Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kipekee namshukuru Mungu wote kuwa hapa na pia nakupongeza kwa kuwa wa matokeo Result Oriented Speaker. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naona kuna kila sababu ya wote tulio hapa tumshukuru Mungu kuzaliwa Tanzania, nchi ambayo imezungukwa na vyanzo vya maji kila upande, tuna Lake Victoria, Lake Nyasa, Lake Tanganyika, kuna Bahari ya Hindi lakini katikati ya Tanzania yetu kuna mabwawa mengi ya maji, kuna maeneo mengi ya milima. Vyote hivyo ni vyanzo vya maji na sioni kwa nini Watanzania miaka nenda rudi tunalalamika hatuna maji hatuna maji. Niseme tu kwa kifupi maji tunayozungumzia hapa ni maji safi na salama na usafi wa mazingira kwa Watanzania wote.

Mheshimiwa Spika, miaka ya nyuma kwa wale ambao wana umri wangu au zaidi watoto walikuwa wanazaliwa wakikuwa wana meno ya brown, lakini sasa hivi kila mtanzania akikuchekea ana meno meupe kwa sababu maji hayo yametibiwa na Serikali yetu iliona ni vyema basi kupunguza ile fluoride ili watu wote wanywe maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna shida, wataalam wetu wako wapi pamoja na vyanzo vyote hivyo vya maji? Jangwani kwenyewe, mfano ukienda Dubai maji yapo, sasa Egypt maji yapo, sisi urafiki wetu na nchi hizo uko wapi? Kwa nini tulalamike maji, maji na tutenge Mifuko ya Maji kila wakati tuje, hapa tu-ring fence hela. Naiomba Wizara hii akiwemo Mheshimiwa Awesu, kijana anayependa kumtua mama ndoo kichwani na anayezungumza sana nchi hii haina ukame, tuone sasa tumefikia muafaka.

Mheshimiwa Spika, nianze kushukuru kwa ule Mradi wa Maji wa Mwanga, Same mpaka Korogwe ambao sasa ikifika Desemba kila mahali patakuwa na maji. Hata hivyo, niseme wazi, nimetokea Kilimanjaro ambako tuna mlima mzuri unaotiririsha maji, wengi wanapenda kuolewa Kilimanjaro au kuoa Kilimanjaro kwa ajili ya yale maji. Tatizo ni tambarare ya Kilimanjaro hatuna maji, ukienda Rundugai hakuna maji, tambarare yote hiyo. Tunaomba sasa Waziri wetu aje atembelee maeneo hayo ili pia naye atupe solution. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunazo success stories za Mamlaka ya Maji Safi na Salama, wewe ni shahidi ulikuwepo hapa miaka hiyo, mkipitisha Sheria za Mamlaka za Maji, tumeona kuna ushindani na tumeona mafanikio katika miji, maji ni salama, miji mingi tu ikiwemo Dar es Salaam, Moshi, Musoma kule Mara. Huko kote nilikozungumza hao Wakurugenzi walipita Moshi wakajifunza, wakaenda sasa kupeleka huo utaalam kwingine na unakunywa yale maji yakitoka kwenye bomba moja kwa moja.

Mheshimiwa Spika, niseme kwamba umefika wakati, baada ya kupunguza kiwango kikubwa cha yale magonjwa ya maji ikiwemo cholera (kipindupindu), sasa tuone kwamba ni haki na siyo ombi tena Wizara hii ya Maji ijue kwamba mwanamke anatakiwa afungue bomba la maji ndani ya nyumba yake na siyo kumtua tu ndoo na kuanza kubeba kwa mkono, hapana kila nyumba iwe na maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni wazi kwamba Wizara hii inapata hela nyingi sana na pia ina wakandarasi wazuri na kelele zinapigwa, lakini wewe ni shahidi kila anayesimama hapa anasema maji hayatoshi. Nataka atakapokuja kuhitimisha Waziri aseme, tumefikia kiwango gani siyo hiyo 95 kwa miji na 75 kwa vijiji tu, kwa sababu maji yote yanaanzia vijijini, hakuna maji yanayoanzia mjini kwa nini kule vijijini asiagize RUWASA kila kijiji yanapoanzia maji lile bomba litoe kwanza maji vijijini halafu ndiyo litoe mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hainiingiii akilini maji yanaanzia kwangu halafu wanaofaidi ni mjini, ina maana wale watu wa mjini ndiyo wanayajua maji na ijulikane kwamba maji hayana mbadala, huwezi kuchukua soda, ukachukua K-Vant au ukachukua kinywaji chochote ukafulia nguo wala kuoga, maji hayana mbadala kabisa, kiu ya maji ni ya maji na matumizi ya maji ni ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme pia Serikali itoe elimu; maji haya safi na salama yanatibiwa kwa hela nyingi sana, lakini maji hayo hayo utayakuta ndiyo yanayoosha magari, maji hayo hayo ndiyo yanafanya kazi za hovyo zile inamwagilia bustani na kadhalika. Kwa nini tusipige hatua maji ya kunywa na kupika yawe ni tofauti na maji ya matumizi mengine yawe ni tofauti. Wengi mmetoka nje kuna mabomba mawili bomba moja ni la kunywa tu lingine ni ya kuoga na mambo mengine yale yale yanazunguka na yanafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo linguine, naona wasomi wetu pia hawachangamshi akili vizuri. Kuna lile Mindu Dam Morogoro, limekuweko siku nyingi na lime-solve matatizo mengi, lakini ukija katika hii barabara kabla hujafika Kongwa pale Kibaigwa maji yanakata mpaka yanavunja barabara, kwa nini kusiwepo na Dam lingine likakinga maji hayo yanayotoka huku Simanjiro yakatengeneza Dam linguine, ina maana wazee wale wa zamani walikuwa na akili kuliko sisi? Wasomi hawa walikuwepo, kwa nini maji yaharibu barabara tu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.