Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Abeid Ighondo Ramadhani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili nizungumzie changamoto za barabara zilizopo katika Jimbo langu la Singida Kaskazini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu muda ni mchache, itifaki ya shukrani na pongezi naomba izingatiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda moja kwa moja kwenye mchango wangu, nizungumzie barabara mbili, tatu, ambazo ni muhimu kwelikweli kwa maisha na uchumi wa wananchi wa Singida Kaskazini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na barabara hii ya kutoka Singida – Haydom kupitia Mji mdogo wa Ilongero ambao ndiyo Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya na inapita katika Mji mdogo wa Mtinko na Kata ya Modeda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni ahadi toka Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi. Nakumbuka wakati huo niko darasa la tatu, mzee Mwinyi alikuja pale Ilongero akaombwa barabara hii akaahidi akasema nitaijenga. Amemaliza amekuja aliyefuata mzee Mkapa naye alifika Ilongero pale akaahidi hii barabara, lakini hakuna kilichofanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi wakati tunaomba kura, Rais, Hayati Dkt. Magufuli, alifika Singida Mjini na akaahidi hii barabara. Kama haitoshi, Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, alifika Ilongero na akaahidi kwamba hii barabara tunaijenga kwa kiwango cha lami. Na kwa matokeo hayo kura zilipigwa nyingi kwelikweli kwa CCM.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ighondo, kuna taarifa; Mheshimiwa Kuchauka.

T A A R I F A

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninampa taarifa mzungumzaji kwamba pamoja na Waziri Mkuu kutoa hiyo ahadi, lakini Waziri Mkuu kwenye Jimbo lake kuna barabara tatu zote hazifikiki, kwa maana ya kwamba Liwale – Ruangwa, Nachingwea – Ruangwa na Nanganga – Ruangwa; zote hazifikiki kwa lami.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, kwa sababu ya muda mfupi ambao kila Mbunge anao wa kuchangia tujitahidi taarifa tunazozitoa basi ziwe za kumuongezea kile anachochangia; Mheshimiwa Ighondo, malizia mchango wako.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na masikitiko hayo ambayo nimeyaeleza naomba basi hii barabara sasa itengenezwe kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa uchache kwamba angalau imeonekana kwenye hotuba ya Waziri, ukurasa wa 42, kwamba inakwenda kufanyiwa upembuzi yakinifu. Basi niombe sana kwa heshima na taadhima, nitaongea kwa lugha ya upole sana leo, sitafanya sarakasi kama alivyosema Mheshimiwa Flatei, lakini ninaomba hii barabara itengenezwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, na hizi fedha kwanza ni kidogo, niliona ni shilingi milioni 100, milioni 100 kwa kilometa 93 kusema kweli siyo haki, siyo sawa hata kidogo. Barabara ambayo imeahidiwa na viongozi wote wa Kitaifa tangu uhuru mpaka leo tunaipa kamilioni 100, hili kwa kweli naomba litazamwe na ninamuomba Waziri nitaishika shilingi yako hapa; ongeza fedha hapa, fedha ziongezeke kwenye eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza barabara hii inakwenda Makao Makuu ya wilaya, lakini pili, ndiyo roho ya uchumi wa Wanasingida Kaskazini; vitunguu, mafuta ya alizeti mnayoona, asali na maziwa yote, hii barabara ndiyo roho ya uchumi wao. Niombe Mheshimiwa Waziri utakapokuja hapa nipe majibu sahihi, vinginevyo hatutaelewana hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo barabara nyingine ya Ilongero – Ikhanoda – Ngamu; hii barabara iliua. Kuna daraja pale la mchepuko, maji yalizidi baada ya mvua kunyesha yakafunika daraja likajengwa daraja la dharura, daraja lile liliua mtu, sasa naomba daraja hili na lenyewe lijengwe. Tuhakikishe linainuliwa ili kuepusha vifo vinavyotokea kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ile ambayo niliisema kwenye swali la nyongeza ya Singida – Kinyeto – Sagara ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais aliyeko madarakani. Naomba hii barabara nayo ijengwe kwa kiwango cha lami.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hoja lakini Kiwanja cha Ndege cha Singida hakionekani kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, naomba na chenyewe akisimama akisemee. (Makofi)