Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Vincent Paul Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwanza nitampongeza kidogo sana Mheshimiwa Aweso kwa sababu, katika hotuba yake jimbo langu halijaguswa, limeguswa kidogo kuna ukakasi. Ma-engineer ndani ya Wilaya ya Nkansi wako wawili, tena ni technicians, engineer hakuna. Kwa hiyo, Wilaya ya Nkansi nzima suala la maji ni sifuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna ahadi alizotoa Mheshimiwa Hayati pamoja na Mheshimiwa Samia Suluhu. Katika mji mdogo ambao katika jimbo langu ndio mji ambao najisifia ulitakiwa kuwe na mradi wa mabwawa ambayo yanaweza kuhudumia vijiji vitatu hadi vinne, lakini kwenye hotuba yake hayapo. Na hii nadhani kutokana na kwasababu, kule wilayani engineer wa maji hamna kwa hiyo, hapati taarifa sahihi. Kwa hiyo, nakuomba Mheshimiwa Aweso njoo uokoe Jimbo la Nkansi Kusini maji ni hoi, hakuna maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Nkansi Kusini nina kata tatu hawajawahi kuona maji ya bomba kila siku ni vifo vya mamba na magonjwa ya tumbo basi. Kwa hiyo, Mbunge nimebaki gari langu ndio ambulance kubebea watu kupeleka hospitali magonjwa ya tumbo na vifo vya mamba, wanaliwa na mamba. Mheshimiwa Aweso baada ya kumaliza Bunge nakuomba hairisha ziara nyingine zote za majimbo, Nkansi Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu, nimeona Wabunge wengi wamechangia humu, kwanza nawashangaa, wengine matenki mabovu, wengine miundombinu chakavu, mimi hakuna miundombinu, hakuna matenki. Kwa hiyo, nakuomba baada ya Bunge mara ya kwanza Nkansi Kusini, ingia Ninde, ingia Kate, ingia Wampembe, utakuja na taarifa kamili. Kule wananchi wanajihesabu kama wako Kongo. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Naibu Spika, huduma ya wananchi ya maji hawajaifurahia nchi yao wananipigia simu wanalalamika wamesahaulika. Mheshimiwa Aweso, Wizara ya Maji, Nkansi Kusini anza nako kule ndio iwe kama sample nakuomba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vipo vijiji ambavyo viko mwambao kule mwa Ziwa Tanganyika hakuna miundombinu. Watu wanasema hapa wanakunywa maji na mifugo kule wanakunywa maji na nguruwe pori. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanasema wana maji mekundu kule wana tope, wanatumia maji machafu, yaani ni shida Wilaya ya Nkansi Kusini. Mheshimiwa Aweso njoo ukomboe Nkansi Kusini upande wa maji, anza na mabwawa ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, njoo uanze na visima. Nakushukuru umeweka visima kidogo, lakini bado asilimia ni ndogo mno. Ipo miradi iliyotelekezwa wameweka tu mabomba ya maji pale mipira hamna miaka, ukiuliza ina miaka nane, mengine mabomba yana miaka saba, yana miaka tisa, ni shida. Maliza bajeti yako Nkansi Kusini moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, yapo majimbo au vijiji ambavyo kama Mbunge wa Wilaya, naongea Wilaya ya Nkansi kwa ujumla kwasababu, ndio Mbunge wa Chama Cha Mapinduzi na ndio chama tawala ambacho naamini ndio kinacholeta maji, ndio kinacholeta huduma ya mabomba kila maeneo kwa Wilaya ya Nkansi jumla. Kwa hiyo, Mheshimiwa Aweso…

MHE. AIDA J. KHENANI: Taarifa. Mheshimiwa Naibu Spika,

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Vincent Mbogo kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Aida Khenani.

MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ndio naipokea Mbunge wangu pacha. (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Ukae kwanza yeye azungumze. Ahsante. Mheshimiwa Aida Khenani.

MHE. AIDA J. KHENANI: Taarifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa Taarifa kaka yangu, pacha wangu anayetoka Nkansi Kusini kwamba, Wilaya ya Nkansi ina Majimbo mawili Nkansi Kusini anakochangia yeye ambako ndio anatoka, lakini Nkansi Kaskazini Mbunge wake aliyechaguliwa na wananchi anatoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Vincent Mbogo unaipokea Taarifa hiyo.

MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei kwasababu, hawana Serikali. Na hata huduma ninazoongea hizi kinacholeta ni Chama Cha Mapinduzi kwa hiyo… (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eeh, kengele imegonga?

MBUNGE FULANI: Bado.

MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, aah, naunga mkono hoja. Ahsante sana na Mbunge wangu pacha, asante sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Asante sana. Taarifa iliwekwa kwa namna ya kuweka mambo sawasawa, lakini wakati ukizungumza Mheshimiwa Vincent Mbogo ulieleza zile kata tatu ambazo hazina miradi ya maji yoyote na ukasema kama wako Kongo. Sasa kwa sababu, ulikuwa unaeleza jambo ambalo wananchi wana hali mbaya nalo na haturuhusiwi kutumia michango ya nchi nyingine, unaweza kuitumia humu ndani ile ambayo inafanya vizuri unataka nchi yetu iige huko. Lakini ile ya kuonesha kwamba, pengine kuna hali fulani hivi ambayo haiku sawasawa hairuhusiwi. Kwa hiyo, ifute hiyo kama wako Kongo halafu tuendelee na mchangiaji mwingine.

MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naifuta hiyo kauli, wako Tanzania. (Makofi/Kicheko)