Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti iliyoko mbele yetu ya Wizara yetu ya Maji. Nianze kwa kumpongeza sana Waziri pamoja na wasaidizi wake wote kwa kazi nzuri wanayofanya lakini kwa bajeti nzuri waliyotuwasilishia hapa mezani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme wazi kabisa Mheshimiwa Aweso toka akiwa Naibu Waziri wa Wizara hii ali-perform vizuri sana na ndiyo maana Mheshimiwa Rais akaamua kumpa Uwaziri kamili. Tuendelee kupongeza na niwatie moyo vijana wengine waendelee kuiga mfano wa aina ya Mawaziri kama akina Aweso, unafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kusema kwamba Ilani yetu ya Uchaguzi, ukurasa ule wa 7, Ibara ya 9(d)(i) inaeleza wazi kwamba katika miaka mitano tutaongeza nguvu katika upatikanaji wa maji vijijini na mijini. Katika taarifa yake aliyotusomea hapa kwa sasa kwa vijijini tumefikia asilimia 85 na kwa mijini tumefikia asilimia 95.

Mheshimwa Spika, kasi inatakiwa iendelee kuongezeka katika kuwekeza Zaidi, najua kazi kubwa imefanyika. Mimi nina ushahidi katika jimbo langu au Wilaya yetu ya Ikungi tuliweza kupata jumla ya shilingi bilioni 3.7 katika mwaka uliopita na hata sasa tumeangalia pale wametutengea fedha naona safari hii kidogo wametuminya sana kwa wilaya nzima kwa majimbo yote mawili tumepata shilingi bilioni 1.7. Kwa shida ya maji tuliyonayo katika wilaya yetu, bado tuko chini sana, naamini kunahitajika juhudi kubwa kuongeza fedha kwa ajili ya kuwekeza zaidi.

Mheshimiwa Spika, nipongeze kwamba katika shilingi bilioni mbili 2 ambazo tulipata tumeweza kupata maji katika Vijiji vya Kipumbuiko, Kinku pamoja na Lihwa, hivi


ninavyoongea wananchi wanapata maji. Hata hivyo, ndiyo kama wanavyosema wenyewe kwamba tuendelee kula mtori nyama iko chini basi tunaendelea kuamini kwamba katika muda ujao tutaendelea kupata zaidi kwa sababu Vijiji vile vya Mkunguwakiendo, Sakamwau navyo vitapata fedha kwa ajili ya kuongeza uwezekano wa upatikanaji wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu ni usimamizi wa miradi hii. Mradi hii tunawekeza fedha nyingi lakini tunaenda kuacha kwenye Kamati za Maji ambazo hazina uwezo kabisa wa kusimamia miradi. Unaenda kuwekeza zaidi ya shilingi milioni 700 kwenye mradi wa maji unakuta hawana uwezo kwa sababu hawana ujuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kumekuwa na upungufu mkubwa wa hawa mainjinia au ma-technician wanaosimamia miradi hii. Pia kumekuwa na urasimu, unakuta huyohuyo injinia au technician anaagizwa aje asaidie wananchi mradi, unaende pale wanaomba hela ya mafuta na kadhalika, ucheleweshaji ni mkubwa sana katika maeneo hayo. Kwa hiyo, unakuta mpaka wamefika mradi umeharibika kabisa. Kwa hiyo, niombe sana kufanyike marekebisho katika eneo hili. Kama tumewekeza fedha tujiandae kutunza miradi ambayo inapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini sheria iliyoanzisha Kamati za Maji ni jambo zuri la ushirikishaji lakini hawana uwezo, miradi mingi inakufa. Tunaweza kusema kwamba wanajipange kutengeneza koki tu lakini hata mhasibu tu hawana kwa sababu pale hakuna mtu mwenye professional ya accounts. Kuna mtu wa kawaida tu mama mmoja amewekwa pale ana mradi anausimamia wa shilingi bilioni 1 hana uwezo wa kuendesha mradi ule. Kwa hiyo, ombi langu kama Taifa tuangalie upya suala la usimamizi wa miradi ya maji ambayo tunawekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika eneo hili la Ikungi sisi tulikuwa tumeomba tuwe na Mamlaka ya Maji Mjini. Tunaamini tukiwa na Mamlaka hiyo itatusaidia sisi kuwa na uwezo wa upatikanaji wa fedha zingine. Mchakato ulianza miaka miwili iliyopita, Waziri utakapokuja hapa uniambie ni lini sasa tutapata Mamlaka ya Maji Mjini Ikungi ili isaidie kuongeza uwezo wa kupata fedha kwa ajili kuongeza miradi hii. Hii itasaidia sana kuongeza kasi ya usimamizi wa maji.

Mheshimiwa Spika, mfano kama Wilaya ya Ikungi leo tunapata maji asilimia 52 tu maana yake tuko chini hata lengo la Ilani, hii ilikuwa kiwango cha mwaka 2000 leo ndiyo sisi tunakitaja kile kieneo pale, asilimia 52 kwa wilaya nzima kwa majimbo yote mawili. Maana yake ni kwamba tuko nyumba sana hata miaka mitano ikiisha kama hatutafanya juhudi za makusudi hatuwezi kuvuka. Maji ni muhimu na hayana mbadala, huwezi kunywa kitu kingine badala ya maji.

Mheshimiwa Spika, nimuombe sana Waziri anapokuja kuhitimisha atuambie kuhusu suala hili. Tuna tatizo la maji katika Vijiji vya Ntuntu, Tunataru, Mboho, Mwaru, Mahambe, Choda, Manjaru, Tumaini na Matongo, Inang’ana. Haya maeneo yote watu wanashiriki kunywa maji pamoja na mifugo, hii ni hatari sana hata kwenye afya zao. Kwa sababu Mheshimiwa Rais ana mpango wa kutua akina mama ndoo kichwani niombe sana juhudi ziongezeke katika eneo hili ili tusaidiane kuwasaidia wananachi hawa waweze kupata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili yake ni kujenga mabwawa kwa ajili ya unyweshaji wa mifugo. Sisi kule ni wafugaji naomba tuongeze uwezo wa kuchimba mabwawa ili angalau yapunguze tatizo la maji katika maeneo yetu. Mabwawa haya yakichimbwa yatasaidia sana kupunguza tatizo la maji kwa ajili ya kufulia au kunywesha mifugo ili maji machache yanayopatika yawe kwa ajili ya kunywa tu. Hii itasaidia sana kuondoa tatizo la maji katika maeneo yetu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mtaturu.

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, vinginevyo nirudie tena kukushushukuru sana, Wizara inafanya kazi nzuri lakini tunaomba tuongeze bidii katika maeneo haya.