Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kunipatia nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Msalala. Nami naomba nichangie hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niende moja kwa moja kwa kuipongeza Wizara kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya katika Taifa letu hili la Tanzania. Pia, niende moja kwa moja kuipongeza Serikali kwa kufikiria na kuanza ujenzi wa standard gauge kwa maana ya kwamba reli ya kati na kufikiria kujenga bandari kavu katika Kata ya Isaka ambayo matumaini yetu kama wana Msalala ni kuhakikisha ya kwamba bandari hii itakapokamilika itaenda kukuza uchumi wa Jimbo la Msalala katika kata ya Isaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwa kuipongeza Wizara na hasa bandari kwa kutupatia mabati 300ya CSR kwa ajili ya ukamilishaji wa kituo cha afya katika Kata ya Isaka. Ahsanteni sana, kwa niaba ya wana Msalala tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja nizungumzie suala la barabara katika Jimbo langu la Msalala. Hali za barabara katika Jimbo langu la Msalala ni mbaya sana. Nimekuwa nikipiga kelele hapa suala la barabara inayotoka Bulyanhulu – Kahama. Barabara hii ni muhimu sana katika uchumi wa Tanzania kwani wote ni mashahidi ya kwamba Serikali yetu inapokea fedha nyingi sana kutoka katika Mgodi ule wa Bulyanhulu lakini barabara hii inahudumia wakazi wengi sana wa Jimbo la Msalala lakini pia wa Mkoa wa jirani wa Geita. Lakini, ndiyo shortcut
ambayo mtu anaenda Geita, ni rahisi kwake kupita pale katika Jimbo la Msalala kuelekea maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii kama nilivyosema hapo mwanzoni kwamba kuna fedha imetengwa na nikaomba Wizara ya Ujenzi, Madini na nikamuomba Waziri wa fedha wakae kwa pamoja waone namna gani fedha hizi zinaweza zikatoka kwenda kukamilisha barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona hapa kama Wabunge wenzangu walivyochangia kwamba ni ukweli usiopingika kwamba tunaona kabisa kama Mbunge mwenzangu Kunambi amesema kwamba anashangaa ni vigezo gani vinatumika Wizarani katika kugawa fedha hizi. Nimeona hapa barabara hii Geita – Bukoli – Kahama imetengwa kwenye route tatu na route tatu hizi ukiangalia Geita kwa maana ya kwamba Bulyanhulu junction road wametenga kiasi cha shilingi bilioni 1.5 lakini hivyo hivyo junction road to kahama wametenga bilioni 1.5.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukiangalia hapa barabara nyingine ambayo inaenda Uyoga – Nyamilangano, barabara ile ile route ile ile, wametenga kiasi cha shilingi bilioni 3, usawa uko wapi? Mmetenga kiasi cha shilingi bilioni 6 kwa maana ya kwamba mmetenga route tatu. Kwanini route ya kwanza mmempa bilioni 1.5, route ya pili mmetupa bilioni 1.5, halafu route ya tatu mkampa bilioni 3? Basi toeni hiyo bilioni 1 mtugawanyishe huku milioni 500, 500 ili wote twende sawa bilioni 2, 2 Mheshimiwa Waziri, nadhani unanisikia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Mheshimiwa Waziri, barabara hii japo ina urefu wa kilometa 160 lakini kilometa zilizotengwa hapa ukiangalia ni jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 6 ambayo ni kilometa 6 tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niendelee kuwapongeza na kuwaomba barabara muhimu naona hapa tumetengewa barabara ambayo inatoka Ntobo – Busangi – Ngaya – Buluma – Jana mpaka Didia mmeitengea kiasi cha shilingi milioni 170 kwa kutengenezwa kiasi cha kilometa 4.8 lakini mmeenda tena mnatutengea kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya kilometa 2.8.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ina urefu wa kilometa 85 lakini ukiangalia hapa ni kilometa kama saba ndiyo mmetutengea hapa. Barabara hii ni muhimu katikauchumi wetu huu wa Jimbo la Msalala. Barabara hii inahudumia Kata ya Ngaya, Kata ya Jana, Kata ya Kashishi na maeneo yote haya ni wazuri wa kuzalisha mpunga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo cha mpunga, unapozungumzia mpunga asilimia 85 ya mpunga unaopatikana Kahama unatoka katika Jimbo la Msalala kwenye kata hizi. Matumaini yangu ni kwamba barabara hii ikienda kuimarika itainua uchumi wa Jimbo langu la Msalala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri, barabara hii muendelee muichukue moja kwa moja. Muimiliki, namaanisha kwamba muiingize kwenye matengenezo ya kila mwaka ili wananchi…

NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Kengele imegonga Mheshimiwa.

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, ninaomba niunge mkono hoja. (Makofi)