyo hatuwezi kufika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine ambalo nataka kuzungumzia hapohapo kwenye TTCL, mwaka 2003 niliingia kwenye Task Force ambacho ni kikosi maalum kwa ajili ya kuuza simu za mezani zilikuwa zinaitwa People’s Phone, wengi mtakuwa mnazifahamu. Baada ya kuona haziende Kampuni yangu ya Vodacom kwa wakati huo ikaunda timu ya watu watatu na mimi ikaniweka kitengo cha mauzo. Nikafikiria nifanye nini, mimi ndiyo mwanzilishi wa hao mnaowaita freelancers, ikabidi niishauri kampuni yangu inipe pesa ili mimi nilete vijana ambao watakwenda mlango kwa mlango kuuza simu. Baada ya kunikubalia, tuliuza zile simu ndani ya mwaka mmoja nchi nzima ilikuwa tayari imeshapata hizo simu za mezani. Kwa hiyo, tuipe nafasi pia TTCL ili iweze kutumia huu mfumo wa freelancers. Tukifanya hivyo, itaweza kupata wateja wengi, hilo nilipenda kushauri pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande mwingine ni upande wa Shirika hili la Mawasiliano (TCRA). Ninaiomba sana TCRA iimarishe mahusiano na watoa huduma. Kumekuwa kama kuna uadui fulani. Nilizungumza siku moja na Waziri kwamba huyu mtoa huduma akifanya kosa kidogo, anapigwa faini kubwa. Kwa hiyo, kumekuwa kuna uhasama wakati mwingine kati ya watoa huduma na hiki chombo ambacho kinadhibiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara inahitaji mahusiano duniani, usipokuwa na mahusiano, huwezi kufanya biashara. Kwa hiyo, napenda Waziri hilo alisisitize sana kwa watu wake. Hii TCRA isiwe Polisi. Ikiwa Polisi, itaharibu biashara, nasi tunahitaji biashara. Kama tunataka hawa watu wawekeze, ni lazima tuwabembeleze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka kuzungumzia ni UCSAF. UCSAF nayo siamini sana kama inapewa pesa ya kutosha. Naishukuru Serikali kwa kuamua kutengeneza huu mfuko ili kusaidia mawasiliano vijijini. Kama nilivyosema kwamba hawa watoa huduma wengine kwenda vijijini hawawezi kwa sababu minara mingi vijijini, unakuta mnara unaleta shilingi milioni moja. Wewe umejenga kwa shilingi milioni 300, lakini kwa mwezi unakupatia shilingi milioni moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unauhudumia huu mnara kwa shilingi milioni 4.8 kwa sababu mnara mmoja kuweka majenereta unaweka lita 2,000 za mafuta unakuta kwamba unatumia kati ya shilingi milioni 4.8 mpaka shilingi milioni tano kwa ajili ya kuuhudumia, lakini unakupa shilingi milioni moja au shilingi 800,000. Kwa hiyo, hakuna mtoa huduma ambaye atakuwa na hamu ya kwenda huko. Ndiyo maana tunaomba hii UCSAF ipewe pesa ya kutosha ili Watanzania wengi wapate mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, nije kwenye Jimbo langu. Jimbo langu nalo lina mawasiliano hafifu katika kata nyingi. Ukiangalia Kata za Magulilo, Wasa, Mgama, Kiwele, Ulanda, mawasiliano yako hafifu. Pia kuna Kata moja ya Masaka, haina mawasiliano kabisa na Kata ya Kihanga pamoja na Kata ya Wasa, naiomba Serikali, kale kasungura kadogo ambako tunakwenda kugawana, nami basi kule Kalenga Waziri unikumbuke kidogo kupitia mfuko huu. Siwezi kusema nikushikie shilingi hapa, siwezi kwa sababu najua huna pesa. (Makofi)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, namsaidia tu Mheshimiwa kwa kumwambia kwamba TTCL ilikuwa na minara nchi nzima ikauza kwa American Tower, sasa hivi inakodi. Yaani iliuza kwa gharama nafuu, sasa hivi inakodi minara. Sasa tutapataje mawasiliano? Endelea Mheshimiwa. (Kicheko/Makofi)

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninachosema ndugu yangu, Mheshimiwa Dkt. Ndugulile, ni kwamba nami mwenzako…

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeipokea taarifa hiyo, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitafafanua anachozungumza huyu; anachozungumza ni suala tu la kimazingira kwamba ilikuwa ni makubaliano ya makampuni na Serikali iliridhia kwamba hatuwezi kuwa na minara mingi, kwa sababu mnara ule mmoja siyo mawasiliano, kinacholeta mawasiliano ni zile antenna tunazofunga.

Kwa hiyo, kampuni hata tano zinaweza zikafunga kwenye mnara mmoja na bado watu wakapata mawasiliano ya makampuni tofauti. Kwa hiyo, hilo lisikutishe kuona mahali minara inaondolewa, lakini hata ukibaki mmoja, makampuni hata kumi yanaweza yakautumia mnara mmoja na mawasiliano bado watu wakaweza kupata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kule Kalenga…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante. Dakika zako saba zimekwisha.
Mheshimiwa Dkt. Kimei. (Kicheko/Makofi)

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)