Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Twaha Ally Mpembenwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika Wizara hii ambayo ni muhimu sana. Awali ya yote, naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake kwa wasilisho zuri la bajeti ambayo walikuwa wamelileta mbele yetu ambalo linaweza kuleta matumaini kwa namna moja ama nyingine, ukizingatia kwamba kuna changamoto Wabunge wote tunafahamu katika Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri pamoja kwamba leo, nimeomba Mwongozo, imekuwa bahati kubwa sana kwasababu nimeweza kupata meseji kutoka kwa Meneja wangu wa TANROADS Mkoa akisema kwamba ndani ya wiki mbili zijazo ile Barabara ya Bungu – Nyamisati sasa inakwenda kutangazwa. Kwa tafsiri hiyo tunakwenda kumpata mtaalam kuanza hatua za awali za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri katika hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa tafsiri hiyo hiyo, japokuwa ulikuwa umetoa ushauri mzuri sana kwamba nibaki na mmoja, sasa kwa haya ambayo yameweza kufanyika naona wazi kabisa kwamba jambo lile la kupata mke wa pili linaanza kusogea karibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Serikali hasa katika miradi mikubwa mikubwa hii. Naomba niishauri Serikali kwa tafsiri kwamba miradi mikubwa mikubwa jana Mheshimiwa Reuben alikuwa amejaribu kuzungumza mambo ya finance model, ni jinsi gani tutakavyoweza kui-finance hii miradi mikubwa mikubwa. Ni ukweli uliokuwa wazi Watanzania tunahitaji maendeleo, ni ukweli uliokuwa wazi, Watanzania wana matumaini makubwa sana na Serikali ya Chama cha Mapinduzi, kwani mengi makubwa yameweza kufanyika katika awamu zote hasa katika Wizara hii. Makubwa sana yameweza kufanyika na sina shaka Awamu ya Sita vilevile inakwenda kuyafanya mambo makubwa na mazuri hasa katika Sekta nzima ya mambo ya Uchukuzi na Usafirishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri hasa katika Mradi wetu wa SGR. Katika mradi huu tuangalie financing model, kwa sababu mradi utakapokuwa umeweza kukamilika tafsiri yake pana ni kwamba tunakwenda kuhuisha matumaini upya ya Watanzania, sio tu katika maeneo ambayo yanapitiwa na mradi huo, lakini kwa Watanzania wote kwa ujumla wake. Kwa sasa tuweze kujaribu kuangalia, ndio maana naanza kurudia tena neno langu hili, lile suala la PPP lina shida gani! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lilizungumzwa hapa Bungeni mwaka 2018 wakati sisi wengine tulikuwa hatua hata ndoto za kuja hapa Bungeni. Sasa shida iko wapi? Tujaribu kuangalia masuala haya kwa sababu tunapokwenda kukopa masharti yanakuwa mengi na Mheshimiwa Reuben amezungumza kwa kirefu sana na sidhani kama atakuwa ameeleweka vizuri. Alizungumza kwamba tunapokwenda kukopa tunapewa na masharti, wanatupa fedha na wakandarasi wanakuwa hao hao. Sasa sisi kama Serikali tujaribu kuweza kuangalia ni jinsi gani tunakwenda kuangalia suala zima la PPP na kuweza kukamilisha hii miradi mikubwa mikubwa. Huo ni ushauri wangu wa kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu wa pili kwa Serikali, naiomba sana Serikali, bahati mbaya sana ama bahati nzuri Wabunge sisi tunasoma hizi bajeti. Sio tu kwamba tukija hapa tunapiga makofi tunaondoka, hapana. Bajeti iliyokuwa imesomwa mwaka juzi, kuamkia mwaka jana, mwaka jana kuja mwaka huu kuna mambo yanakuwa yanaainishwa mle ndani. Wanavyosema kwenye bajeti hii kwamba upembuzi yakinifu umekamilika tunasubiri ujenzi, inasikitisha sana ukija tena katika mwaka huu tunaanza kumtafuta mtalaam wa kuweza kufanya upembuzi yakinifu. Tukifanya hivi tuna-send wrong signal kwa wananchi ambao wana matumaini makubwa sana na Serikali hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba sana kwa wale wataalam wetu ambao wanaandaa bajeti hizi, naomba twende tukatoe tahadhari kule kwamba Bunge hili la Kumi na Mbili, hawa watu wanasoma. Tunasoma hizi bajeti zinavyokuwa, tunapitia nyaraka moja hadi nyingine. Kwa hiyo, tukija hapa na majibu tunayoyategemea sio majibu ya kisiasa siasa. Tunategemea tupate majibu ambayo yanakwenda kwenye uhalisia ili sasa wananchi wale waliokuwa wametupigia kura kwa kishindo na Chama Cha Mapinduzi kikawa kimeingia madarakani waendelee kuwa na matumaini na nchi yetu hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho naomba nizungumze, pamoja na uhalisia kwamba tayari nanyemelea kupata mke wa pili kwa sababu ya ile barabara ya Bungu – Nyamisati, pale kwetu vile vile kuna barabara ya kutoka Kibiti – Demani kwenda kule Mloka. Hii ni barabara muhimu sana kwa sababu kule ndiko mradi ule wa Mwalimu Nyerere unafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba sana Serikali, najua pamoja na mambo makubwa na mazuri ambayo tayari tumeshayafanya kama Serikali katika Sekta nzima ya Mambo ya Ujenzi na Uchukuzi lakini vile vile tuangalie. Nimewasifia hapa kwamba imefanya vizuri, sina maana kwamba eti kwa sababu Kibiti haikuwekewa bajeti ile nisiseme kwamba mmefanya vizuri, hapana! Mmefanya vizuri sana lakini tuweze kuangalia vile vile uwezekano wa kuweza kupatikana fedha za dharura ili pale watu wa Kibiti na Demani kule ambako wananchi wangu wanakohoa sana kwa vumbi na malori yanayopita pale kwa kupitia mizigo ile inayokwenda kule kutengeneza mradi ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ikiwezekana Mheshimiwa Waziri ungekaa na wataalam wako kama kuna ka– emergency kule pembeni basi kaweze kutoka kale kafedha uweze kwenda kufanyika hatua za awali za upembuzi yakinifu ili sasa tuweze kuangalia jinsi gani tutakavyoweza kuokoa wananchi wale kuondokana na matatizo ya kifua wanayoyapata. Magari mengi sana yanapita pale, na haya mambo ukiona mtu mzima anapiga piga kelele, kuna jambo, Mheshimiwa Aweso huwa anasema hivyo. Ukiona mtu mzima anapigapiga kelele, kuna jambo, Mheshimiwa waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, amezungumza hapa jana, alisimama kwa mara ya kwanza sikutegemea. Alisema kutoka pale Mbeya kwenda Tunduma kapata kilometa tano ndani ya miaka 6. Haya mambo ya kuona sana, sasa mtu mzima akiwa amesimama hivi, kuna jambo. Ninavyozungumza kwamba jamani nawataka wale wake wanne, liko jambo! Wazee wameniahidi wale kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri sitaki wewe mchawi wangu. Najua utalifanya hilo na nina imani sana na Serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi hasa Serikali ya Awamu ya Sita kwa mambo makubwa na mazuri ambayo yanakwenda kutekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, nashukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)