Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nitaanza na suala la TAZARA. Toka waasisi wa nchi yetu na nchi ya Zambia waunde TAZARA ni zaidi ya miaka 46 sasa. Waliunda kwa Sheria Na. 23 ya mwaka 1975.

Mheshimiwa Naibu Spika, TAZARA imekuwa na matatizo ya kifedha kwa muda mrefu sana. Imeshindwa hata wakati mwingine kutoa mishahara na kwa wanaostaafu kwa wakati. Ninaiomba Serikali iweze kuwekeza fedha zake kwa watu wa TAZARA ili iweze kujiendesha. Tunajua kabisa TAZARA – na kama ulivyosema hapo awali, inasaidia Nyanda za Juu Kusini ambao sisi ndio tunaozalisha mali nyingi, na hasa chakula katika Taifa hili. Sasa tukiwekeza kwenye reli hii itasaidia sana upatikanaji wa chakula hata kwa Dar es Salaam na kwenda huko huko Zambia ambako tunapeleka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, natoa ushauri; kwa sasa tunajua kabisa barabara zetu zinaharibika kwa sababu ya shaba inayobeba toka Zambia kuja kwenye Bandari ya Dar es Salaam. Sasa iwekwe sheria kama ikibidi, watu wa Zambia wapitishe shaba hiyo kwa kutumia reli hii ili iweze kupata fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, si hivyo tu, wenzetu wa TAZARA ya Zambia wameacha na kuweka nguvu zaidi kwenye reli hii, wametuachia sisi wenyewe. Hivyo basi, tunaomba tuisaidie reli hii iweze kufanikiwa na hasa kupata fedha ya kulipa mishahara na kujiendesha mpaka hapo itakaposimama yenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua TAZARA ina majengo katika stesheni zote, ina majengo pale TAZARA Makao Makuu, lakini bado wanashindwa hata kuweza kuitengeneza. Tunahitaji tuipatie fedha zaidi. Kama tuna miradi mipya ya SGR tumeanzisha, tunaweza tukawekeza katika TAZARA nayo ikaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie TANROADS. Kwenye ripoti ya CAG; wamesema TANROADS ilishindwa kutoza tozo ambayo ilikuwa ni zaidi ya shilingi bilioni tano kwa watu wa Sanzali ambayo ilikuwa ni barabara ya kilometa 50. Sasa hili ni tatizo. Kama tunashindwa kufanya tozo, tunawezaje kupata mapato kama Taifa? Kwa hiyo, nawakumbusha watu wa TANROADS kuwa makini kusimamia shughuli ambazo tunawapatia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Daraja la Kigogo na Busisi lilianzishwa kabla ya cheti cha kuangalia madhara ya kimazingira. Walianza ujenzi kabla ya kupata kile cheti. Tunawaomba sana wasifanye chochote mpaka wawe wametimiza haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado tumezungumzia daraja lile la Jangwani, bado mpaka leo hii wanasema kwamba wanaendelea kuangalia upembuzi yakinifu na mambo kama hayo. Tunaomba wafanye haraka ili Jangwani isiendelee kuzama na watu waendelee.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado kuna shida ya pesa ya maendeleo. Tunapitisha sisi kama Bunge, tunasema tunatoa fedha hizi, lakini mwisho wa siku bado fedha hizo haziendi kwenye Wizara husika. Leo hii Kamati imetoa maoni pale, kwamba miezi minne imebaki fedha ziwe zimekwisha, lakini bado hawajaletewa fedha zote. Tumeona nyingine ni asilimia 30, nyingine asilimia 50; hatuwezi kufanikiwa kama hatutoi fedha na maendeleo yakaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba ujenzi wa viwanja vya ndege vile vya kimkakati. Kwa mfano, Viwanja vya Ndege vya Songwe, Moshi, Manyara na Iringa, hivi vimewekwa kwa ajili ya utalii, lakini bado havijaanza kuwekewa mkazo wa kujengewa pale. Tukija Uwanja wa Ndege wa Songwe, mpaka leo taa hazipo kwa hiyo, ndege haiwezi kuondoka usiku. Kwa hiyo, tunaomba waziweke hizo taa, maana ni muda mrefu tumekuwa tukilizingumzia suala hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, madeni ya wananchi ambao wamepisha ujenzi wa viwanja vya ndege, tunaomba walipwe kwa wakati. Tunaomba tafadhali kwa sababu wananchi wanajitolea kwa ajili ya kuweza kusaidia maendeleo ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia barabara za mikoa zinazounganisha vipaumbele kwa ajili ya maendeleo mbalimbali, kwa mfano, Kyela kuna barabara ambayo inaunganisha Kyela na Ileje, ile ni barabara muhimu sana. Tunafahamu Ileje kwa kupitia Mbeya ni mbali lakini wakijenga ile barabara ya Ileje kuelekea Kyela itatusaidia sana kufanya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado ninajua kwamba kuna shida ya vibali TRA. Pale barabara zinapojengwa TRA wamekuwa wakichelewa kutoa ule msamaha wa kodi na hiyo husababisha barabara zinapojengwa zinakuwa zinachelewa na kuleta deni kwenye Serikali yetu. Ninaomba waweze kusimamia hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninaomba niishie hapo na huo ndiyo mchango wangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)