Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia kidogo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kupongeza Baraza zima la Mawaziri na Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa wanayoifanya hasa kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa ni Tanzania ya Viwanda. Nawapongeza sana! Kwa namna ya pekee nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa kazi kubwa anayoifanya hasa kuhakikisha kwamba tunafikia azma ya kuwa na viwanda au kufikia uchumi wa viwanda katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema kwamba hatuwezi kufikia huo uchumi wa viwanda bila kufikiria Sekta ya Kilimo. Sekta ya Kilimo ndiyo sekta mama ambayo itatuwezesha sisi Watanzania kuingia kwenye uchumi wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua sote kwamba zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania ni wakulima, sasa huwezi kuiacha sekta hiyo ya kilimo ukaingia kuwekeza viwanda vya aina nyingine na ukataka kufika kwenye uchumi wa viwanda. Kwa hiyo, ni lazima tuitazame Sekta ya Kilimo, tufikirie kuwekeza kwenye viwanda vya kilimo. Historia inatuambia kabisa kwamba hata nchi zilizoendelea, tunafahamu wote nchi za Uingereza, Ujerumani na Marekani walianza kwanza na viwanda vya Sekta ya Kilimo; Agro Processing Industries ambavyo vilikuwa vinaongeza value ya mazao au thamani ya mazao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nasi Watanzania tukitaka twende huko kwenye uchumi wa viwanda ni lazima tuangalie wakulima wetu waweze kuwa na viwanda ambavyo vitaongeza thamani ya mazao yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukishakamilisha kuwa na viwanda vya uongezaji wa thamani ndipo hapo sasa hawa wakulima watahitaji zana mbalimbali, watahitaji magari ya kusafirishia, basi itafanya sasa kuwe na demand ya vitu vingine ambavyo hivyo sasa vitahitaji viwanda vya mechanical industries na baadaye tutaingia pengine kwenye Chemical Industries.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nami nasema kwamba, ni muhimu Waziri wetu wa Viwanda aanze sasa kuangalia maeneo hasa ya uzalishaji ili kuwavutia Wawekezaji ili waweze kuwekeza viwanda vya kuongeza thamani kwenye mazao yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiweza kuongeza thamani ya mazao, kwanza kabisa itatusaidia kutoa ajira kwa vijana wetu. Tunatambua vijana wengi wako huko vijijini na sasa hivi wanakimbilia mijini wakifikiria kutafuta kazi kwenye Maofisi au kwenye viwanda mbalimbali na wakifika huko wanakosa hizo ajira. Sasa tuanze kufikiria kuanzisha viwanda hivi vijijini ili vijana wetu wengi waweze kuajiriwa kwenye viwanda hivyo, wabaki kule na kufanya kazi ya uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapata changamoto moja kubwa; mimi natokea Jimbo la Lupembe ambapo tunazalisha chai, kahawa, tunazalisha mazao ya matunda, kama mananasi, ndizi, machungwa na matunda mengine mengi tu, lakini kule Lupembe mpaka sasa hivi wale wananchi hawawezi kuuza mazao yao vizuri kwa sababu ya tatizo moja na hata Wawekezaji hawapendi kuwekeza maeneo yale kwa sababu ya tatizo la miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika,kwa hiyo, lazima tunapofikiria uchumi wa kati, tunapofikiria uanzishwaji wa viwanda kama nilivyosema lazima tuhakikishe kwamba kwenye maeneo ya uzalishaji ambapo huko ndiko tunategemea kuanzisha viwanda, ni lazima miundombinu ya barabara, tuhakikishe kwamba tunakuwa na barabara nzuri ambazo zinapitika muda wote ili watakaowekeza waweze kusafirisha hizo bidhaa kirahisi zaidi na hatimaye kufikia soko au kufikia maeneo ambayo wanaweza wakaongeza thamani zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia lazima tufikirie kuwekeza kwenye umeme. Kwa hiyo, unaona hapo Wizara nyingi sana zinahusika. Ni lazima tuwe na umeme wa kutosha kwenye maeneo haya ili tuweze kuwavutia wawekezaji waweze kuwekeza kwenye maeneo haya ya uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, ni lazima tuwe na maji. Tukiwa na maji ya kutosha automatically tutavutia wawekezaji, kwa sababu naamini kwamba, siyo Serikali itakayokwenda kujenga viwanda, wanaojenga viwanda ni wawekezaji wa ndani na nje. Sasa hawa lazima kuwe kuna huduma hizi muhimu. Huduma za maji, umeme, lakini pia huduma za afya ni lazima ziwe za kutosha ili wawekezaji waweze kuwekeza kwenye maeneo ya vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ilivyo sasa kwenye maeneo mengi ya uzalishaji, watu hawapendi kwenda kuwekeza kwa sababu hizi huduma muhimu hazipo. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri, tunapotaka kuwekeza, ni lazima tufikirie mambo hayo muhimu na hasa tufikirie kuwekeza kwenye kilimo ambacho kwanza viwanda vyenyewe ni vya bei ndogo, ni rahisi kuwekeza, lakini pia vinaweza vikaajiri Watanzania wengi na katika sera yetu tumesema kwamba lazima tuanzishe viwanda, tuanzishe shughuli ambazo zitawaajiri vijana wengi kwenye sekta mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ili tuweze kupata uwekezaji mzuri na hatimaye uwekezaji ukawa na tija, ni lazima tufikirie maeneo ya kuwekeza, hasa maeneo yale ambayo kuna uzalishaji, maana tunaweza tukawekeza kama ilivyokuwa kwenye viwanda vile vya tumbaku, badala ya kuwekeza Songea na Tabora ambako tumbaku inazalishwa, vikawekezwa Morogoro. Hatimaye utakuta wakulima wanakata tamaa kwa sababu hawawezi kusafirisha mazao yao kuyaleta Morogoro. Kumbe viwanda hivi vingekuwa vimewekezwa sehemu zile ambazo wanazalisha, basi wakulima wangeweza kupata faida kubwa na wangehamasika kuzalisha hilo zao na hatimaye nchi kupata faida kubwa au uchumi wetu kuweza kukua kwa kuwa viwanda vimewekwa kwenye maeneo ya uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunapoweka viwanda kwenye maeneo ya uzalishaji tunawasaidia wakulima wetu kuweza kupata faida katika kilimo. Ilivyo sasa hivi wanaofaidika sio wakulima, wanaofaidika ni wale middlemen, wale watu wanaonunua mazao toka kwa wakulima na kwenda kuwauzia watu watu wenye viwanda.
Kwa hiyo, haiwasaidii wakulima kama tutawekeza viwanda vyetu mbali na kule wanakozalisha. Kwa hiyo, tuweke jirani na eneo la uzalishaji ili wakulima wetu waweze kuuza mazao yao na kupata faida na hatimaye Taifa lipate faida kupitia viwanda na ajira hizi ambazo tumewekeza kupitia viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nijaribu kuongelea suala la kodi. Mara nyingi kumekuwa na kodi nyingi sana kwenye mazao, hasa mazao ya biashara. Kwenye zao la chai, kahawa, tumbaku na pamba, kuna kodi nyingi au kuna utitiri wa kodi. Utakuta kodi za mazao haya hufika mpaka 20 nyingine mpaka 25 au 27. Sasa mwisho wa siku anayekuja kulipa hizi kodi zote ni mkulima. Kwa hiyo, utakuta kupitia hizi kodi, tunamnyonya huyu mkulima ambaye kwanza anapata shida sana kuzalisha hili zao na soko lake halina uhakika; sehemu ya kuuzia kwenye kiwanda, hakina uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho wa siku anauza zao lake; anauza chai yake, kahawa, pamba au tumbaku yake kwa bei ya chini kwa sababu ya kuwa na kodi nyingi. Kwa hiyo, tunapofikiria viwanda au uzalishaji ni lazima tufikirie pia na hizi kodi, tujaribu kuzipunguza ili angalau mkulima aweze kupata faida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusu wawekezaji wazawa. Mara nyingi tumekuwa tukiwavutia wawekezaji wa nje tunawasahau wazawa. Tunasahau kuwahamasisha wananchi wale wanaotaka kujiunga kwenye vikundi vidogo vidogo na kuanzisha viwanda au kuna maeneo mengine tayari kuna wakulima ambao wameonesha nia ya kuwekeza kwenye kilimo na kwenye viwanda, ni vizuri Serikali tuwe na utaratibu wa kuhakikisha kwamba tunawawezesha kwa kuwapa mikopo au kwa kuwasaidia kuweza kupata mikopo rahisi na kuweza kuwekeza kwenye viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kule kwangu kuna mkulima mmoja anataka kuwekeza kwenye kiwanda cha chai, kwenye processing industries, lakini anashindwa kupata utaratibu gani mzuri ili aweze kupata mkopo na hatimaye aweze kufungua kiwanda cha chai. Kwa hiyo, naomba tunapofikiria uwekezaji, tuwafikirie sana Watanzania wenzetu ambao wanataka kuwekeza kwenye viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Waziri wangu wa viwanda ajaribu kuhamasisha au kututafutia wawekezaji wengi kwenye mazao ya chai. Kule Lupembe tuna viwanda viwili tu na vile viwanda haviwezi kutosha, havikidhi mahitaji ya chai ya Lupembe. Lupembe tunazalisha chai nyingi na vile viwanda viwili haviwezi ku-process ile chai yote, matokeo yake chai nyingi zinamwagwa na wananchi wanapata hasara kubwa sana. Kwa hiyo, naomba, kama kutakuwa na mwekezaji wa kiwanda cha chai, tunaomba aje awekeze Lupembe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye matunda, nanasi na…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja.