Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, lakini pia namshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyenipa uzima hata niweze kusimama hapa katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kupongeza ushindi wa kishindo wa Majimbo mawili ya Kigoma; Jimbo la Buhigwe na Jimbo la Muhambwe. Kwa kifupi sana napenda niwataje makamanda ambao walikwenda kwa niaba ya Wabunge wengine wote kufanya kazi. Hawa walikwenda front line. Napenda kumtaja Major General Shangazi; Mheshimiwa Shangazi, pia Major Aeshi, Major Jacqueline Msongozi, Captain Bupe Mwakang’ata, Captain Mariam Ditopile na Afande Santiel, ambao walishiriki kikamilifu katika Jimbo la Buhigwe na kuhakikisha ushindi wa asilimia 83. Hongera nyingi sana kwao. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka sasa niende kwenye mchango wangu. Napenda kuzungumzia Daraja la Mkenda ambalo linakwenda Mitomoni…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Jacqueline hivyo vyeo vya kijeshi sijajua kama mmetunukiwa kule au ndiyo unatunuku sasa hivi humu ndani! (Kicheko)

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Hii ni katika shughuli mahususi, inaruhusiwa. Daraja la Mkenda kwenda Mitomoni Wilaya ya Nyasa kuna kivuko kinaitwa Limonga. Kivuko hiki kimekuwa na changamoto kubwa sana. Kivuko hiki kina upana wa karibia mita 100 kama sijakosea, lakini pia napenda tu kusema, Serikali hii badala ya kuweka tu kile kivuko cha kuwabeba wale watu na kuwavusha, basi lijengwe daraja moja kwa moja kwa sababu tayari imeshaleta maafa makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kivuko hicho tarehe 1 Julai, 2016 wananchi 10 walipoteza maisha akiwepo Zuhura, Awetu, Fadhili, Rajabu, Bahati, Khadija, Saidi, Selemani, Omari na Juni. Kana kwamba haikutosha, mwaka 2020 mamba alipindua mtumbwi. Sasa itoshe tu kuona kwamba Watanzania wenzetu wanapoteza maisha sana katika kivuko kile. Naiomba sana Wizara, ione umuhimu wa kwenda kuweka mikakati mizuri ambayo itasaidia na itaondoa adha hii ambayo imekuwa ikisababisha wananchi hawa wanapoteza maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie Bunge lako Tukufu hili kumwomba Waziri mwenye dhamana aongozane nami baada ya Bunge hili, pamoja na Mbunge wa Jimbo la Nyasa na Mbunge wa Jimbo la Peramiho, twende kwa pamoja kwenye kivuko kile kuhakikisha kwamba mikakati mizuri inawekwa kwa ajili ya kuokoa ndugu zetu hao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuzungumzia barabara ya kutoka Mtwara Pachani kuelekea Tunduru kupitia Ruchiri – Rusewa – Magazini – Narasi – Mbesa – mpaka Tunduru. Barabara hii ina urefu wa kilometa 300 ni barabara ya kimkakati ambayo itasaidia kurahisisha usafirishaji lakini kuchochea kasi ya uchumi katika Mkoa wa Ruvuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, napenda nizungumzie mpango mzuri wa Serikali wa kuhakikisha kwamba miji mikuu inapokuwepo basi barabara za pembezoni zinawekwa, barabara ambazo haziingiliani na mambo ya malori katikati ya miji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napenda kuizungumzia barabara ya bypass ya kutoka Mretele kwenda Ruwiko ya Songea Mjini yenye urefu wa kilometa 11. Barabara hii imekuwa na msongamano mkubwa wa magari, bajaji na pikipiki. Imekuwa ni rabsha na ajali zimekuwa nyingi sana. Vilevile ni barabara ambayo ni ya muda mrefu sana; siku zote tumekuwa tukiambiwa upembuzi yakinifu, upembuzi yakinifu, jamani ni urefu wa kilometa 11. nikuombe Mheshimiwa Waziri funga macho, hebu nenda kajenge ile barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii niseme tu, huu ni mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba hakuna msongamano katikati ya miji. Tunaangalia katika Mji wa Iringa, hakuna msongamano, barabara ile kule chini inapita malori. Vile vile ukiangalia Mwanza na Dar es Salaam, hakuna msongamano wa malori.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nizungumzie barabara ya bypass; nimekwenda Mbeya tukiwa ziara na Wabunge, tukafika Mbeya…

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: …Taarifa amekataa Naibu Spika. Mnanipotezea muda bwana! (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tabasam.

T A A R I F A

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika... (Kicheko)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, anataka kukulisha maneno mdomoni huyu Mheshimiwa. Namshangaa anasema Mwanza hakuna msongamano; lini umetoka Mwanza wewe! Mwanza kuna msongamano wa kutisha kama Mbeya ilivyo na Dar es Salaam na Dodoma sasa hivi kuna msongamano. Majiji yote yana msongamano. Jiji huwezi kulinganisha na mkoa. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tabasam!

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Naam!

NAIBU SPIKA: Ngoja kwanza. Kaa tu. Waheshimiwa Wabunge, nadhani nilieleza jana wakati tunafunga Bunge hapa. Misongamano inatofautiana. Kuna msongamano wa magari kushindwa kupita kabisa kwa sababu ya utelezi, kuna msongamano unaoweza kusababishwa na mvua kama Dar es Salaam ambako wanahitaji mitaro. Kwa hiyo, misongamano inatofautiana. Nadhani tuelewane hapo. Mheshimiwa Mbunge ukiwa na hoja, huwezi kumwuliza Mbunge, yaani unakuwa unampa taarifa, usimuulize swali kwa sababu siyo kazi yake yeye kujibu.

Wewe unampa taarifa kwamba, unaanza ukisema, naomba kumpa taarifa kwamba Mwanza kuna msongamano barabara moja, mbili, tatu; moja, mbili, tatu. Huwezi kumwuliza swali kwamba wewe umepita lini; na msongamano upo? Mheshimiwa Jacqueline Msongozi, malizia mchango wako.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Tabasam hiyo siyo nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kama ifuatavyo. Mwezi wa Tatu, Wabunge…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Haya, muda wako umeisha Mheshimiwa, nakumbushwa hapa.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: …tulipata fursa ya kwenda Mbeya…

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: …na nilikuta kule kuna msongamano wa hatari sana. Kilometa 48.9 kutoka Uyole kwenda Songwe, sasa mimi niombe…

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, Mheshimiwa Jacqueline.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Naunga mkono hoja. (Makofi/Kicheko)