Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Ajali Rashid Akibar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Newala Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nachukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi hii, kuchangia katika hoja ya viwanda na biashara. Pili, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniweka hai mpaka leo kwamba nimepata nafasi ya kuweza kumshukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kuchangia kwangu ni mara ya kwanza, naomba kuchukua nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Newala, kama wanayofanya wenzangu, kumsifu Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa kuchaguliwa kwake kwa kura nyingi na kazi anazozifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nampongeza Rais wa Zanzibar, ndugu yetu Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda vile vile kuwasifu Waheshimiwa Mawaziri ambao wameteuliwa ambao kwa kweli uchapaji wao wa kazi unaendana na hali halisi tuliyonayo Tanzania sasa hivi. Maana Tanzania ya leo tulikuwa tunahitaji viongozi wa design hii, maana tulishafikia mahali pabaya sana ambapo wananchi walikuwa wamekosa imani na Serikali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijikite katika mchango wangu kwa Wilaya ya Newala. Wilaya ya Newala inalima korosho takribani tani 80,000 hadi 70,000 wakati korosho ambazo tunasafirisha nje zinakuwa ni tani 150,000. Kwa hiyo, karibu nusu ya korosho ambazo zinasafirishwa zinatoka Newala na Tandahimba.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Newala tuna viwanda viwili vya kuchakata korosho. Kuna kiwanda kimoja au viwili vyote tulikuwa tumepata kwa mkopo wa Benki ya Dunia ambao naamini mpaka leo tunalipa zile fedha nyingi sana. Vile viwanda vilifanya kazi takriban kwa miaka miwili tu. Hivyo viwanda vikawa vimesimama, haviendelei tena kufanya kazi. Kwa hiyo, nashindwa kuelewa, kama viwanda viwili vipo na tunazalisha korosho zaidi ya tani 70,000, kinachofanyika ni nini? Kwa sababu kinachofanyika hapo unaona kwamba watu ambao wanazalisha korosho wapo, maana yake product zipo na vile viwanda vipo, tatizo ni nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, inavyoonyesha ni kwamba hapa tatizo labda ni management. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri aje atueleze hapa, kwamba uchakataji wa korosho katika Wilaya ya Newala utaanza lini? Sambamba na Wilaya ya Newala, kuna viwanda vingine kwa mfano vya Mtama, Likombe pale Lindi, Mtama viwanda vyote hivyo vimesimama na hawa watu wanazalisha korosho, ni kitu gani kinachofanya kwamba tusiendelee kuchakata hizi korosho?
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunaingia katika mchakato mwingine wa kujenga viwanda vingine vya pili. Kwa nini tunaendelea kujenga viwanda vingine wakati vile ambavyo Mwalimu Nyerere alikuwa amevijenga tunashindwa kuvisimamia na kuchakata korosho? Ni kitu gani kinachofanyika? Kama kweli tumeshindwa, basi tunge-hire management.
Mheshimiwa Naibu Spika, inavyoonyesha ni kwamba sisi tunashindwa kuzalisha, basi tukodi management ili hivi viwanda vianze kufanya kazi. Ukiangalia kiundani, utaona kabisa kwamba hivi viwanda vyote vinatumika kama maghala leo. Wengine wameondoa mashine zile, wameuza au wamekata chuma chakavu. Sasa Mheshimiwa hapo nashindwa, tutaendaje kwenye hivyo viwanda vingine vya kisasa?
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo kama haitoshi, kuna wananchi wangu pale wa Newala baada ya kuona kwamba hizi korosho sasa hazichakatwi tena, wale akinamama wameanzisha vikundi vidogo vidogo ambavyo kwa kweli sasa wanachakata kwa kutumia mikono yao; lakini zile korosho ndiyo korosho ambazo ni nzuri in the world, lakini sasa zinapatikana kwa kiasi kidogo. Watu wa nje wanakuja wanataka zile korosho, lakini zinakuwa ni kiasi kidogo kwa sababu ile process wanayoitumia kuchakata inakuwa ni finyu kwa kuwa wanatumia mikono.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atueleze kwamba ana mkakati gani? Kama vile viwanda ameshindwa kuviendesha, je, anawezeshaje akinamama ili waweze kuchakata korosho kwa wingi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, pale Nachingwea kuna kiwanda kikubwa sana cha kuchakata ufuta, alizeti pamoja na karanga. Sasa sisi tunalima ufuta kule, ule ufuta unalimwa kwa kiasi kikubwa sana; ni kitu gani ambacho kinazuia tusichakate ufuta tukapata mafuta ambayo ni the best in the world? Maana inasemekana kwamba mafuta ya ufuta hata wale ambao wanasumbuliwa na pressure iwe ya kushuka au kupanda, ukiyatumia kwa muda mrefu inasaidia kuweka afya yako kuwa nzuri. Kwa nini tusiendelee au tusifufue kiwanda hiki tukawa na process tena ya kuchakata huu ufuta au alizeti? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Farm Seventeen pale, kwa wale ambao labda hawajafika Nachingwea, kuna Farm Seventeen, Farm Twenty One, yale yalikuwa ni mashamba ya Wajerumani ambao walikuwa wanalima karanga. Sasa Mheshimiwa Waziri aje atuambie, kama kile kiwanda kipo na yale mashamba yapo, ana mpango gani wa kutafuta watu? Maana wale Wajerumani walilima karanga pale, japokuwa wao walikosa time, lakini leo Jeshi la Wananchi wanatumia eneo lile kwa ajili ya mazoezi. Yale yalikuwa ni mashamba kwa ajili ya karanga!
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri atueleze kwamba je, nchi yetu ina mpango gani wa kutumia yale mashamba kulima karanga ili tuweze kupata mafuta? Pia kile kiwanda kilichopo pale Nachingwea kuna mpango gani wa kufufuliwa badala ya kula mafuta mabovu mabovu ambayo tunaletewa kutoka nje? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa Diwani pale Kinondoni. Kwa hiyo, mchango huu ni wa Kitaifa. Kwa mfano, pale Ilala kuna Kiwanda cha Bulb. Kile Kiwanda cha Bulb kimefungwa! Leo tuna-import bulb kutoka nje, hivi hii siyo aibu kweli? Bulb za kuweka juu; kile kiwanda leo wanatumia watu wa TATA kwa ajili ya ghala la kuuzia magari. Ile mitambo yote imeng‟olewa. Hivi ni nani ambaye alichukuwa kile kiwanda na kwa nini ile mitambo iliondolewa? Kwa nini sasa badala ya kutengeneza bulb, watu wanatumia kama maghala ya kuuzia magari?
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na East Afrika Cables. Leo wana-import badala ya kutengeneza zile nyaya ambazo zilikuwa the best katika dunia hii kutegemeana na hali halisi ya Tanzania, kwa sababu wale ma-engineer walikuwa wanajua hali halisi ya Tanzania ikoje. Leo wana-import nyaya kutoka nje, kwa nini wameshindwa kutengeneza zile nyaya ndani, leo wana-import kutoka nje? Hivi ni vitu ambavyo nadhani Mheshimiwa Waziri ayaangalie kabla hajaingia katika viwanda vingine ambavyo anasema anaweza kuhamasisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi, utakuta viwanda zaidi ya 300 au 400 havifanyi kazi. Kwa nini hivi viwanda vimegeuzwa kama maghala? Kwa nini wasitafutwe wawekezaji ambao utawaambia kwamba mimi leo nina viwanda vya design fulani halafu wale wakaja ukawapa yale maghala wakaweka tu mitambo badala ya kuwatafutia ardhi ambayo haina chochote? Huoni kama huo utakuwa ni utendaji mzuri zaidi kuliko leo unaanza kutafuta ardhi lakini wale watu leo wana maghala na hayo maghala wanayatumia kwa kuhifadhia mali badala ya kuzalisha? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine katika TIC, yaani huu uwekezaji; uwekezaji should be epically ina maana kwamba huu uwekezaji maana yake lazima umnufaishe Mtanzania. Wawekezaji wengi wanapokuja hapa Tanzania, hawawanufaishi Watanzania, wao, wanaangalia rasilimali zao. Hamna nchi yoyote duniani ambapo unaweza uka-import vitu kutoka outside halafu hapa ndani ukaviuza vile vitu kwa dola. Kwa nini hawa wawekezaji zile rasilimali zao wanazozileta hapa ndani wanauziuza kwa dola? Hicho ndicho chanzo kikuu cha kushusha thamani shilingi yetu, kwa sababu sisi wenyewe tumeshaidharau fedha yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nenda India, China, nenda mpaka zile hospitali za Wilaya, haiwezekani wewe kule ukafika na dola wakakubali. Watakwambia kabadilishe upate fedha za nchi ile. Hata China, ni lazima ubadilishe zile fedha za Tanzania iwe ni dola, uibadilishe upate fedha ya nchi ile then uende ukanunue. Leo hapa tunaletewa magari ya TATA unauziwa in US Dollars. Maana yake exchange rate ya hayo magari yanabadilika kila siku kutegemeana na shilingi yetu inavyoshuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kama kweli tungekuwa tunauza kwa shilingi, basi zile gari ambazo zimeingia mwaka 2015, mwaka huu zisingeweza kupanda bei. Leo gari ambayo imeingia mwaka 2015 kwa dola fulani, labda exchange rate ilikuwa shilingi 1,200/=, mwaka huu kila siku unauziwa kwa rate ya leo; uone hapo fedha yetu inakosa thamani. Kwa hiyo, tuangalie kwamba Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji washirikiane na Mheshimiwa Waziri wa Fedha, waone ni namna gani tutakuwa na sheria za kuweza kudhibiti fedha yetu ikawa na thamani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.