Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Ndaisaba George Ruhoro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Ngara ninakushukuru kwa kunipatia fursa ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Maji. Kwa namna ya kipekee kabisa ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Maji, kaka yangu Juma Aweso; napenda kumpongeza Naibu Waziri, Mheshimiwa Maryprisca; napenda kumpongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Eng. Sanga kwa utendaji wao mkuu uliotukuka wa Wizara ya Maji. Kwa kweli tunawashukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa, napenda kuwashukuru viongozi hawa kwa kuridhia kuidhinisha shilingi milioni 500 kwa ajili ya kujenga Mradi wa Maji wa Ngara Mjini ambao pia utafikisha maji kwenye Kijiji cha Mkididili, Buhororo, Kumuyange, pamoja na Nyamiaga. Ninawashukuru sana kwa kuidhinisha hiyo fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa, napenda kuwashukuru Serikali ya Uingereza, Balozi wa Uingereza pamoja na mtu anaitwa Eng. Lukas Kwezi, kwanza kwa kubuni mradi wa nyumba ni choo, lakini kwa kubuni mradi wa RBF (Result-Based Financing). Kwa Jimbo la Ngara peke yake kupitia ubunifu wa hii miradi na ruzuku walizotupatia kama Taifa, tumepata takribani shilingi milioni 604 kwenye awamu iliyopita ya mgawanyo wa fedha za RBF.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumwomba ndugu yangu Eng. Lukas Kwezi aendelee kuwa na ubunifu huu na kwa vile mradi huu unakaribia kufika mwisho, basi aweze kubuni mradi mwingine wa miaka mitano ili katika kipindi changu cha miaka mitano cha kuongoza Jimbo la Ngara niendelee kupata mgao kama huu kila mwaka ili niweze kuondokana na changamoto za maji zilizoko kwenye Jimbo la Ngara. Napenda pia kushukuru, nimeona ukurasa wa 154 orodha ya miradi iliyotengewa fedha na Wizara ya Maji kwa ajili ya Jimbo la Ngara, kwa kweli ninashukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nielekeze mchango wangu kwenye upande wa usimamizi endelevu wa rasilimali za maji. Waheshimiwa Wabunge waliotangulia hapo nyuma kabla yangu, wameeleza changamoto nyingi zilizopo kwenye usimamizi wa miradi ya maji. Nami naomba hapa Wizara ya Maji mnisikilize vizuri, nina uzoefu kwenye kutengeneza hizo CBUWSO ambazo ndiyo Kamati za Maji na kuzisimamia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kimuundo wa hizi CBWSO kuna tatizo la social setup. Maeneo mengine ni ngumu kutenganisha uongozi wa Kamati ya Maji pamoja na Uongozi wa Serikali ya Kijiji. Maeneo mengine utakuta Mwenyekiti, Katibu na Mweka Hazina wa Kamati ya Maji wana undugu na Serikali ya Kijiji. Hivyo, hata kwenye uwajibikaji wao inakuwa ni ngumu. Hata mimi Mbunge siwezi kukubali Kamati ya Maji iwajibishwe wakati Kamati hiyo hiyo ukitaka kuiwajibisha ni kama vile unawajibisha wapigakura wangu walionichagua kwenye kile kijiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwaomba Wizara ya Maji waje na model nyingine ya kusimamia miradi ya maji vijijini inayoitwa Franchise Model. Sina Kiswahili cha jina hilo, lakini Franchise Model ni utaratibu wa kusimamia miradi ya maji kwa kuwapa mikataba watu binafsi au kampuni ziweze kuendesha ile miradi ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hii nchi kuna double standard kama mjini kuna Watanzania na vijijini kuna Watanzania, halafu mjini zimepewa kusimamia maji kama DUWASA na DAWASA, halafu vijijini tumeachiwa sisi wananchi wenyewe tusimamie miradi yetu ya maji. Haya mambo hayakubaliki kwa sababu kama wanatuachia sisi wananchi hatuna mafunzo, hatuna wataalam, tunawezaje kusimamia miradi hii ya maji ambayo ni uwekezaji mkubwa, fedha ya Serikali inaingia pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Wizara ya Maji waruhusu RUWASA iweze kuwapa mikataba makampuni binafsi ama watu binafsi wenye uwezo wa kuendesha hii miradi ya maji. Ni rahisi kumwajibisha mtu binafsi, pump ikikataa kufanya kazi, bomba likikatika ama tape ikavunjika ni rahisi kwenda kumwajibisha mtu binafsi ama kampuni binafsi kuliko kuwawajibisha wananchi ambao ndio wasimamizi wa hiyo miradi ya maji. Hilo naomba lieleweke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nielekeze mchango wangu pia kwenye kitu kinaitwa Mfuko wa Maji wa Taifa yaani National Water Fund. Maji unayoyaona tunayoyatumia yana sehemu mbili, ukishachukuwa maji ukayatumia, asilimia kubwa ya maji yanayotumika yanageuka kuwa maji taka yaani waste water. Maji taka haya ni yale tunayotumia vyooni, ni yale tunayotumia bafuni na asilimia 80 ya maji yote unayopeleka nyumbani yanabadilika na kuwa maji taka.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Taifa wa maji una jina ambalo haliakisi mnyororo mzima wa maji. Jina lake ni National Water Fund, nawaomba sana Wizara Maji mwende mkabadilishe hili jina kutoka National Water Fund kwenda kuwa National Water Fund and Sanitation yaani Mfuko wa Maji wa Taifa na Usafi wa Mazingira. Hapo tutakuwa tumeakisi ile sehemu ya pili ya matumizi ya maji ambayo maji mengi yanaenda kubalika na kuwa maji taka.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji taka uwa tunayahifadhi vyooni hasa yale tunayoyatumia vyooni na tunayahifadhi kwenye septic tank, maji mengine ambayo ni maji taka ni yale yanayotoka jikoni. Tunavyoyahifadhi haya maji kwenye septic tank zile septic tank zina tumika na baadaye zinajaa. Ukienda ukachukua sampuli ya maji taka kwenye septic tank vyooni ukiyapima unakutana na virusi zaidi ya laki moja, unakutana na protozoa zaidi ya elfu 10, unakutana na virus protozoa pamoja na bakteria, wadudu wengi wako kwenye yale maji taka, ndio maana kuna umuhimu wa kuwekeza fedha kwenye usimamizi endelevu wa maji taka ili…(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashusha nondo na najua watanitafuta ili niwaongezee nondo. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa kupiga makofi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee, yale maji taka yale kwenye maeneo ya mijini ambako kuna mifumo ya sewerage yaani ya sewer system, vyoo vile vinaunganishwa kwenye ile mifumo na yale maji yanaenda kutibiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye maeneo ya miji inayokuwa hasa kwenye Jimbo langu la Ngara, Mji wa Rulenge na Mji wa Ngara Mjini hata hapa Dodoma, maji haya yapo kwenye septic tank yanahitaji kuchukuliwa na magari yanayokwenda kufyonza yale maji na kwenda kuyapeleka kwenye mifumo ya kuyatakasa ili maji hayo yanapotolewa kwenye ile mifumo yawe pathogens free yaani yasiwe na hao wadudu niliowataja na maji hayo hata tukuyaruhusu yakarudi ardhini yanakuwa hayawezi kuchafua maji yaliyoko chini ya ardhi yaani underground water. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndio maana naishauri Wizara ya Maji kubadilisha jina la Mfuko kutoka kuwa kwenye Mfuko wa Maji wa Taifa kuwa kwenye Mfuko wa Maji na Usafi wa Mazingira wa Taifa na matumizi ya fedha iliyoko kwenye huo Mfuko yaweze kuwekezwa kwenye kusimamia hayo maji taka ili tuweze kuondoa magonjwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisikia milipuko mjini ujue ni hayo maji taka yaliyosambaa. Ukisikia magonjwa kama kipindupindu na mengine ya kuhara ujue ni haya maji yameachiliwa, yametapakaa mijini yanaleta magonjwa kwa wananchi. Ndio maana siku ya leo nachukua fursa hii kuwaomba Wizara ya Maji na kuwashauri kabisa kwa namna ya kipekee, mgawanyo wa fedha za Mfuko wa Maji na Usafi wa Mazingira, nimeshaanza kuuita hivyo, ziende kwenye maji safi na ziende kwenye kusimamia maji taka.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba Wizara ya Maji iwekeze kwenye mifumo ya kisasa ya kutibu maji taka inaitwa Faecal Sludge Treatment System, haina Kiswahili sijawahi kukisikia, lakini kuna mfumo mwingine unaitwa Decentralized Waste Water Treatment System (DEWATS). Hii nayo

NAIBU SPIKA: Hiyo Mheshimiwa…

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, hii nayo haina Kiswahili chake.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ndaisaba hiyo ungekuwa umemwona Mheshimiwa Maige kabla angekupa tafsiri hiyo. (Makofi)

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia na kwenye kamusi sijaona, naomba unisamehe.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kuchangia kwamba, Wizara ya Maji iwekeze kwenye kujenga hiyo mifumo ili katika sehemu nyingi katika nchi hii ambapo septic tank zinajaa, wananchi waweze kwenda kunyonya vyoo vyao na wapeleke maji taka hayo yaende kutibiwa kwenye hiyo mifumo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba Wizara itakapoanza kutekeleza haya mawazo yangu, Jimbo langu la Ngara liwe la kwanza kupewa allocation kwa sababu hizi nondo nimezileta mimi na Wizara itakapoanza kufanyia kazi mchango wangu sisi jimbo la Ngara tuweze kupewa kipaumbele. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ruhoro kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Agnes Hokororo.

MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nataka kumpa taarifa mzungumzaji hilo neno alilosema tiritimenti, kwa lugha ile ya kwetu ni treatment. Ahsante. (Makofi/Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, malizia sekunde thelathini.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli mchango wake, sijui nini hiyo aliyoitoa nimeikataa, kwa sababu mimi ningemuambia ataje Faecal Sludge Treatment System asingeliweza kutaja, kwa hiyo naikataa. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa, naomba mawazo yangu mawili hayo Wizara ya Maji iweze kuyachukua na iende ikayafanyie kazi hasa hili la kubadilisha jina la Mfuko wa Maji wa Taifa

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: lakini vilevile na kwenye mifumo ya usimamizi endelevu wa miradi ya maji yaani Kamati za Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)