Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi. Nina mambo matatu. Najua muda siyo mrefu sana, dakika ni chache; dakika tano siyo nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niweze kutoa mawazo yangu kwenye wizara hii. Moja, nawaomba watu wa ujenzi; ujenzi wa viwanja vya ndege wapewe watu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege wajenge wenyewe. Kazi ambayo wanafanya sasa hivi TANROAD ni ujenzi wa viwanja vya ndege wakati kazi hiyo inaweza kufanywa na watu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege. Naomba Wizara ilichukuwe hili na ifanye mabadiliko. Kama kuna maboresho, wafanye maboresho lakini bajeti ipelekwe na isimamiwe na watu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege. Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nawaomba watu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, katika wind-up mtuambie, kwa sababu kuna maombi ya kuundwa kwa Bodi ya Wataalamu ya Usafirishaji. Kuwepo na bodi hii ili iweze kusimamia masuala yoyote ya uchukuzi na usafirishaji ndani ya nchi yetu. Juzi nimemwona Mheshimiwa Waziri Mkuu ameenda kukagua DART. Msimamizi wa DART anatoka Ujenzi; watu wanaotoka uchukuzi, hawaendi kusimamia masuala yao. Huwezi kupata performance. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba watu wa Ujenzi na Uchukuzi; DART na mambo yote ya uchukuzi, tunacho Chuo cha Usafirishaji, kinatoa wataalam, tuwatumie wataalamu hao. Haiwezekani masuala ya usafirishaji mchukue watu wa ujenzi wakasimamie fani ya usafirishaji, haiwezekani, mbadilishe. Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi chukuwa wataalam kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji wakasimamie kazi hizi za DART na bandari na maeneo menginge ili kuleta ufanisi katika kazi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naomba watu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, naipongeza kamati ya Ujenzi na Uchukuzi wamezungumzia ahadi za viongozi wetu wa Kitaifa. Wakati wa kampeni yam waka 2015, Mheshimiwa Rais, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alisimama Ziba akatuahidi barabara ya lami. Mwaka 2020 amesimama tena, ameahidi barabara ya lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwenye Ilani ya Chama chetu cha Mapinduzi, imeandikwa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Ziba - Choma, Ziba – Nkinga - Ndala mpaka Puge; ili ujenzi huu uanze, lazima muweke bajeti. Hamuwezi kujenga bila kuweka bajeti ya feasibility study. Naomba tuweke bajeti. Niliwahi kukutana na Mkurugenzi wa TANROAD, Mheshimiwa Eng. Mfugale akatuambia suala hilo la feasibility study litafanywa na watu wa Mkoa. Leo ni mwaka wa tatu toka atoe maelekezo kwamba watatenga fedha watu wa mkoa waweze kufanya study hiyo. Study haijafanyika na katika bajeti hii sijaona study. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri amesema mkoa wanapata fedha za kuweza kufanya feasibility study; nakuomba sasa katika wind-up utoe maelekezo study hiyo ifanyike kwa sababu barabara hiyo ni muhimu na ikizingatiwa barabara hiyo inaunganisha Mkoa wa Tabora na Shinyanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hiyo ina hospitali kubwa mbili, kila siku tunaeleza; tuna Hospitali ya Rufaa ya Nkinga ambayo inahudumu ndani ya Mikoa zaidi mitatu; Tabora, Shinyanga, Kigoma pamoja na Katavi na Singida, wanaletwa pale, wanatoka kule kote wanakuja kwa lami, wakifika pale wanatumia vumbi. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri lichukuwe hili na katika wind-up tunataka tuone ukitoa maelekezo ya barabara hiyo ya lami.


Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa muda wako.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, atafuatiwa na Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo na Mheshimiwa Mathayo Manyinyi ajiandae.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante.