Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii nami nichangie kwenye hoja iliyopo mbele yetu. Nataka kuanza kwa kushukuru Chama changu cha Mapinduzi, kwa mara ya kwanza kutambua umuhimu wa barabara ya Mabokweni - Maramba, Mtoni Bombo kuelekea Korongwe halikadhalika kuelekea Umba Junction mpaka Same, kwamba kwa mara ya kwanza barabara hii sasa imeingia kwenye Ilani ya uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, licha ya kuingia kwenye Ilani ya uchaguzi, kwa masikitiko makubwa, bajeti hii imeisahau barabara hii. Barabara hii nimeizungumzia kwa miaka 10 mfululizo tukipewa ahadi barabaraba itajengwa. Tukipewa ahadi kipindi fulani kwamba barabara hii sasa itajengwa kwa kupitia MCC, mpango ule ukayeyuka. Akaja ndugu yangu Mheshimiwa Kwandikwa mwaka 2019 akaahidi kwamba bajeti ijayo tutaiingiza kwenye mpango wa kufanya feasibility study, halikutokea na hata leo halikutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii imeahidiwa na Mheshimiwa Benjamini Wiliam Mkapa, Marehemu, haikutokea; barabara hii akaiahidi Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, hakutokea; barabara hii amehiahidi Mheshimiwa Hayati Dkt. Magufuli, haipo hata kwenye feasibility study; barabara hii walizungumzia viongozi wetu wa dini wakubwa wa nchi hii; Shehe Mkuu ameizungumzia barabara hii na alipewa ahadi na Mheshimiwa Rais pale Korongwe mwaka 2020, haijatokea; Askofu Mkuu wa Anglikana wa nchi hii ameizungumzia barabara hii, akaahidiwa itajengwa, haijajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama mmepuuza maneno ya Kitandula, basi hata ya hawa viongozi mnayapuuza! Hivi mwambiwe na nani ili mwelewe? Sisi watu wa Mkinga tunasikitika sana na jambo hili; na ninataka niweke rekodi sawa hapa, kuna maneno huwa yanasemwa hapa, kwamba watu wa Kaskazini walipendelewa; jamani, Mkinga hatuna barabara, Tanga hatuna barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Mkinga tuna kilometa zisizozidi 25 za lami na hizi zinakwenda kule Horohoro kwenye boarder yetu na Kenya. Hazikwenda kwenye maeneo ya uzalishaji. Hebu tutendeeni haki, njooni mtusaidie kujenga barabara hii ya kutoka Mabokweni – Maramba - Mtoni Bombo - Mashewa kwenda Korongwe, vile vile tuiunganishe na barabara hii ya kwenda Umba Junction mpaka Same. Hivi ni kwa nini kwa upande ule wa Same feasibility study imekamilika, lakini huku kuna kigugumizi? Tunaomba maelezo, Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja hii, atupe maelezo ya kina, vinginevyo hakitaeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna barabara iliyoanza kujengwa ya kwenda Makao Makuu ya Wilaya, kichekesho ni kwamba tunajenga mita 200, mita 150; barabara ya kilomita 28 tunajenga mita 200, hivi tutamaliza lini? Naiomba Serikali ifikirie mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)