Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Husna Juma Sekiboko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Mawasiliano ambayo ni moja ya Wizara muhimu sana katika uchumi wa nchi yetu. Napenda kupitia kwenye mambo mawili, lakini kabla sijapitia huko naomba nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi nzuri ambayo wameanza kuifanya katika Wizara hii mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ambalo napenda kulizungumza limezungumzwa na Wabunge wengi ni kuhusiana na mawasiliano kwenye baadhi ya vijiji. Actually, inasikitisha na inashangaza sana kwa nchi ya Tanzania nchi ambayo sasa tunajinasibu kwamba tuko kwenye uchumi wa kati lakini tunashindwa kukusanya mapato haya yaliyo wazi kabisa kutoka kwenye simu, kwa kutokupeleka mawasiliano kwenye baadhi ya maeneo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kata nyingi zinakosa mawasiliano lakini pamoja na kukosekana kwa hayo mawasiliano tunayo kampuni yetu ya Serikali ya simu ya TTCL ambayo ingeweza kuchukua hiyo fursa, hiyo changamoto ikageuza kuwa fursa na kwenda kuwekeza kwenye hayo maeneo kwa maana ya kujenga minara na kuweka mawasiliano ya simu na internet kwa ajili ya kurahisisha huduma kwa wananchi, lakini vilevile kupata soko na kuimarisha uchumi wa Shirika hilo. Hata hivyo, hilo halifanyiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii sasa kuishauri Serikali na Shirika letu la TTCL, kuamua kwa dhati kabisa kwenda kuwekeza huduma hii ya mawasiliano katika yale maeneo ambayo mitandao mingine haijafika. Nina mfano wa baadhi ya maeneo kule Lushoto Jimbo la Mlalo kuna maeneo ya Bustani kule Rangwi na kuna maeneo ya Umba kule Mlalo, kuna shida kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia kwenye maeneo ya Muheza kuna Kata inaitwa Kwemigondo ni around kilometa 30 tu kutoka Makao Makuu ya Wilaya pale Muheza, lakini uwezi kuamini kwamba ukaribu wa kiasi hicho kutoka kwenye Makao Makuu ya kwenda kwenye hiko kijiji ama hizo kata hakuna mawasiliano ya simu kabisa siyo makampuni mengine wala siyo kampuni yetu ya TTCL. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kidogo inaleta shida ni vizuri wenzetu wakaona sasa umuhimu wa kwenda kuwekeza huko siyo tu kwa ajili ya kukusanya mapato kwa sababu wakitumia simu wanalipia siyo tu kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano. Lakini vile vile, kwa ajili ya kuwasaidia hawa watu kuwaweka salama kwa maana watakuwa wanapata nafasi nzuri ya kutoa taarifa ya kiusalama pale ambapo panakuwa na changamoto kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ambalo nilitamani kulisema ni kuhusiana na uwekezaji ambao kwenye kampuni ya TTCL. Kampuni kwa kipindi kirefu sasa tangu uhuru, tangu tupate uhuru kampuni hii imekuwa ikifanya kazi kwa mazoea kiasi cha kutokuwa na mabadiliko makubwa ukiendana na uwekezaji mwingine unaofanywa kwenye makampuni ya binafsi. Sasa nishauri Serikali kuwekeza kwa maana ya kufanya pia mapinduzi kwenye utumishi wa kampuni ya hii kwa maana ya kuajiri vijana ambao wanahari na uwezo wa kuwajibika na ambao wako tayari kuwa na mawazo mapya ya kimtandao kama ambavyo yanaonekana sasa kuliko kuendelea kuwekeza fedha nyingi kwenye kampuni hii tunaipa mishahara mingi, lakini hakuna mabadiliko eneo linaloleta tija katika kampuni hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo nilipenda kulizungumzia kuhusiana na gharama za mawasiliano. Hapo kati pametokea sana sinto fahamu ya kupanda na kushuka kwa gharama za mawasiliano hasa kwa maana ya muda wa mazungumzo na bando, lakini bado hatujawa na utaratibu ambao kweli unatu-guide namna gani ambavyo tunaweza tukatumia hizi bando hizi dakika kwenye mitandao mingine ambayo wanafanya biashara, mitandao mingine unakuta wana bei tofauti na mitandao mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Mtanzania mlaji tuko kwenye soko huria, lakini je kama nchi tunapaswa kununua vifurushi hivi angalau isizidi kiasi gani na isipungue kiasi gani? Ni jambo muhimu sana wananchi wetu wakalifahamu hilo ili waweze kupata huduma hiyo wakiwa wanafahamu kiunagaubaga namna gani inatakiwa kugharamiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hayo naomba nikushukuru kwa fursa hii naunga mkono hoja. (Makofi)