Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Anatropia Lwehikila Theonest

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nitaongelea maeneo matatu kama muda wangu ukiniruhusu. Kwanza, nitaongelea tathmini ya upatikanaji wa fedha lakini na uendelezaji wa habari ya maji. Pili, nitaongelea bajeti iliyoletwa kwenye Halmashauri ya Kyerwa lakini pia na tathimini ya CAG kuhusiana na utendaji lakini na mikataba mbalimbali ambayo imekuwa ikitekelezwa kwenye miradi ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, niseme bajeti imekuwa haiendi na haitoshi. Wabunge kadhaa wamesema utekelezaji wa bajeti ya maendeleo umekuwa ni asilimia 53 ambayo ni ndogo. Nisisahau kusema Mheshimiwa Waziri na Naibu wako mnafanya kazi nzuri sana lakini kazi mnayoifanya isipokuwa na fedha inakuwa ina matunda au tija ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mdogo tu ukiangalia kwa takwimu mlizoweka kwenye kitabu chenu mmesema katika mwaka wa wa fedha 2019/2020 mmeweza kuongeza tija katika upatikanaji wa maji vijijini kwa asilimia 2.3 ina maana kutoka kwa asilimia 70.1 hadi asilimia 72 point something ambayo naona kwamba ni tofauti ya asilimia 2 tu. Pia upatikanaji wa maji mjini kutoka asilimia 84 mpaka asilimia 86 unaona kwamba ni asilimia 2 tu. Kwa hiyo, kazi kubwa mnayoifanya ni asilimia 2 tu bado ni ndogo sana. Hata hivyo, mngefanya nini kama hamna fedha au bajeti? Nadhani sasa ni kazi ya Serikali kuhakikisha kwamba inapeleka fedha ya kutosha, hata kama bajeti tunayotenga Bungeni ni ndogo basi iende lakini inavyokwenda kwa asilimia 52, 53 hata kutokee maajabu hakuna kitakachofanyika. Hiyo hoja yangu ya kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ya pili ambayo nataka niongelee, kuna msemo amesema Mhindi mmoja anaitwa Rajendra Singh amesema vita ya tatu ya dunia itatokana na kukosekana kwa maji na wanavyochangia Wabunge hapa inaonyesha Dhahiri. Vita siyo lazima ushike bunduki lakini ukiona kila sehemu kuna changamoto ya maji ujue tayari hiyo ni vita. Kwa hiyo, naomba sana Serikali itoe kipaumbele kuhakikisha kwamba fedha zinakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sio tu fedha kwenda na hiyo ninaingia kwenye sehemu yangu ya tatu, CAG ameainisha changamoto nyingi sana katika miradi ya maji, muda hautoshi ningeweza kuwaeleza. Kwa uchache mikataba haitekelezwi inavyostahili na fedha zinakwenda lakini hakuna usimamizi unaofaa. Naomba Mheshimiwa Waziri utupe majibu ya ripoti ya CAG alivyoeleza changamoto hasa kwenye masuala mazima ya tendering kwamba michakato inakuwa haiendi sawasawa ndiyo maana fedha inapotea na ndiyo maana hatuoni tija katika uwekezaji wa maji. Nitakuomba Mheshimiwa Waziri uweze kuongelea suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sio hiyo tu katika bajeti iliyopita mlipanga kutekeleza miradi 1,116 imetekelezwa miradi takribani 355 ambayo ni sawasawa na asilimia 30 yaani kama tunaogelea pale pale. Hapa nirudi kwenye miradi sasa inayokuja kutekelezwa katika Halmashauri yangu ya Kyerwa. Nimekuwa nikieleza mara nyingi na Mheshimiwa Waziri nimekuwa nikikutumia picha za changamoto za maji za Kyerwa, tuna maji kwa asilimia 50 tu, zaidi ya watu asilimia 50 hawana maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Kyerwa tuna vyanzo vya maji vya kutosha na chanzo kikubwa cha maji ambapo nimewasikia wenzangu wanaongelea huko kwao Rukwa sisi kwetu tuna chanzo kikubwa cha maji ambacho ni Mto Kagera na kata zote zinazozunguka mto huu hazina maji. Nimeona mmeweka kwenye bajeti Kata za Mrongo, Bugomora, Kibale, Businde, Bugara zina changamoto ya maji lakini ni kata zinazopakana na Mto Kagera. Fedha iliyotengwa hapa, muda hautoshi ningeweza kusoma ni ndogo mtakuwa tu mnazibaziba tu viraka. Tunaomba utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji tuweze kutibu changamoto ya maji Wilaya ya Kyerwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sio hiyo tu watu wa Kyerwa hawatanielewa nisipoongelea changamoto ya Kata ya Kikukuru, kule tangu Uhuru hawajawahi kuona bomba la maji. Kata hiyo ina wakazi zaidi ya 17,000, kwa hiyo, ni kata kubwa sana ambapo lazima Serikali iweze kusikiliza na kupeleka miradi ya maji. Hata kama haina fedha za kutosha basi chimba visima at least kwa wakati huo ambapo tunasubiria miradi mikubwa watu waweze kupata maji. Bajeti ya shilingi bilioni 3 iliyotengwa kwa ajili ya Kyerwa nisema ukweli hiyo ni ndogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, muda wangu ni mchache lakini Kata ya Songambele pia ndiyo picha zile nilizokutumia, watu wanakunywa maji na ng’ombe. Kuna Kata ya Rwabwere sehemu inaitwa Mkijugwangoma hawajawahi kuona maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)